Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda Godfrey Nzowa akionyesha moja ya shehena kubwa ya dawa za kulevya za kulevya zilizokamatwa.
Huenda mwaka huu ukavunja rekodi ya kuwakamata watu
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwani ndani ya siku 120,
Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kimekamata
kilo 238 za aina mbalimbali za dawa hizo.
Rekodi hii ni kubwa kuliko ya kiasi cha dawa cha kilo 54 kilichokamatwa kwa mwaka jana.
Kitengo hicho kimekuwa kikiwatia nguvuni watu wanojihusisha na uangizaji au usafirishaji kwa njia mbalimbali
Tangu kuanza kwa mwaka huu, Januari hadi Aprili
30, kitengo hicho kimeeleza kukamata kilo 238 za kulevya zilizokuwa
zikisafirishwa kwa njia mbalimbali.
Kamanda wa Kitengo hicho, Godfrey Nzowa anasema kwa kipindi kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu, walikamata kilo 228 za heroin na kilo 10 za cocaine.
Anasema kati ya kilo 228, kilo 200 zilikamatwa
baharini na kilo 28 kwenye viwanja vya ndege huku kesi za watuhumiwa 17
zikiwa katika hatua mbalimbali mahakamani.
Kamanda Nzowa anasema mwaka 2012 walikamata jumla ya kilo 416 za dawa za kulevya, kati ya hizo kilo 265 ni za heroin na kilo 151 za cocaine.
Anasema: “Kati ya kilo 265 kilo 211 zilikamatiwa
majini na 54 kwenye viwanja vya ndege na mipaka ya Tunduma na Rusumo na
jumla ya washtakiwa wa dawa zote 416 walikuwa 39 na kati yao 21 ni raia
wa kigeni.
Kamanda Nzowa anasema mwaka 2013 walikamata kilo 54 kati ya hizo kilo 50 zilikuwa za heroin na kilo nne zikuwa za cocaine. Jumla ya watuhumiwa 44 walifikishwa mahakamani na hatua za kisheria zilichukuliwa kwa wahusika hao.
“Kutokana na kubaini mbinu ambazo wanazitumia,
tulihakikisha tunapambana nao ndio maana mwaka jana tulikamata kiasi
kidogo ukilinganisha na mwaka juzi. Hii inafanikiwa kutokana na
ushirikiano wa wananchi kwa kutoa taarifa wanapowabaini wasafirishaji,”
anasema Nzowa.
Mapambano dhidi ya udhibiti wa dawa za kulevya
nchini umeendelea kushika kasi nchini kwa lengo la kuhakikisha vijana
ambao ni taifa la kesho hawaathiriki na matumizi wa dawa hizo.
Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ikiwa ni
pamoja na kuboresha ulinzi kwenye uwanja wa ndege na njia za majini ili
kuwabaini waingizaji na wasafirishaji wa kwa njia mbalimbali.
Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la tatu la abiria
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es
Salaam mwezi uliopita, Rais Jakaya Kikwete alisema anashangazwa kuona
dawa za kulevya zinapita ovyo katika uwanja huo na ule wa Kilimanjaro
(KIA) huku watendaji wote wapo na zinakwenda kukamatwa Afrika Kusini.
Rais Kikwete alitoa agizo la kuwataka watendaji katika viwanja hivyo kuhakikisha wanakuwa makini ili dawa hizo zisiingie nchini.
Ugumu wa kazi
Kamanda Nzowa anasema vita ya dawa za kulevya
inahitaji wema na uadilifu wa hali ya juu kutokana na wahusika kuwa na
fedha za kutoa rushwa ili wasikamatwe.
Anasema watuhumiwa hao wako tayari kutoa kiasi chochote cha fedha ili wasikamatwe.
“Usipokuwa mwadilifu, vita hii hutoiweza. Mimi
hapa nina pata taarifa kutoka nchi mbalimbali duniani kutokana na
mtandao tuliojiwekea, lakini kama utapata taarifa halafu ukaweka mbele
tamaa ya fedha, hutaweza kupambana nao,” anasema Nzowa.
Anaeleza kuwa katika Biblia Zaburi 37:1-4 huku
akinukuu kitabu hicho kitakatifu kuwa “usikasirike kwa sababu ya watenda
mabaya. Usiwahusudu wafanyao ubatili”. Nzowa anafafanua kuwa amekuwa
akitumia maneno hayo kutotishwa na kushawishika kwa rushwa za waharifu
hao.
Matarajio ya baadaye
Kamanda Nzowa anasema vita ya dawa za kulevya
inahitaji ushiriki wa wananchi kutoa taarifa kila wanapowabaini
wahusika, ili hatua za haraka zichukuliwe dhidi yao. Anasema wamekuwa
wakitoa elimu katika shule, vyuo na jamii kuhusu madhara ya matumizi ya
dawa za kulevya na jinsi ya kuziepuka.
“Unapomwelimisha mtu madhara ya dawa hizi na
akielimika siku akiona mtu anajihusisha na kuuza au kusafirisha, ni
lazima atatoa tu taarifa na sisi tunawachukulia hatua kali.
“Vijana ndio waathirika wakubwa wa dawa hizi na
jamii itambue kuwa taarifa watakazozitoa, zinafanyiwa kazi lakini pia
tunawalinda watoa taarifa wetu kwa hali yeyote ili wahusika
wasiwabaini,” anasema Kamanda Nzowa
Wadau wazungumza
Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii
(ESRFTZ), Dk Oswald Mashindano anasema vita ya dawa za kulevya nchini
inaweza kumalizika tu iwapo viongozi wa nchi watajisafisha.
Anasema kushamiri kwa biashara hii kunatokana na
ukweli kwamba baadhi ya viongozi serikalini wasio waadilifu
wanajihusisha na biashara hii.
“Kila mtu atakwambia sababu mbalimbali kwanini
anafanya biashara hii ikiwemo, umaskini na kukosa ajira, lakini siyo
sababu ya kuwaacha kwani inaangamiza taifa,” anasema.
“Viongozi waache uoga katika matumizi ya sheria.
Wengi wanaingiza siasa katika masuala kama haya na kutotekeleza sheria
kali kwa kuhofia kunyooshewa mkono au kukosa kura,” anasisitiza.
Anaongeza kuwa viongozi wajenge uaminifu kwa jamii
na kuficha siri za raia wema ambao hujitokeza kuwafichua
wanaofanyabiashara hii. “Jamii inawafahamu wanaofanya biashara hii,
lakini inaogopa kuwa wazi kwa sababu hakuna uaminifu kwa viongozi, hasa
jeshi la polisi,” anaongeza.
Mratibu wa Mtandao wa Kimataifa wa Utekelezaji
Sheria na Virusi vya Ukimwi (LEAHN), Greg Denham anasema serikali
inatakiwa kupunguza madhara hasi yatokanayo na matumizi ya dawa za
kulevya kwa wananchi.
Anasema watu wanaotumia dawa za kulevya wamekuwa
wakikumbana na unyanyapaa, lakini wote wanahitaji msaada na huduma
muhimu za kibinadamu kama watu wengine. “Kama serikali ina mchakato wa
kuimarisha sera ya dawa za kulevya ni lazima kuhakikisha kwamba
watumiaji wa dawa hizo wanachukuliwa kama watu wenye matatizo ya kiafya
na wathaminiwe kama watu wengine,” anasema Denham.
Ofisa sheria wa Shirika la Madaktari wa Ulimwengu
(MdM), Lina Saguti anasema watu wanaotumia dawa za kulevya hukabiliwa na
changamoto za kisheria kabla na wakati wa kesi zao kuwa mahakamani.
Anasema mtumiaji wa dawa hizo anapokamatwa,
hatakiwi kupelekwa mahabasu bali anatakiwa kupelekwa katika kituo cha
tiba kwa lengo la kupata ushauri nasaha katika harakati za kumwokoa na
matumizi hayo.Ili vita hii ifanikiwe, Serikali na jamii inapaswa kuwa
upande mmoja wa mapambano tofauti na sasa.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment