"...Basil, kusanyeni kodi... hata hao wakubwa IMF na World Bank nao wanawahimiza ...'kusanyeni kodi'...!" Haya ni baadhi tu ya maneno mengi ambayo nakumbuka Mwalimu Julius Nyerere aliyasema siku ile ya Mei Mosi 1995 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya. Alikuwa akiwakumbusha viongozi wa serikali, akimtaja Waziri wa Basil Mramba (Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati huo), kwamba wanapaswa kukusanya kodi kwa bidii ili kuleta maendeleo.
Naam, wajumbe wenzangu. Leo nilishuka mtini, asubuhi na mapema. Nikabahatika kumsikiliza Waziri wa Hazina, Daktari William Mgimwa, akizungumzia masuala ya jimboni kwake. Lakini akazungumza kwamba Serikali ina fedha za kutosha kuendesha majukumu yake.
Hili kidogo limenitia shaka, shaka yenyewe si ndogo, ni kubwa kwa sababu, tunaona jinsi mfumuko wa bei ulivyo, namna huduma muhimu za kijamii zinavyosuasua kama siyo kukosekana kabisa. Shule zinakosa chaki, dawa hazitoshi, mishahara ya watumishi inachelewa, halafu tutasemaje kwamba serikali ina fedha?
Ni aibu kutamka hadharani hivyo (pengine kwa masuala ya kiusalama zaidi), lakini inatisha inapofikia hatua hata wafanyakazi wa majeshi ya usalama wanacheleweshewa mishahara yao kwa sababu serikali haina fedha.
Tatizo kubwa lililopo hapa ni kwamba, serikali na idara zake hazikusanyi kodi! Kusanyeni kodi, kama Mwalimu Nyerere alivyohimiza! Lakini wote wamelala, hakuna walau anayesinzia anayeweza kugutuka. Wanakoroma hawana habari na maslahi ya nchi yetu.
Usingizi wenyewe umewachukua kiasi cha kuota namna ya kutunisha mifuko yao na waja wao, siyo Watanzania wengine akina siye. Wamekuwa maswahiba wakubwa wa wafanyabiashara wanaowajaza mapesa mifukoni mwao badala ya kupeleka Hazina. Wafanyabiashara hao, ambao wanapaswa kulipa kodi ya mabilioni ya shilingi, wakiwapelekea vimilioni kadhaa wateule hawa wanakoroma, wanalala fofofo.
Mbaya zaidi, wateule wetu wenyewe nao wamegeuka wafanyabiashara, no hapana, wajasirimali wakubwa kwa kutumia nafasi zao ambazo mishahara yao inatokana na kodi zetu.
Kwa uroho wao na ulafi, wafanyabiashara wameigeuza serikali yetu kama ya shemeji yao! Wanafanya watakavyo, wanakwepa kodi mbele ya TRA na vyombo vingine, mwisho wa siku fedha zimejaa mifukoni mwa watu badala ya kuwa serikalini. Utafika wakati ambapo Serikali inabidi ikakope kwa akina Mbega Mnyama, maana Hazina hakuna fedha ati!
Taarifa zilizopo ni kwamba, hivi sasa uwezo wa serikali ni kukusanya Shs bilioni 300 tu hivi kwa mwezi. Lakini wachambuzi wa mambo ya uchumi wanasema, uwezekano uliopo serikali ilipaswa kukusanya Shs trilioni mbili hadi tatu kwa mwezi ikiwa wafanyabiashara wote wangeondoa ushemeji na kulipa kodi inavyostahili. Kwa msingi huo uchumi wetu ungepanda.
Wajumbe wenzangu, napata hasira wakati mwingine ndiyo maana naamua kubakia mtini tu, nijifiche na unafiki na uzandiki wa waheshimiwa hawa tuliowapa dhamana. Kwa nini TRA hawakusanyi kodi? Kwa nini tunachekelea kupewa misaada kila mwaka wakati tunao uwezo wa kukusanya fedha nyingi?
Niseme tu ukweli, nazifagilia serikali za Mwalimu Nyerere na Ben Mkapa, hali ilikuwa ngumu lakini kodi ilikusanywa. Hakukuwa na ushemeji. Ninaota, ni ndoto ingawa ndoto si pato, kwamba ipo siku tutampata kiongozi bandidu ambaye atasimamia kwa fimbo ya chuma kuhakikisha tunakusanya kodi! Vinginevyo, ni aibu sana kwa Rais kutembeza bakuli kuomba misaada huku bakuli lenyewe limetoboka!
Ni mtazamo wangu binafsi, washkaji msije mkanitoa roho bure,
Wasaalam,
Mbega Mnyama
0655-220404
0 comments:
Post a Comment