Tuesday, May 6, 2014

WADAU,SERIKALI WANA MENGI YA KUFANYAKUNUSURU ELIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Hii ni wiki ya maadhimisho ya elimu. Wadau wa sekta hiyo kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa wamekuwa wakikutana kujadili hatima ya elimu nchini.
Maadhimisho ya wilaya na mikoa yaliyoanza tangu Mei 3, ni hatua kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufika kikomo Mei 10 mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, maadhimisho hayo ya kwanza kufanyika nchini pamoja na kutumika kama jukwaa la kuwakutanisha wadau wa elimu, yatatumiwa na serikali kutoa motisha kwa wanafunzi, shule na halmashauri zilizofanya vizuri katika taaluma.
Upi mtazamo wa wadau wa elimu kuhusu maadhimisho hayo? Mwananchi imewahoji baadhi ya  wasomi na wananchi wa kawaida wanaotoa maoni yao kuhusu maadhimisho hayo.
David Michael (Mkazi wa Buguruni mkoani Dar es Salaam)
Wiki hii inatakiwa kutumika kutafakari wapi tumekwama na kipi kifanyike ili tuweze kupiga hatua zaidi. Kwa miaka mingi tumekuwa tukijikita katika kulalamika na kubainisha mipango mbalimbali, lakini ukiangalia uhalisia hatupigi hatua kama tunavyopanga.
Serikali inatakiwa kutumia wiki hii kujichunguza, kwa nini wanafunzi wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma, kuhesabu na kuandika? Wapi tumekosea na kipi kifanyike?
Boniventure Godfrey (Meneja Idara ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Shirika la HakiElimu)
Suala la kutoa motisha ni jambo jema, lakini ni mapema sana kufanya hivyo. Tunatakiwa kuanza kwa kupanga mambo, ili baada ya miaka kadhaa tufurahie matunda hayo, lakini sio kuanza kupeana zawadi.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inatakiwa kuhakikisha inatoa sera mpya ya elimu kabla ya  kujipongeza. Hiyo itasaidia kufanikiwa kwa mipango yake kama vile Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
Naomba siku ya maadhimisho, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,  Dk Shukuru Kawambwa asimame na kuelezea changamoto zinazoikabili wizara yake na atoe mikakati ya kuitatua.
Wanajivunia kujenga shule, kuandikisha wanafunzi wengi shuleni, lakini je, wanapokwenda shule wanafunzi hao wanajifunza ipasavyo?

Dk Perpetua Urio (Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE)
Kitendo cha kuwazawadia wanafunzi waliofanya vizuri ni jambo jema, kwa kuwa linalenga hata walio pembeni nao wahamasike kusoma kwa bidii.
Kitendo cha kuangalia malengo yao ni jambo zuri litakalowapima kwa kipindi cha mwaka mmoja wamefanya nini  na wanatakiwa kupanga mikakati gani kusonga mbele.
Naishauri serikali kuitazama sekta ya elimu kwa jicho la tatu kwa kuhakikisha inaboresha mazingira ya walimu na kila palipo na upungufu ufanyiwe kazi.
Hii ni kwa kuwa hakuna taifa lolote duniani lililo endelea bila kuwekeza katika elimu. Serikali inatakiwa kuifanya sekta ya elimu kuwa kipaumbele chake cha kwanza.
Ofard Juma (mkazi wa Temeke mkoani Dar es Salaam)
Sekta ya elimu itapiga hatua endapo wadau kutoka sekta binafsi, vyombo vya umma na wazazi wataungana kwa pamoja. Katika wiki hii tunapojivunia ongezeko la shule, tuangalie pia jinsi ya kushirikisha wadau wa kada mbalimbali katika kutatua changamoto za elimu.
Profesa  Nerey Mvungi (Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)
Kutoa zawadi ni jambo jema, lakini linatakiwa kuangaliwa katika kada tofauti na sio moja. Zawadi hizo zinatakiwa pia kuelekezwa kwa walimu na shule ambazo zimefanya vizuri,  jambo litakaloamsha ari kwa walimu na shule kupambana ili mwaka mwingine wajitahidi nao wapate zawadi.
Ili shule zifanye vizuri zinatakiwa kuwa na uongozi imara na madhubuti utakaoweza kuwasimamia walimu na wanafunzi kila mmoja kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Ukiangalia idadi ya walimu wenye shahada imeongezeka, idadi ya wanafunzi nayo imeongezeka na wanafunzi wanaohitimu darasa la saba na kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka, hivyo tuimarishe kila sekta ili tusonge mbele zaidi.
 Kwa mfano, tunahitaji kuongeza maabara katika shule zetu, walimu tuwaboreshee mazingira lakini pia tuondoe changamoto zilizopo shuleni na vyuoni ili kuhakikisha kwamba elimu yetu inapiga hatua zaidi.

Dk Kitila Mkumbo (Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)
Wiki hii ni nafasi nzuri ya kutathmini tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Kwa miaka kadhaa sekta ya elimu imepiga hatua katika uandikishaji wa wanafunzi na walimu katika ngazi mbalimbali, lakini pia mwitikio wa wazazi na walezi katika kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule umeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Ni sawa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa imeongezeka, lakini je, wanapokwenda shule wanajifunza? Serikali inatakiwa kuwekeza katika ubora wa walimu kwa kuwasimamia ipasavyo katika ufundishaji na kuwawekea mazingira mazuri mahali pa kazi na makazi.
Aneth Samson (mkazi wa Tabata, Dar es Salaam)
Katika miaka ya hivi karibuni sekta ya elimu imepiga hatua hasa katika dhana nzima ya ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa shuleni na vyuoni.
Idadi hii ikiendelea kuongezeka kila mwaka bila kuhakikisha kuwa miundombinu ya madarasa, vyoo, vifaa vya kujifunzia na kufundishia iko ya kutosha, hakutakuwa na maana yoyote ya kujisifu kwa ongezeko hilo.
Tunatakiwa kuwaboreshea mazingira walimu hasa  wale wa maeneo magumu. Wiki hii itumike kujadili mambo yote haya na sio kufurahia vitu ambavyo kimsingi bado viko nyuma.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment