Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
mstaafu Joseph Warioba amesema wajumbe wa kundi la walio wengi
linaloundwa na wabunge wa CCM na baadhi ya 201 katika Bunge la Katiba
hawawezi kupitisha Katiba kwa kuwa hakuna maridhiano.
Jaji Warioba aliyasema hayo juzi usiku katika
Kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV na kusema kuwa
lazima kuwapo na maridhiano.
Kauli hiyo imekuja baada ya kuwapo na kauli
mbalimbali zinazosema kuwa akidi iliyopo ya wajumbe wa Bunge la Katiba
inaweza kupitisha uamuzi wowote kwa mujibu wa Sheria za Marekebisho ya
mabadiliko ya Katiba.
“Kwanza kilichotokea wajumbe walisahau kufanya
kama ilivyokuwa kwenye tume, sisi tuliweka pembeni itikadi za vyama na
kuweka mbele utaifa lakini Dodoma watu waliingiza siasa na kuanza
kushindana,” alisema Warioba na kuongeza:
“CCM imeamua kupitisha yao, wale wengine
wanatafuta njia ya kuzuia wasipate wingi wa kura na kuna uwezekano bila
maridhiano tutapata matatizo katika mchakato...lazima kuwapo na
maridhiano.”
Jaji Warioba pia alitoa angalizo kuhusu kutokuwapo
kwa maridhiano, “Lakini kama wakienda hivi walivyopanga, wanaweza
kukwama tu...haiwezi kupatikana Katiba kama kundi hili likipitisha,
kundi lingine litadai, lingine likifanya hivyo, hawa watalalamika,”
alisema.
Alisema awali Zanzibar iliingia katika matatizo na
kupelekea hata kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa ajili
ya kuleta utulivu kutokana na kusigana lakini kwa maridhiano
yakamalizika.
“Binafsi nina wasiwasi mkubwa na Zanzibar na hata
ukiangalia matusi yaliyokuwa yanaporomoshwa bungeni na Wazanzibari
siamini kama maridhiano yatakuwapo.” Jaji Warioba alirejea kusema kuwa
waliotoka bungeni kuna kila sababu ya kutafuta maridhiano nao kwa kuwa
wasiporidhiana hapatakuwa na Katiba nzuri yenye sura ya Watanzania.
“Kwa hali iliyopo ni vigumu kupata theluthi mbili
ya wajumbe kutoka Zanzibar watakaokubaliana na hoja zao, ni vigumu kwani
Wazanzibari wana mambo yao kwa hapa nisingependa tufikie huko ila
kinachotakiwa ni maridhiano ili tupate Katiba ya Watanzania,” alisema
Jaji Warioba.
Jaji Warioba aliwasisitiza wajumbe kufanye maboresho yaliyotoka kwa wananchi na yaliyopendekezwa na wao kuingizwa kwenye Katiba.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment