Tuesday, July 8, 2014

WIZI KITUO CHA DALADALA MAKUMBUSHO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki
Kituo cha daladala cha Makumbusho kimegeuzwa kuwa mradi wa kujipatia fedha kwa njia za ujanja, baada ya baadhi ya watu kujitungia utaratibu wa kuitoza kila daladala na pikipiki, maarufu kama “bodaboda” Sh. 1,000 zinapopakia abiria ndani au nje ya kituo hicho kwa siku.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa fedha hizo ni mbali na zile zinazotozwa mlangoni wakati daladala husika linapokuwa linatoka katika kituo hicho baada ya kupakia abiria.

Baadhi ya watumiaji wa kituo hicho waliozungumza na NIPASHE kwa wakati tofauti walisema kuhamishiwa kituo Makumbusho kumesaidia kupunguza wizi uliokuwa umekithiri kwenye kituo cha Mwenge, lakini baadhi ya watu wamegeuza ni mahali pa kupatia fedha.

Bismaki Katwila, ambaye ni mwendesha pikipiki, maarufu kama “bodaboda”, alisema: “Tunalipa Sh. 1,000 kila tunapopakia abiria. Na hapa Makumbusho kuna pikipiki zaidi ya 120.

Hebu jiulize. Kwa siku wanapata kiasi gani? Na hawatoi risiti ya malipo kuonyesha kama umelipa,” alisema Katwila
Alisema hapingi kulipa ushuru, ila anachotaka fedha zifike halmashauri na siyo kuchukuliwa na wajanja waliokuwa wanaiba wakati kituo kilipokuwa Mwenge.

Dani Mmanga, ambaye ni kondakta wa daladala alisema wamekuwa wakihoji kuhusiana na fedha wanazotoa kila wanapopakia na kujibiwa zinakwenda kwenye mfuko wa madereva.

“Tumeambiwa tunachangia mfuko wa madereva. Sasa fikria. Kwa siku mimi mwenyewe natoa zaidi ya Sh. 15,000. Magari yapo zaidi ya 300. Wanakusanya shilingi ngapi? Na kwa mwezi ni kiasi gani kinapotelea mikononi mwa watu wa kawaida? Kama hizi fedha zingefika halmashauri zingesaidia kukarabati miundombinu,” alisema Mmanga.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Guninita Kamba, aliahidi kulishughulikia suala hilo, ikiwa ni pamoja na kujua utaratibu unaotumiwa kuwatoza fedha watumiaji wa kituo hicho.

“Nashukuru umeniambia. Nilikuwa sijui kama kuna jambo kama hilo. Nitahakikisha nalifanyia kazi na kujua ni namna gani tunaweza kuwadhibiti watu kama hao,”alisema Kamba.

Akizungumzia suala la miundombinu inayoingia ndani ya kituo hicho, Kamba alisema kitengo cha ujenzi wa barabara za halmashauri kitahakikisha kinakarabati kila eneo linaloingia ndani ya kituo cha Makumbusho.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment