Tuesday, December 18, 2012

CHIKAWE AFUNGUA WARSHA YA VIONGOZI WA DINI KUHUSU NAFASI YA DINI KATIKA KULINDA NA KUDUMUSHISHA AMANI NCHINI



Baadhi ya washiriki
Mhe. Mathias Chikawe (MB) Waziri wa Katiba na Sheria (wa pili kuumeni)  leo tarehe 18/12/2012 akifungua Warsha ya Viongozi wa Dini kuhusu nafasi ya Dini katika kulinda na kudumisha amani Nchini.
 Baadhi ya viongozi wa Dini katika Picha na Mhe. Chikawe
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Uhalifu wa Kivita, Uhalifu dhidi ya Binadamu na aina zote za Ubaguzi wakiwa kwenye picha na Mhe. Chikawe.


Mhe. Mathias Chikawe (MB) Waziri wa Katiba na Sheria leo tarehe 18/12/2012 amefungua Warsha ya Viongozi wa Dini kuhusu nafasi ya Dini katika kulinda na kudumisha amani Nchini. 
Warsha hiyo iliandaliwa na Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Uhalifu wa Kivita, Uhalifu dhidi ya Binadamu na aina zote za Ubaguzi ambayo iko chini wa Wizara ya Katiba na Sheria. 
Warsha hiyo ina lengo la kuyajengea uwezo makundi mbalimbali katika jamii na kuleta uelewa wa ujumla wa wananchi kuhusu vyanzo, madhara na namna ya kuzuia mauaji ya kimbari, hii ni pamoja na kupinga vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na ubaguzi, matamshi ya kichochezi na kunyamazia mambo kwa vyombo husika. 
Mhe Chikawe aliwataka viongozi wa Dini zote kuendelea kukemea vitendo vya kibaguzi, vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani. 
Pia kutumia warsha hiyo kubaini na kujadili kwa amani vyanzo vya chokochoko za kidini zilizoanza kujitokeza hivi karibuni na kutafuta majibu ya njia za kuzuia.

Kamati ya Kitaifa kuzuia Mauaji ya Kimbari kama inavyojulikana kwa kifupi ilizinduliwa Februari 2012 na chimbuko lake ni Protokali ya Umoja wa Nchi za Maziwa Makuu ya kuzuia mauaji ya Kimbari ambayo  inazitaka Nchi zote za Umoja wa Maziwa Makuu ziunde Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia mauaji ya kimbari. Tanzania iliunda Kamati hiyo Februari 2012, Kenya Machi 2012 na Uganda Oktoba 2012. Kamati hiyo inafanya kazi kwa karibu sana na Sekretarieti ya Maziwa Makuu na Ofisi ya Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari.





No comments:

Post a Comment