Tuesday, July 8, 2014

MAWAZIRI WATANO,UINGEREZA KUJADILI GESI,MAFUA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Dk. Mary Nagu
 
Mawaziri watano wa Tanzania wanatarajiwa kukutana leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Mark Simmonds, kujadili mambo ya uhusiano wa kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo jana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza inayoshughulikia masuala ya Afrika ilisema baadhi ya mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na uwekezaji wa gesi na mafuta.

Mawaziri wanaotarajiwa kukutana na ujumbe huo kutoka Uingereza, ni Chrisopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Profesa Sospeter Muhongo ((Nishati na Madini), Dk. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk. Abdalla Kigoda (Viwanda na Biashara) na Dk. Mary Nagu (pichani) (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Uwekezaji na Uwezeshaji).

Wajumbe wengine wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue; Mtendaji Mkuu wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Omari Issa; Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Florens Turuka.

Wengine ni Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji, Juliet Kairuki; Mkurugenzi Mtendaji Saggot, Geoffrey Kirenga; Katibu Kituo cha Biashara, Raymond Mbilinyi; Balozi wa  Uingereza nchini, Dianna Melrose; na watu wengine kutoka Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) ya Uingereza pamoja na sekta binafsi.

Adha, waziri huyo wa Uingereza leo anatarajiwa kuzindua umoja wa wafanyabiashara wa Uingereza nchini, ambao utahudhuriwa na Balozi Merlrose, ambaye ataongoza mpango wa uwezeshaji vijana.

Hii ni mara ya tatu waziri huyo wa Uingereza kuwasili nchini kwa mwaka huu, ambaye pamoja na mambo mengine, atapata fursa ya kuangalia utekelezaji wa sheria ya uwindaji wanyamapori iliyojadiliwa na wajumbe kutoka nchi mbalimbali katika mkutano uliofanyika Uingereza, Februari, mwaka huu.

Mkutano huo uliozikutanisha nchi mbalimbali duniani zilizojadili namna ya kudhibiti ujangili unaoendelea nchini, uliwakilishwa na Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Uingereza.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kesho waziri huyo wa Uingereza atakutana na Waziri Nyalandu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Ilifafanua kuwa ziara za waziri huyo nchini zinatokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi mbili hizo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment