Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa chuo cha usafiri wa Anga, kilichopo chini ya Mamlaka ya Usafiri
wa Anga Tanzania (TCAA) margareth Kyarwenda akaimueleza mwandishi wa
mwananchi (hayupo pichani) namna wanavyotumia mitambo ya kisasa
kufundishia wanafunzi somo la uongozajiwa wa ndege. Picha na Nuzulack
Dausen
Dar es Salaam. Ukiwa ndani ya ndege tayari kwa kupaa au kutua
uwanjani unaweza usifahamu kinachoendelea baina ya rubani na mwongozaji
wa ndege kwa upande mwingine.
Wakati huo abiria, hasa waliopanda ndege kwa mara
ya kwanza, hujikuta wakimwomba Mungu wapae au watue salama kutokana na
zoezi hilo kuhusisha kashkash kidogo na umakini wa hali ya juu kuzuia
ajali.
Wakati abiria hao wakifikiria juu ya usalama wao,
waongozaji ndege katika kiwanja husika huwa na kazi ya ziada ya
kuwasiliana kwa makini na rubani kuhakikisha ndege inapaa na kutua
salama kwa kuondoa kikwazo chochote hatarishi.
Katika kazi hiyo, vyombo vya teknolojia vya hali
juu vya mawasiliano na wataalamu waliosomea sayansi ya usafiri wa anga
hufanya kazi kwa umakini.
Yote hayo hufanyika kuzuia visa kama kilichotokea
hivi karibuni jijini Barcelona, Hispania baada ya rubani wa ndege kutoka
Urusi aina ya Boeing 767 ya kampuni ya UTair kuepusha ajali ya
kugongana na ndege nyingine ya Argentina iliyokuwa ikitembea katika
kiwanja hicho bila mwelekeo.
Mkufunzi mwandamizi wa usimamizi wa ndege kutoka
chuo cha mafunzo ya usafiri wa anga (CATC), Shadrack Kalinga anaeleza
kazi inavyofanyika ili kuiongoza ndege inapopaa na kutua:
“Pale huwa hakuna tena mchezo, lazima mwongozaji
awe makini kuwasiliana kikamilifu na ndege inayokuja au inayotaka kupaa.
Lugha wanayotumia hapa ni ya kitaalamu na sio kiingereza mlichozoea,”
anasema.
“Aina hii kwa Kiingereza tunaiita phraseology ina
maneno maalumu tofauti na haya ya kawaida. Ninaposema hapana nasema
‘negative’ na siyo ‘no’ kama ilivyozoeleka au napotaka kusema ndiyo
nasema ‘affirm’ na siyo ‘yes’ tena.”
Anasema kuwa waongozaji hukaa katika mnara maalumu
(Air Traffic Control Tower) ambao unaonyesha pande zote za uwanja kwa
umakini na angani kwa umbali wa fulani ambao mara nyingi ni takribani
maili 15 hivi.
Kalinga anaongeza kuwa muongozaji ana uwezo wa
kumwongoza rubani mpaka umbali huo iwapo anga lipo sawia bila tatizo
lolote la hali ya hewa.
“Kama hali ya hewa ni mbaya muongozaji hawezi
kuongoza ndege mpaka ‘nautical mile 15’ (wastani wa maili 15)…
ataiongoza pale itakapo potea…na haraka atamwachia Approach controller
(mwongozaji mwenye uwezo wa kuona mbali zaidi),” anasema Kalinga.
Anaongeza kuwa hata hivyo uongozaji wa namna hiyo
hutegemea sana na mtindo anautumia rubani kuendesha ndege yake. Wapo
wanaotumia kuendesha kwa kuangalia nje katika hatua hiyo na wapo
wanaongozwa kwa vyombo pekee
“Yule anayeongozwa na vyombo mara nyingi huongozwa kwa takriban
dakika mbili hivi na baada ya hapo kazi hiyo huachiwa ‘approach
controller’ ambaye huiongoza ndege hiyo mpaka maili 100, 120 au zaidi,”
anasema mtaalamu huyo na kuongeza;
“Kama hali ya hewa ni mbaya sana basi ndege ikishaoondoka tu anapewa ‘approach controller’.”
Katika chumba hicho cha uongozaji ndege huwa kuna
mitambo maalumu na ya kisasa inayohakikisha mawasiliano yasiyo na
vikwazo na kwamba utulivu wa hali ya juu wa mwongozaji na rubani
huhitajika.
“Ndiyo maana tunasisitiza sana marubani na
waongoza ndege wasiwe na stress (msongo wa mawazo) kutokana na asili ya
kazi yao,” anasema Kalinga na kuongeza;
“Na pale uwanjani mwongozaji anatakiwa awe na
taarifa ya kila kitu kinachoendelea ikiwemo kujua shughuli zote nyingine
tofauti na ndege zinazoendelea kama vile muda ambao trekta la kukata
nyasi litakapoanza kazi yake.”
No comments:
Post a Comment