JAJI
mstaafu, Mark Bomani, amelishauri Bunge Maalumu la Katiba, kuweka kando
mjadala wa muundo wa Serikali katika Bunge lijalo linalotarajiwa kuanza
Agosti 5 mwaka huu badala yake liendelee kujadili masuala mengine
yaliyopo kwenye rasimu.
Alisema muundo wa
Serikali, unaweza kujadiliwa katika wakati mwafaka hata baada ya
Uchaguzi Mkuu 2015 kwani tayari kuna katiba inayoendelea kufanya kazi
ingawa ina dosari.
Jaji Bomani aliyasema
hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya
maoni yake kuhusu mchakato huo, mvutano uliopo kwa wabunge kuhusu
muundo wa Serikali tatu na mbili pamoja na mustakabali wa nchi.
Alisema badala ya
wajumbe wa Bunge hilo kuendelea na mvutano uliojitokeza, Katiba iliyopo
inaweza kuendelea kutumika akishauri suala la idadi ya Serikali ni vyema
likaingizwa kwenye ilani za uchaguzi za vyama mbalimbali vya siasa.
"Kwa maoni yangu,
vipengele vinavyoweza kuafikiwa vinaweza kuingizwa kwenye Katiba ya sasa
bila kuhitaji kura ya maoni, hatua kama hii, ingeboresha kwa kiasi
kikubwa Katiba tuliyonayo," alisema.
"Yapo mambo yanayoweza
kujadiliwa na kupatikana mwafaka kama suala la Mawaziri kutokuwa
wabunge, Muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi, uwakilishi sawa wa kijinsia
kwenye vyombo vya uwakilishi, mgombea huru na tunu za Taifa," alisema.
Aliwasihi wajumbe wa
Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), warudi bungeni
kuendelea na mjadala wa vipengele vingine vinavyopaswa kujadiliwa
kwenye rasimu.
"Mimi naamini kuwa,
tukilazimisha uamuzi wa idadi ya Serikali, ipo hatari ya kuiingiza nchi
kwenye tafrani kubwa ambayo matokeo yake yanaweza kuvuruga amani ya nchi
hata kuvunja Muungano uliopo.
"Hatuwezi kuendelea na
mjadala usio na matumaini ya mafanikio, zaidi ya sh. bilioni 60
zimetumika kuwalipa wajumbe wa Bunge Maalumu ukiondoa mamilioni ya fedha
zilizotumika kuwalipa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba," alisema Jaji Bomani.
Alisema msingi wa
kupata Katiba nzuri ni maridhiano na haiwezi kupatikana kwa wingi wa
kura au hoja ya nguvu bali inapaswa kukubalika na walio wengi si
vinginevyo.
Wakati Rasimu ya Pili
ya Katiba ikisema muundo wa Serikali tatu ndio unaotakiwa na wananchi
wengi, mjadala wa rasimu hiyo uliibua malumbano makali na kusababisha
baadhi ya wajumbe kutoka nje.
Rasimu hiyo iliwasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa tume, Jaji mstaafu Joseph Warioba Aprili mwaka huu.
Mustakabali wa nchi
Jaji Bomani alisema
kuwa, baada ya Tanganyika kupata Uhuru wake, Hayati Mwalimu Julius
Nyerere alitangaza kwamba kazi kubwa ya Taifa ni kupambana na maadui
watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.
Alisema maadui hao hadi
sasa ndio maadui wakubwa wa nchi ambapo mafanikio yaliyopatikana katika
mapambano dhidi ya maadui hao hayaridhishi kwani bado hatujafuta
ujinga, maradhi na umaskini ambao umekithiri na unawatesa Watanzania
wengi.
"Inasikitisha kuona
msongamano mkubwa wa wananchi wakingoja matibabu katika Vituo vya
Afya... mara nyingi wananchi wasiojiweza kifedha wanakosa matibabu
muhimu na kurudi nyumbani kwa kukosa fedha, wangapi wanakosa sh. 500,000
ili wafanyiwe upasuaji hata katika hospitali za Serikali kama
Muhimbili.
"Wangapi wanamudu
kununua dawa katika maduka ya watu binafsi baada ya kuzikosa katika
hospitali za Serikali...nchi yetu ina rasilimali za kutosha zinazoweza
kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi kama zitatumika au kusimamiwa
vizuri kwa uadilifu bila kuporwa au kufanyiwa ufisadi na wajanja
wachache," alisema.
Alisema janga lingine
ambalo baadhi ya viongozi wanaliita 'bomu', linalosubiri kulipuka ni
uhaba wa ajira kwa vijana ambao wengi wao hawana ajira hivyo hujikuta
wakizurura pamoja na suala la rushwa ambalo linatishia maendeleo ya nchi
na adui mkubwa wa haki.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment