Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
. Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Mzee Hassan Nassor Moyo
amesema wajumbe wa CCM ndani ya Bunge la Katiba wanatakiwa kujiuliza
sababu zilizolifanya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
kutoka nje ya Bunge na ndipo watafute suluhu.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu kutoka Zanzibar,
Moyo alisema haitoshi kwa wajumbe wa CCM na wale wa kundi la 201,
kuendelea na mijadala bila kukaa chini na kutafakari kwa nini Ukawa
wametoka na hatima yake ni nini ndipo wajisahihishe.
“Hii hali ya mgawanyiko si nzuri hata kidogo.
Kinachoendelea hakileti mantiki kwani kutengeneza Katiba ni kwamba, kila
jambo linafanyika kwa maridhiano. Sasa hawa wako ndani hawa wako nje,
ina maana wanataka kutupa Katiba yenye mpasuko?” alihoji Mzee Moyo.
Alisema kuwa kutoka nje ya mkutano wowote si jambo
geni, kwamba ikiwa upande mmoja utaona mambo hayaendi inavyotakiwa,
unatoka kwa sababu hakuna kinachokufanya uendelee kukaa.
“Haya mambo hayakuanza leo, hata wakati nikiwa
mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria Zanzibar, katika mikutano ya pamoja
na Hizbu, ZNP, ZPP na ASP wajumbe wa ASP waliwahi kutoka nje kwa kupinga
mwenendo wa mkutano.
“Katika mkutano lazima watu waelewane, wakae
mstari mmoja ndipo mambo yaende. Siasa ni mapambano na hakuna kuogopa.
Lazima kusimamia pale mtu anapopaamini na kutambua mambo yanavyoendeshwa
ama ndani au nje ya mstari,” alisema.
Hata hivyo, Mzee Moyo alielezea kuchukizwa na
mipasho, kejeli, kebehi na vijembe ndani ya chombo hicho muhimu cha
kutengeneza Katiba ya Tanzania.
“Hawa wamepewa jukumu la kutengeneza katiba,
lakini inasikitisha wanatuletea mambo yao hapa. Wanapashana, matusi,
kejeli kwani hayo ndiyo tuliyowatuma? Pale tumewapa kazi ya
kututengenezea Katiba ya Watanzania kwa maendeleo ya Tanzania, kwa kweli
imenisikitisha sana,” alisema.
Kwa upande mwingine, alimshutumu mjumbe wa Bunge
hilo, Mohamed Seif Khatib kwa kutumia muda mwingi kumshambulia, Makamu
wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Shariff Hamad badala ya kujadili
kilichompeleka bungeni.
“Badala ya kuchangia yake anamjadili Maalim Seif,
inamhusu nini? Ya nini hayo wakati mambo yalishapita. Kwa kweli
imenikera hasa kwa mtu mzima kama yule kujadili ya kale. Pale tunataka
Katiba, azungumze yanayotokana na mkutano ule,” alisema.
Juzi wakati akiwasilisha hoja zake, Khatib
alitumia muda mwingi kumshambulia Maalim Seif hasa katika utendaji wake
hata kutimuliwa kwake katika chama na Serikali pamoja na watumishi
wengine.
“Tunataka yeye (Khatib) na hata wengine,
wazungumze yanayohusu mkutano huo, lakini si ya Maalim Seif, si ya Aboud
Jumbe hayana faida leo, hayo yameshapita. Sasa kama alikuwepo wakati
huo na kilimuuma, si angemtetea Maalim Seif palepale kusema anaonewa.
“Alikuwa na nafasi katika Serikali, alikuwa na uwezo wa
kuwasilisha hoja za kumtetea, hakufanya hivyo, leo anakuja kutusimulia.
Sasa tufanye nini, haina maana. Hayo yameshatokea, tuyaache yabaki
kumbukumbu tu.
“Hata mimi nilipokuwa Waziri wa Kilimo, kuna jambo
lilitokea na Maalim akiwa Waziri Kiongozi alitaka kunishtaki, lakini
imebaki historia. Ya nini kuweka nongwa leo bado niko naye na tunafanya
kazi. Khatib ameonyesha upungufu wake, haina maana hata kidogo.
Azungumzie yaliyompeleka pale,” alisema Mzee Moyo.
Chanzo:Mwannchi
Chanzo:Mwannchi
0 comments:
Post a Comment