Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Raymond Domayo, baba mzazi wa kiungo mkabaji Frank Domayo,
amesema fedha nono ndiyo zilizomshawishi mwanaye atimkie Azam FC, hivyo
amewataka viongozi na mashabiki wa Yanga wasimchukie badala yake
wamuunge mkono.
Domayo, ambaye alikuwa kiungo tegemeo wa Yanga
msimu uliopita, hivi karibuni alimwaga wino wa kuichezea Azam FC kwa
mkataba wa miaka miwili na kuvuna kitita cha Sh70 milioni.
Pia, kiungo huyo ambaye mkataba wake na Yanga
unatarajiwa kumalizika mwanzoni mwa Juni, atazoa Sh3 milioni kama
mshahara wake wa kila mwezi baada ya kujiunga na Azam.
Kwa upande mwingine, uamuzi huo wa Domayo kutimkia
Azam uliwakasirisha mashabiki wa Yanga, ambao wamekuwa wakiwashutumu
viongozi wao kwa kufanya uzembe uliosababisha kiungo huyo kuwakimbia.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Tabata
Kisiwani jana, Mzee Domayo aliwataka viongozi na mashabiki wa Yanga
kutambua kwamba soka ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, hivyo uamuzi
wa mwanaye umetokana na kupata masilahi mazuri na siyo kitu kingine.
“Nawaomba mashabiki wa Yanga wasimchukie mwanangu
kwani Azam amekwenda kwa sababu amepata masilahi mazuri zaidi ingawa
alikuwa anaipenda klabu ya Yanga.
“Ukweli ni kwamba soka ni kazi kama zilivyo kazi
nyingine. Leo hii unaweza kuwa hapa kesho ukahamia kwingine ambako
wanakupa masilahi mazuri,” alisema Mzee Domayo. Aliongeza: “Hata hao
mashabiki, ikitokea timu inawahitaji wakaishabikie leo hii halafu
watalipwa, unafikiri hawataenda? Ni wazi watakwenda kwa sababu ya fedha
hata kama wanaipenda klabu yao.
“Isitoshe mimi baba yake sina kazi kwa sasa, hivyo
namtegemea yeye na nina watoto wengine bado wanasoma,” alisema Mzee
Domayo, ambaye alidai ana taaluma ya udereva. Katibu mkuu wa Yanga, Beno
Njovu, akizungumzia kauli ya mzee huyo, alisema: “Hatuna tatizo na
Domayo kwa vile amehama Yanga na kwenda Azam kwa mapenzi yake, kwa sasa
tunajipanga.”
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment