Home » » WAFANYAKAZI STRABAG SASA WAREJEA KAZINI

WAFANYAKAZI STRABAG SASA WAREJEA KAZINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Ujenzi,Dk.John Magufuli.
 
Mgomo wa wafanyakazi wa kampuni ya Strabag inayojenga barabara katika mradi wa magari yaendayo kwa kasi jijini Dar es Salaam (Darts) ulimalizika jana na kurejea kazini.
NIPASHE jana iliwashuhudia wafanyakazi hao wakiendelea na wengine walielekea katika maeneo mengine ya kazi.

Mmoja wa wafanyakazi hao, Mohamed Kivishe, alisema waliamua kurejea kazini baada ya kikao cha juzi kati yao menejimenti, Chama cha wafanyakazi wa Ujenzi, Migodi na Madini (Tamico) na uongozi wa serikali Wilaya ya Kinondoni ambacho kilitoa maazimio ya kuwataka warejee kazini na kuwataka wasubiri maamuzi ya mahakama kuhusu madai yao.

Kabla ya kurejea kazini jana, juzi katika mkutano huo  waligomea maamuzi yaliyotolewa na menejimenti, Tamico na viongozi wa serikali Wilayani Kinondoni.

Wafanyakazi hao waligoma kwa takribani wiki moja waliyakataa maamuzi ya viongozi hao juzi ambao walikutana Mei 2 na Mei 5, mwaka huu kupata mwafaka.

Katibu wa Tamico Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Charles Mgashi, akisoma maamuzi ya mkutano huku polisi wenye silaha za moto na mabomu wakiwa wamezunguka wafanyakazi hao, alisema kikao kimeamua wafanyakazi wote warejee kazini kuanzia jana.

Alisema madai ya posho yataweza kutekelezwa baada ya Mahakama kutoa uamuzi katika kesi iliyofunguliwa na wafanyakazi hao  na suala la vitendea kazi litatekelezwa.

Hata hivyo, baada ya kusoma maamuzi hayo, wafanyakazi hao waliyapinga wakitaka walipwe haki zao zote za nyuma ndipo suala la kurejea kazini lifuate.

Wafanyakazi hao walianza mgomo Aprili 28, mwaka huu kwa kile walichodai kuwa wanafanya kazi kwa kubaguliwa katika malipo ya stahili na posho.

Mwenyekiti  wa Chama cha Wafanyakazi  Strabag, Abdullah Rukusa, alisema  sababu kubwa ya mgomo huo  ni ubaguzi  unaofanywa na uongozi wa juu katika suala la malipo ya stahili  zao Sh. 65,000.

Rukusa alisema wafanyakazi wa kampuni hiyo hasa wazawa wamekuwa wakibaguliwa katika malipo na kwamba raia wa kigeni  wamekuwa wakipewa  kipaumbele.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa