Friday, July 11, 2014

SUMAYE BADO AOTA URAIS

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

  Aibukia alikopita Membe
  Makamba azidi kushukiwa
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Harakati za kuusaka urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinazidi kuchukua sura mpya baada ya  Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kuonyesha nia yake ya kutaka kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.
Sumaye ambaye ni Waziri Mkuu pekee aliyedumu katika wadhifa huo kwa miaka 10 tangu alipoteuliwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kwa vipindi viwili vya kati ya 1995 hadi 2005, amedhihirisha nia yake hiyo jana wakati akizungumza na vijana jijini Mwanza.

Alidhihirisha ndoto yake ya kutaka kurejea madarakani wakati alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ofisi za taasisi ya Kituo cha Maendeleo ya Vijana (TYDC) jijini Mwanza baada ya kusema kuwa ataendelea  kupigania maisha bora na kupambana na dhulma dhidi ya umma, "iwe awe katika nafasi kubwa ya madaraka ya nchi ama vinginevyo".

Bila kutaja moja kwa moja kuwa atawania urais, Sumaye alisema kuwa amekuwa akisikia vitimbwi mbalimbali na kwamba mengi yamekuwa yakisemwa juu yake; lakini hababaishwi na daima ataendelea kusema ukweli.

"Vitimbwi  vimeanza kweli kweli,  kwa sababu  tangu  niingie  hapa (Mwanza) kama  siku  tatu  ama  nne  sasa,  nimesikia  mengi  yakizungumzwa juu  yangu... lakini mimi nasema nitaendelea  kusimamia ukweli," alisema Sumaye ambaye ni mlezi wa TYDC.

Sumaye aliingia jijini Mwanza siku nne zilizopita lakini hakuwahi kuonekana kwenye hafla zilizojumuisha umma mpana hadi alipotokea kwenye uzinduzi huo jana.

Akizungumzia mbio za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, Sumaye alisema dhamira yake ya kupambana na uovu imekuwapo kwa muda mrefu licha ya kuwapo njama na hujuma zinazoelekezwa kwake.

"Mimi,  kwa wale mnaonifahamu... nipo  mstari wa mbele  kupambana  na maovu. Siyo  katika  urais; bali  hata nisiwe na madaraka  makubwa serikalini,  nitaendelea  kupambana,"  alisema Sumaye.

 Hafla hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo walimu  na wanafunzi  kutoka vyuo  vya elimu  ya juu  vilivyopo kanda  ya Ziwa  Victoria.

Aidha, Sumaye aliwataka vijana nchini kote kutokubali  kujihusisha na vitendo viovu, vikiwamo vya kupokea  rushwa kutoka kwa wanasiasa wanaoutafuta urais.

Alisema, kwa vile TYDC inawajumuisha vijana wenye itikadi tofauti za kisiasa, hakuna sababu kwa wanasiasa kuwatumia kwa maslahi yao.

Kwa mujibu wa Sumaye, kuitumia TYDC kisiasa kutasababisha madhara zaidi kwa vijana badala ya kuwa sehemu ya kuwakomboa kifikra, kijamii na kiuchumi.
“Mimi nimekubali kuwa mlezi wa TYDC baada ya kujua ni taasisi inayojishughulisha na maendeleo ya vijana, matatizo ya vijana, matatizo ya jamii, kupambana na maovu katika jamii na kuhimiza uzalendo na mshikamano katika taifa,” alisema na kuongeza kuwa:

“Mimi ni mpambanaji dhidi ya matatizo na maovu ambayo yametajwa kwenye malengo ya TYDC, hivyo nimepata wapiganaji wenzangu katika vita hii yaani ni vijana ambao ni wengi, wenye nguvu na uchungu na nchi yao."

Alizitaja  baadhi  ya changamoto  zinazolikabili  Taifa kuwa ni  kukithiri  kwa rushwa, biashara  ya dawa za kulevya, umaskini  na upungufu  wa ajira  miongoni  mwa  vijana.

Kwa mujibu wa Sumaye, sehemu  kubwa ya changamoto  hizo  zinasababishwa na  ubinafsi  pamoja  na ulafi  miongoni  mwa viongozi  na watendaji serikalini.

Awali  Mwenyekiti  wa TYDC, Lengai  Ole  Sabaya, alisema taasisi hiyo inalenga kutetea  uwapo wa mazingira mazuri na fursa za maendeleo  miongoni  mwa vijana  nchini.

Kuwapo kwa Sumaye Mwanza kwa siku ya nne jana kuliibua hisia kuwa huenda amedhamiria kujisafishia njia ya kukubalika jijini humo ambako hivi karibuni kulitembelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe; ambaye ni mmoja wa watu wanaotajwa kutaka kuwania urais kupitia tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu wa 2015. 

MAKAMBA AZIDI KUSHUKIWA
Katika hatua nyingine; Kauli ya  Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kwamba Tanzania inahitaji kiongozi kijana katika nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao, imezidi kupingwa na baadhi ya viongozi wa chama chake (CCM) na serikali.

Akizungumza na NIPASHE, Mkuu wa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Anthony Mtaka  alisema anapingana na kauli ya Makamba kwa vile suala la ujana peke yake halipaswi kuwa kigezocha kumuwezesha mtu kuwa rais.

Mtaka alisema hoja hiyo iliyowahi pia kutolewa na Waziri Mkuu wa zamani, Jaji mstaafu Joseph Warioba, haina mashiko kwa kuwa anaweza kuchaguliwa rais kijana, lakini asiweze kutatua matatizo ya wananchi anaowaongoza kama inavyodhihirishwa na baadhi ya mawaziri vijana ambao hadi sasa wameshindwa kutatua changamoto lukuki ndani ya wizara zao.

Alisema ni vema kufuata maoni ya Baba wa Taifa,  Mwalimu Julius Nyerere kuhusiana na rais anayefaa kuiongoza Tanzania.

“Hoja ya ujana wanayotumia January na Mzee Warioba haina mashiko kwa sababu anaweza kuchaguliwa rais kijana, lakini asiweze kutatua matatizo ya vijana. Na pia anaweza kuchaguliwa rais mzee, lakini asiweze kumaliza matatizo ya wazee,” alisema Mtaka.

Aliongeza: “Hivyo, ni bora wananchi wakafahamu ujana au uzee siyo kigezo cha kuwa rais kama hana sifa nzuri ya utendaji kazi ni kazi bure.”

Alisema jambo la msingi ni kiongozi kuwa na hekima na busara, uadilifu, uwajibikaji na utendaji wa kazi wenye rekodi iliyotukuka.
“Nasisitiza ndugu yangu January Makamba kuleta hoja ya kutaka kuwania urais kwa kuwa ni kijana, pia haina mashiko, kwani kuwa kijana siyo hoja ya kuwa rais. Hata kama amepata nafasi ya kutembea nchi mbalimbali na kuandika hotuba za rais, siyo kigezo,” alisema.

Juni 23 mwaka huu, Membe alikuwa jijini Mwanza  mgeni rasmi katika uzinduzi wa filamu iitwayo 'I love Mwanza' iliyoandaliwa na kikundi cha Lake Zone Youth Empowerment Foundation kwa kushirikiana na Tropical Media Tanzania Limited. 

 Sumaye, Membe,  Janaury Makamba na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ni miongoni mwa makada wa CCM waliowahi kuonywa na chama chao kuhusiana na madai ya kuanza mapema mbio za kuwania urais katika uchagunzi mkuu ujao.

Wengini ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mawasiliano na Uratibu),  Stephen Wassira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment