Tuesday, July 8, 2014

BOMANI:TUACHE KUJADILI SERIKALI 3

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

JAJI mstaafu, Mark Bomani, amelishauri Bunge Maalumu la Katiba, kuweka kando mjadala wa muundo wa Serikali katika Bunge lijalo linalotarajiwa kuanza Agosti 5 mwaka huu badala yake liendelee kujadili masuala mengine yaliyopo kwenye rasimu.

Alisema muundo wa Serikali, unaweza kujadiliwa katika wakati mwafaka hata baada ya Uchaguzi Mkuu 2015 kwani tayari kuna katiba inayoendelea kufanya kazi ingawa ina dosari.

Jaji Bomani aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maoni yake kuhusu mchakato huo, mvutano uliopo kwa wabunge kuhusu muundo wa Serikali tatu na mbili pamoja na mustakabali wa nchi.

Alisema badala ya wajumbe wa Bunge hilo kuendelea na mvutano uliojitokeza, Katiba iliyopo inaweza kuendelea kutumika akishauri suala la idadi ya Serikali ni vyema likaingizwa kwenye ilani za uchaguzi za vyama mbalimbali vya siasa.

"Kwa maoni yangu, vipengele vinavyoweza kuafikiwa vinaweza kuingizwa kwenye Katiba ya sasa bila kuhitaji kura ya maoni, hatua kama hii, ingeboresha kwa kiasi kikubwa Katiba tuliyonayo," alisema.

"Yapo mambo yanayoweza kujadiliwa na kupatikana mwafaka kama suala la Mawaziri kutokuwa wabunge, Muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi, uwakilishi sawa wa kijinsia kwenye vyombo vya uwakilishi, mgombea huru na tunu za Taifa," alisema.

Aliwasihi wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), warudi bungeni kuendelea na mjadala wa vipengele vingine vinavyopaswa kujadiliwa kwenye rasimu.

"Mimi naamini kuwa, tukilazimisha uamuzi wa idadi ya Serikali, ipo hatari ya kuiingiza nchi kwenye tafrani kubwa ambayo matokeo yake yanaweza kuvuruga amani ya nchi hata kuvunja Muungano uliopo.

"Hatuwezi kuendelea na mjadala usio na matumaini ya mafanikio, zaidi ya sh. bilioni 60 zimetumika kuwalipa wajumbe wa Bunge Maalumu ukiondoa mamilioni ya fedha zilizotumika kuwalipa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba," alisema Jaji Bomani.

Alisema msingi wa kupata Katiba nzuri ni maridhiano na haiwezi kupatikana kwa wingi wa kura au hoja ya nguvu bali inapaswa kukubalika na walio wengi si vinginevyo.

Wakati Rasimu ya Pili ya Katiba ikisema muundo wa Serikali tatu ndio unaotakiwa na wananchi wengi, mjadala wa rasimu hiyo uliibua malumbano makali na kusababisha baadhi ya wajumbe kutoka nje.

Rasimu hiyo iliwasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa tume, Jaji mstaafu Joseph Warioba Aprili mwaka huu.

Mustakabali wa nchi

Jaji Bomani alisema kuwa, baada ya Tanganyika kupata Uhuru wake, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alitangaza kwamba kazi kubwa ya Taifa ni kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

Alisema maadui hao hadi sasa ndio maadui wakubwa wa nchi ambapo mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya maadui hao hayaridhishi kwani bado hatujafuta ujinga, maradhi na umaskini ambao umekithiri na unawatesa Watanzania wengi.

"Inasikitisha kuona msongamano mkubwa wa wananchi wakingoja matibabu katika Vituo vya Afya... mara nyingi wananchi wasiojiweza kifedha wanakosa matibabu muhimu na kurudi nyumbani kwa kukosa fedha, wangapi wanakosa sh. 500,000 ili wafanyiwe upasuaji hata katika hospitali za Serikali kama Muhimbili.

"Wangapi wanamudu kununua dawa katika maduka ya watu binafsi baada ya kuzikosa katika hospitali za Serikali...nchi yetu ina rasilimali za kutosha zinazoweza kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi kama zitatumika au kusimamiwa vizuri kwa uadilifu bila kuporwa au kufanyiwa ufisadi na wajanja wachache," alisema.

Alisema janga lingine ambalo baadhi ya viongozi wanaliita 'bomu', linalosubiri kulipuka ni uhaba wa ajira kwa vijana ambao wengi wao hawana ajira hivyo hujikuta wakizurura pamoja na suala la rushwa ambalo linatishia maendeleo ya nchi na adui mkubwa wa haki.

Chanzo:Majira

 

No comments:

Post a Comment