Wednesday, May 7, 2014

UTAFITI TWAWEZA WAANIKA UOZO KATIKA VITUO VYA AFYA NCHINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Ni mtu mmoja kati ya watu 20 wenye umri zaidi ya miaka 60, na mtoto mmoja kati ya watano wenye umri chini ya miaka mitano wanaopata huduma na matibabu bure, kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Twaweza.
Idadi hiyo kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 60 ni sawa na asilimi sita tu, wakati idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni asilimia 18 tu kwa mujibu wa utafiti huo.
Awali, mpango wa Serikali ni kutoa bure huduma kwa wagonjwa wa nje kutoka makundi hayo mawili.
Taasisi ya Twaweza ilifanya utafiti wake kwa makundi hayo walioupa jina la Je, Vituo vya Afya Vipo kwa Ajili ya Kuwahudumia Watu? Wananchi na Watumishi wa Afya Wazungumzia Huduma za Afya.
Taarifa ya muhtasari huo, kwa mujibu wa Twaweza, umetokana na takwimu kutoka sauti za wananchi, utafiti kwa njia ya simu za mkononi na wenye uwakilishi wa kitaifa uliofanyika kwenye kaya zote Tanzania Bara.
Inasema huduma za afya ni muhimu kwa kuwa zinahitajiwa na wananchi wengi. Zaidi ya nusu ya Watanzania ambao ni sawa na asilimia 57, waliotembelea vituo vya afya kati ya Mei na Juni 2013, walikwenda kwenye vituo hivyo kwa dhumuni la kutibiwa au kumsindikiza mgonjwa.
Waliohojiwa ambao ni sawa na asilimia 77, walitembelea zaidi vituo vya afya vya Serikali kuliko vya binafsi au vya dini.
Wengine ambao ni sawa na asilimia 63 wanaamini kuwa Serikali inashughulikia vibaya suala la uboreshaji wa huduma za afya. Upatikanaji wa huduma za afya, pia hutegemea watumishi na upatikanaji wa dawa.
Taarifa hiyo inasema kuwa Septemba 2013, Sauti za Wananchi iliripoti kuwa wagonjwa ambao ni sawa na asilimia 41, hawakupata dawa kwenye vituo vya afya.
Utafiti umebaini pia kuwa zahanati na vituo vya afya vina upungufu mkubwa wa wafanyakazi na sehemu kubwa vinaendeshwa vikiwa na nusu ya idadi ya watumishi tofauti na ilivyopendekezwa na Serikali kwa watumishi wa kada za waganga na wauguzi.
Kwa upande mwingine, theluthi moja ambayo ni sawa na asilimia 31 ya watoa huduma za afya, hawakuwepo vituoni wakati vituo hivyo vilipotembelewa na pia ilibainika kuwa hawakutoa taarifa ya kutofika kwao kazini.
Upungufu wa watumishi walioajiriwa na kutokuwepo kwao kazini, vinaweza kusababisha wagonjwa kusubiri kwa muda mrefu na wakati mwingine kupata huduma duni.
Wagonjwa wengine ambao ni sawa na asilimia 70 wanaotembelea vituo vya afya vya Serikali, wanalazimika kusubiri kwa zaidi ya dakika 30 ndipo wahudumiwe, tofauti na vituo binafsi ambavyo inaelezwa kuwa nusu ya asilimia 45 ya wagonjwa husubiri kwa muda huo huo.
Vilevile, wagonjwa ambao ni sawa na asilimia 53 ya wagonjwa wote wanaotembelea vituo mbalimbali vya afya, hulazimika kusafiri kwa zaidi ya dakika 30 kukifikia kituo cha afya.
Akizungumzia hali hiyo, Elvis Mushi, mtafiti kutoka Twaweza alisema: “Wagonjwa wananyimwa haki zao za kupata huduma kikamilifu za kiafya kutokana na uhaba wa dawa muhimu, upungufu wa wafanyakazi na utoro wa watumishi.”
Naye mkuu wa taasisi ya Twaweza, Rakesh Rajani alisema kuwa wazee na watoto wanaumia kwa sababu Sera hazitekelezwi.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment