Tuesday, May 13, 2014

WATANZANIA CHANGAMKIENI FURSA ZA BIASHARA UN-TPSF

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imehamasisha Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa za biashara katika Umoja wa Mataifa (UN).
Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, wakati wa semina ya kuwahamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kufahamu na kuzitumia fursa za biashara zinazojitokeza katika UN.

Semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, iliandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na kitengo cha manunuzi cha ofisi ya UN.

Simbeye alisema kuwa semina hiyo ililenga kuwahamasisha wafanyabiashara  kuwekeza kimataifa na kutanua wigo wa biashara.

“Tumeleta wafanyabishara wa Tanzania katika semina hii ili kuangalia ni fursa zipi wanazoweza kuzipata katika zabuni za Umoja wa Mataifa,” alisema Simbeye.

Alisema kwamba Tanzania inashiriki kwa kiwango kidogo sana katika zabuni za UN, kitu ambacho kinawashangaza wadau mbalimbali hasa kutokana na mchango mkubwa wa Tanzania katika kuleta amani kwenye nchi nyingi duniani.

Hatujafanya semina ya namna hii kwa miaka tisa sasa, kama inavyofanywa na nchi jirani kama Kenya na Uganda…kuna fursa nyingi za biashara na Umoja wa Mataifa,” alisema Simbeye.

Aliongezea kuwa lengo ni kueleza wafanyabiashara fursa zilizopo, jinsi ya kuzitumia na pia kujua utaratibu unaofanywa na UN katika kupata wazabuni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Manunuzi, UN, Yavar Khan, alisema kuna kila sababu kwa Watanzania kushiriki kwa kiwango kikubwa katika kufanya biashara na umoja huo wa mataifa.

Naye, Ofisa Manunuzi Mwandamizi wa Ujumbe wa UN Sudani ya Kusini (UNMiss), Bruno Maboja, alisema kuwa mategemeo yao ni kuona kampuni za Tanzania zinashiriki katika biashara na umoja huo.

Alisema kuwa mwaka 2012 kampuni za kitanzania zilipata mkataba wa dola za Marekani milioni 7.2, kiwango alichosema ni kidogo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment