Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Hii ni wiki ya maadhimisho ya elimu. Wadau wa sekta hiyo kuanzia
ngazi ya wilaya na mikoa wamekuwa wakikutana kujadili hatima ya elimu
nchini.
Maadhimisho ya wilaya na mikoa yaliyoanza tangu
Mei 3, ni hatua kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yanayotarajiwa
kufika kikomo Mei 10 mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, maadhimisho hayo ya kwanza kufanyika nchini
pamoja na kutumika kama jukwaa la kuwakutanisha wadau wa elimu,
yatatumiwa na serikali kutoa motisha kwa wanafunzi, shule na halmashauri
zilizofanya vizuri katika taaluma.
Upi mtazamo wa wadau wa elimu kuhusu maadhimisho hayo? Mwananchi imewahoji baadhi ya wasomi na wananchi wa kawaida wanaotoa maoni yao kuhusu maadhimisho hayo.
David Michael (Mkazi wa Buguruni mkoani Dar es Salaam)
Wiki hii inatakiwa kutumika kutafakari wapi
tumekwama na kipi kifanyike ili tuweze kupiga hatua zaidi. Kwa miaka
mingi tumekuwa tukijikita katika kulalamika na kubainisha mipango
mbalimbali, lakini ukiangalia uhalisia hatupigi hatua kama tunavyopanga.
Serikali inatakiwa kutumia wiki hii kujichunguza,
kwa nini wanafunzi wanamaliza darasa la saba hawajui kusoma, kuhesabu na
kuandika? Wapi tumekosea na kipi kifanyike?
Boniventure Godfrey (Meneja Idara ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Shirika la HakiElimu)
Suala la kutoa motisha ni jambo jema, lakini ni
mapema sana kufanya hivyo. Tunatakiwa kuanza kwa kupanga mambo, ili
baada ya miaka kadhaa tufurahie matunda hayo, lakini sio kuanza kupeana
zawadi.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inatakiwa
kuhakikisha inatoa sera mpya ya elimu kabla ya kujipongeza. Hiyo
itasaidia kufanikiwa kwa mipango yake kama vile Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa.
Naomba siku ya maadhimisho, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa asimame na kuelezea changamoto
zinazoikabili wizara yake na atoe mikakati ya kuitatua.
Wanajivunia kujenga shule, kuandikisha wanafunzi
wengi shuleni, lakini je, wanapokwenda shule wanafunzi hao wanajifunza
ipasavyo?
Dk Perpetua Urio (Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE)
Kitendo cha kuwazawadia wanafunzi waliofanya
vizuri ni jambo jema, kwa kuwa linalenga hata walio pembeni nao
wahamasike kusoma kwa bidii.
Kitendo cha kuangalia malengo yao ni jambo zuri
litakalowapima kwa kipindi cha mwaka mmoja wamefanya nini na wanatakiwa
kupanga mikakati gani kusonga mbele.
Naishauri serikali kuitazama sekta ya elimu kwa
jicho la tatu kwa kuhakikisha inaboresha mazingira ya walimu na kila
palipo na upungufu ufanyiwe kazi.
Hii ni kwa kuwa hakuna taifa lolote duniani lililo
endelea bila kuwekeza katika elimu. Serikali inatakiwa kuifanya sekta
ya elimu kuwa kipaumbele chake cha kwanza.
Ofard Juma (mkazi wa Temeke mkoani Dar es Salaam)
Sekta ya elimu itapiga hatua endapo wadau kutoka
sekta binafsi, vyombo vya umma na wazazi wataungana kwa pamoja. Katika
wiki hii tunapojivunia ongezeko la shule, tuangalie pia jinsi ya
kushirikisha wadau wa kada mbalimbali katika kutatua changamoto za
elimu.
Profesa Nerey Mvungi (Mkuu wa Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)
Kutoa zawadi ni jambo jema, lakini linatakiwa
kuangaliwa katika kada tofauti na sio moja. Zawadi hizo zinatakiwa pia
kuelekezwa kwa walimu na shule ambazo zimefanya vizuri, jambo
litakaloamsha ari kwa walimu na shule kupambana ili mwaka mwingine
wajitahidi nao wapate zawadi.
Ili shule zifanye vizuri zinatakiwa kuwa na
uongozi imara na madhubuti utakaoweza kuwasimamia walimu na wanafunzi
kila mmoja kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Ukiangalia idadi ya walimu wenye shahada
imeongezeka, idadi ya wanafunzi nayo imeongezeka na wanafunzi
wanaohitimu darasa la saba na kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka,
hivyo tuimarishe kila sekta ili tusonge mbele zaidi.
Kwa mfano, tunahitaji kuongeza maabara katika
shule zetu, walimu tuwaboreshee mazingira lakini pia tuondoe changamoto
zilizopo shuleni na vyuoni ili kuhakikisha kwamba elimu yetu inapiga
hatua zaidi.
Dk Kitila Mkumbo (Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)
Dk Kitila Mkumbo (Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)
Wiki hii ni nafasi nzuri ya kutathmini tulikotoka,
tulipo na tunakokwenda. Kwa miaka kadhaa sekta ya elimu imepiga hatua
katika uandikishaji wa wanafunzi na walimu katika ngazi mbalimbali,
lakini pia mwitikio wa wazazi na walezi katika kuhakikisha watoto wao
wanakwenda shule umeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Ni sawa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa
imeongezeka, lakini je, wanapokwenda shule wanajifunza? Serikali
inatakiwa kuwekeza katika ubora wa walimu kwa kuwasimamia ipasavyo
katika ufundishaji na kuwawekea mazingira mazuri mahali pa kazi na
makazi.
Aneth Samson (mkazi wa Tabata, Dar es Salaam)
Katika miaka ya hivi karibuni sekta ya elimu
imepiga hatua hasa katika dhana nzima ya ongezeko la wanafunzi
wanaoandikishwa shuleni na vyuoni.
Idadi hii ikiendelea kuongezeka kila mwaka bila
kuhakikisha kuwa miundombinu ya madarasa, vyoo, vifaa vya kujifunzia na
kufundishia iko ya kutosha, hakutakuwa na maana yoyote ya kujisifu kwa
ongezeko hilo.
Tunatakiwa kuwaboreshea mazingira walimu hasa
wale wa maeneo magumu. Wiki hii itumike kujadili mambo yote haya na sio
kufurahia vitu ambavyo kimsingi bado viko nyuma.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment