Home » » KUENDESHA NDEGE NI ZAIDI YA KUWA NA RUBANI

KUENDESHA NDEGE NI ZAIDI YA KUWA NA RUBANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkuu wa chuo cha usafiri wa Anga, kilichopo chini ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) margareth Kyarwenda akaimueleza mwandishi wa mwananchi (hayupo pichani) namna wanavyotumia mitambo ya kisasa kufundishia wanafunzi somo la uongozajiwa wa ndege. Picha na Nuzulack Dausen  

Dar es Salaam. Ukiwa ndani ya ndege tayari kwa kupaa au kutua uwanjani unaweza usifahamu kinachoendelea baina ya rubani na mwongozaji wa ndege kwa upande mwingine.
Wakati huo abiria, hasa waliopanda ndege kwa mara ya kwanza, hujikuta wakimwomba Mungu wapae au watue salama kutokana na zoezi hilo kuhusisha kashkash kidogo na umakini wa hali ya juu kuzuia ajali.
Wakati abiria hao wakifikiria juu ya usalama wao, waongozaji ndege katika kiwanja husika huwa na kazi ya ziada ya kuwasiliana kwa makini na rubani kuhakikisha ndege inapaa na kutua salama kwa kuondoa kikwazo chochote hatarishi.
Katika kazi hiyo, vyombo vya teknolojia vya hali juu vya mawasiliano na wataalamu waliosomea sayansi ya usafiri wa anga hufanya kazi kwa umakini.
Yote hayo hufanyika kuzuia visa kama kilichotokea hivi karibuni jijini Barcelona, Hispania baada ya rubani wa ndege kutoka Urusi aina ya Boeing 767 ya kampuni ya UTair kuepusha ajali ya kugongana na ndege nyingine ya Argentina iliyokuwa ikitembea katika kiwanja hicho bila mwelekeo.
Mkufunzi mwandamizi wa usimamizi wa ndege kutoka chuo cha mafunzo ya usafiri wa anga (CATC), Shadrack Kalinga anaeleza kazi inavyofanyika ili kuiongoza ndege inapopaa na kutua:
“Pale huwa hakuna tena mchezo, lazima mwongozaji awe makini kuwasiliana kikamilifu na ndege inayokuja au inayotaka kupaa. Lugha wanayotumia hapa ni ya kitaalamu na sio kiingereza mlichozoea,” anasema.
“Aina hii kwa Kiingereza tunaiita phraseology ina maneno maalumu tofauti na haya ya kawaida. Ninaposema hapana nasema ‘negative’ na siyo ‘no’ kama ilivyozoeleka au napotaka kusema ndiyo nasema ‘affirm’ na siyo ‘yes’ tena.”
Anasema kuwa waongozaji hukaa katika mnara maalumu (Air Traffic Control Tower) ambao unaonyesha pande zote za uwanja kwa umakini na angani kwa umbali wa fulani ambao mara nyingi ni takribani maili 15 hivi.
Kalinga anaongeza kuwa muongozaji ana uwezo wa kumwongoza rubani mpaka umbali huo iwapo anga lipo sawia bila tatizo lolote la hali ya hewa.
“Kama hali ya hewa ni mbaya muongozaji hawezi kuongoza ndege mpaka ‘nautical mile 15’ (wastani wa maili 15)… ataiongoza pale itakapo potea…na haraka atamwachia Approach controller (mwongozaji mwenye uwezo wa kuona mbali zaidi),” anasema Kalinga.
Anaongeza kuwa hata hivyo uongozaji wa namna hiyo hutegemea sana na mtindo anautumia rubani kuendesha ndege yake. Wapo wanaotumia kuendesha kwa kuangalia nje katika hatua hiyo na wapo wanaongozwa kwa vyombo pekee

“Yule anayeongozwa na vyombo mara nyingi huongozwa kwa takriban dakika mbili hivi na baada ya hapo kazi hiyo huachiwa ‘approach controller’ ambaye huiongoza ndege hiyo mpaka maili 100, 120 au zaidi,” anasema mtaalamu huyo na kuongeza;
“Kama hali ya hewa ni mbaya sana basi ndege ikishaoondoka tu anapewa ‘approach controller’.”
Katika chumba hicho cha uongozaji ndege huwa kuna mitambo maalumu na ya kisasa inayohakikisha mawasiliano yasiyo na vikwazo na kwamba utulivu wa hali ya juu wa mwongozaji na rubani huhitajika.
“Ndiyo maana tunasisitiza sana marubani na waongoza ndege wasiwe na stress (msongo wa mawazo) kutokana na asili ya kazi yao,” anasema Kalinga na kuongeza;
“Na pale uwanjani mwongozaji anatakiwa awe na taarifa ya kila kitu kinachoendelea ikiwemo kujua shughuli zote nyingine tofauti na ndege zinazoendelea kama vile muda ambao trekta la kukata nyasi litakapoanza kazi yake.”

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa