Home » » KINYEREZI I KUANZA KUZALISHA GESI MWAKANI

KINYEREZI I KUANZA KUZALISHA GESI MWAKANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Umeme Tanzania,Felchesmi Mramba.
Watanzania wanatarajia kuanza kunufaika zaidi na gesi asilia baada ya mtambo wa kuzalisha nishati hiyo wa Kinyerezi I jijini Dar es Salaam, kuanza uzalishaji Januari, mwakani.
Hayo yalibainishwa na mhandisi Gladstone Kombe, kutoka Shirika la Umeme nchini (Tanesco), wakati akizungumza  kwenye banda la Wizara ya Nishati na Madini katika viwanja vya Maonyesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) .

 Mhandisi Kombe, alisema mtambo wa Kinyerezi I, unatarajia kuanza kazi Januari mwakani kwa kuzalisha umeme unaotokana na gesi asilia kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi megawati 150.

 Kwa mujibu wa Kombe, umeme kutoka kwenye mtambo  huo utaingizwa katika Gridi ya Taifa kwa ajili ya matumizi ya nchi nzima.
Alitaja baadhi ya mitambo mingine ambayo inazalisha umeme unaotokana na gesi asilia kuwa ni pamoja na Songas uliopo Ubungo na IPTL uliopo Tegeta jijini humo.

 Kuhusu kushuka kwa gharama za umeme baada ya kiasi cha nishati hiyo kuendelea kuongezeka, alisema, kwa sasa hana uhakika iwapo kuna uwezekano wowote na kwamba, lengo la  serikali kuongeza mitambo mipya ni kwa ajili ya kuimarisha Gridi ya Taifa.

 Mitambo na miradi mingine ya umeme ambayo inatarajia kuanza uzalishaji wake ni pamoja na (kwenye mabano mwaka wa kuanza uzalishaji), Kinyerezi II megawati 240 (2014), Kinyerezi III megawati 600 (2016) na Kinyerezi IV megawati 450 (2017).

 Mingine ni Singida Geo Wind awamu ya kwanza megawati 150 (2017) na Kilwa Energy megawati 210 na  baada ya kukamilika kwa miradi hiyo, Tanzania inatarajia kupata kiasi cha umeme wa megawati 1, 310.

Wakati huo huo,  ujenzi wa bomba la kusafisha na kusafirishia gesi asilia kutoka Mnazibay (Mtwara) na Songosongo (Lindi), hadi Mei mwaka huu ulifikia asilimia 82.

Akizungumza na gazeti hili kwenye banda hilo, mmoja wa wafanyakazi kutoka Wizara ya Nishati na Madini ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa siyo msemaji, alisema ujenzi huo umefikia kwenye kiwango hicho na kwamba mtambo wa kusafisha gesi wa Mnazibay wenye njia tatu, una uwezo wa kusafisha nishati hiyo futi za ujazo milioni 210 kwa siku.

 Kwa mujibu wa mfanyakazi huyo, mtambo wa kusafisha gesi wa Songosongo, una njia kuu mbili huku ukiwa na uwezo wa kusafisha nishati hiyo futi za ujazo milioni 140 kwa siku.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa