WATANZANIA
taratibu wameanza kuona kama ni mchezo wa kuigiza au mazoea pale kila
baada ya muda fulani tukio la kulipuka kwa bomu katika kanisa au sehemu
ya mkusanyiko au kwenye mkutano wa kisiasa kama ni jambo la kawaida.
Imefikia
mahali kwamba milipuko ya mabomu inaanza kuonekana kama ni sehemu ya
utamaduni wetu kwa kukubali kwa kirahisi watu wenye dhamira ovu na
katili ya kutaka kuangamiza binadamu wenzao pasipo sababu ya msingi na
hata kama mtu ana sababu ya msingi kuelezea hisia zake juu ya jambo
fulani lakini si kwa njia ya kutoa roho ya mtu mwingine.
Imekuwa
kama mazoea kwa baadhi ya makundi ya watu kutumia imani (dini) kuelezea
hisia zao kali kwa kushambulia sehemu ya imani nyingine hii kwa kweli
kwa jamii iliyostarabika haikubaliki hata kidgo tena kwa watanzania
waliozoea kuishi pamoja bila kujali tofauti zao za rangi, dini, kipato,
itikadi au tofauti zozote wamekuwa wamoja tangu uhuru.
Na
ndugu msomaji watanzania hawa wamekuwa wamoja tangu enzi na enzi na
waasisi wa taifa hili yaani Baba wa taifa, Mwl Julius Nyerere na Mzee
Abeid Amani Karume waliweza kwa nguvu zao zote kuwaunganisha watanzania
na kuwa kitu kimoja bila mifarakano yoyote ndani ya jamii.
Sisi
Moblog tunapenda kuchukua nafasi kuwaambia watu, mtu au kikundi cha
watu au magaidi kwamba watashindwa kwa nguvu ya dola na Mwenyezi Mungu
kwa mipango yao ya kiovu kutaka kutoa roho za watu wasio kuwa na hatia.
Lakini
kama kuna kikundi cha watu kinajificha kwenye kichaka cha imani kutaka
kuelezea hisia zao kwa kuwaua watu wengine yaani watu wenye misingi au
imani kali za kidini(Religious Fanaticism) kwa kweli ni upofu wa
kutokuona mbali kabisa lakini vyombo vya dola lazima viwajibike haraka
na kuwashughulikia kwa ukamilifu vikundi au kikundi kama hivi hapa
nchini.
Tunasema
mapema kwa kuvikumbusha vyombo vya dola kwa sababu imani kali za
kidini zikiachwa kama ule msemo usemao ‘mchelea mwana kuliwa matangani’
kama kule Nigeria ambapo kikundi cha kigaidi cha Boko Haram
kinavyowatesa wananigeria na viongozi wao.
Tumesema
hayo tukijua kwamba juzi tu mtu mmoja amejeruhiwa baada ya kulipukiwa
na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kwenye kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Ziwa
Victoria, Makongoro Misheni, Mwanza.
Ambapo
aliyejeruhiwa ni mhudumu wa nyumba ya wageni ya kanisa hilo, Benadeta
Alfred (25) aliyekumbwa na mkasa huo juzi saa mbili usiku.
Huo
ukiwa ni muendelezo wa matukio kama hayo katika sehemu mbalimbali hapa
nchini hususani jijini Arusha chonde chonde Jeshi la Polisi nchini
chukueni hatua mapema ya kudhibiti hali hii isifike mahali tukajuta kama
nchi na watu wake.
Naomba kuwasilisha
Damas Makangale
Mhariri Mkuu MOblog Tanzania
0 comments:
Post a Comment