Home » » KARAKATA WAPINGA UJENZI OFISI SERIKALI MTAA KUSIMAMISHWA

KARAKATA WAPINGA UJENZI OFISI SERIKALI MTAA KUSIMAMISHWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Wakazi wa Mtaa wa Karakata, Manispaa ya Ilala, wamepinga hatua iliyochukuliwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kipawa, Said Fundi, ya kupiga marufuku ujenzi wa ofisi ya serikali ya mtaa na kumpa siku saba kutengua amri hiyo.
NIPASHE ilipata nafasi ya kuiona amri hiyo iliyotolewa kwa mujibu wa kifungu namba 68 cha sheria namba 8/82, iliyomtaka mwenyekiti wa mtaa kusimamisha ujenzi katika eneo la Shule ya Sekondari ya Ilala, Kata ya Kipawa mara moja, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa.

Msimamo huo umechukuliwa na wakazi hao baada ya Mwenyekiti wa Mtaa huo, Gerson Malik, kuitisha mkutano wa dharura kujadili kero mbalimbali, ikiwamo kusimamishwa kwa ujenzi wa ofisi yake.

Mmoja wa wakazi hao, Ally Ndumile, alisema katika mkutano huo kuwa haitawezekana ofisi inayojengwa kwa nguvu zao kusimamishwa kinyemela.

“Inawezekana serikali inafurahishwa na kitendo cha serikali ya mtaa wetu kuendelea kupanga na kuipeperusha bendera yake nyumbani kwa mtu. Kama siyo, kwanini amri hiyo imetolewa?” alihoji.

Akiwasilisha hoja ya kusimamisha ujenzi wa ofisi mtaa huo kwa wananchi mwishoni mwa wiki, Malik alisema alipokea amri hiyo Mei 30, mwaka huu na kutakiwa kufika ofisi ya mtendaji kata saa 3:00 asubuhi.

Diwani wa Kata ya Kipawa, Bonah Kalua, aliwatuliza wakazi hao, ambao wengi wao walionyesha kukerwa na hatua iliyochukuliwa na mtendaji.

Alisema mtendaji hawezi kuwapangia wananchi, bali wajibu wake kama mtaalamu ni kushauri na kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na wananchi kwa ajili ya maendeleo yao.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa