Friday, July 11, 2014

WINGI WA MASHINE ZA BVR WAONGEZA GHARAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kupanda kwa gharama za kampuni iliyoshinda tenda ya kuleta nchini mashine za kisasa za kuandikisha wapigakura za Biometric Voters Registration (BVR) inatokana na idadi ya mashine hizo kuongezeka kutoka 12,000 hadi 15,500.
Mashine za BVR zitaanza kutumika Septemba mwaka huu katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura likakalofanyika kwa muda wa wiki mbili.
Awali, gharama za ununuzi wa mashine hizo ilikuwa Sh78 bilioni lakini baada ya kampuni iliyoshindwa tenda hiyo kukata rufaa katika Mamlaka ya Rufani za Manunuzi ya Umma (PPAA), NEC iliibuka na kueleza kuwa gharama hizo zimepanda hadi Sh 117 bilioni.
Akizungumza jana katika mkutano kati ya Tume hiyo na vyama vya siasa, Mkurugenzi wa Ununuzi na vifaa wa NEC, Gregory Kaijage alisema katika awamu ya kwanza, NEC ilipanga kununua mashine 12,000 lakini kutokana na tume hiyo kuamua kuongeza vituo vya kujiandikishia wapigakura, walilazimika pia kuongeza idadi za mashine hizo.
“Uandikishaji utafanyika katika vituo vilivyopo katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa. Kwa utaratibu huu vituo vimeongezeka kutoka 24,919 hadi 40,015 ili kuwarahisishia wananchi waweze kujiandikisha kwa wingi” alisema Kaijage.
Kaijage alisisitiza kuwa sababu nyingine za kuongezeka kwa gharama zimetokana na kuanzishwa kwa ofisi za kanda, na ufungwaji wa vifaa katika vituo mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hadi itakapofika siku ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 wananchi watakaokuwa wamejiandikisha kwa ajili ya kupiga kura watakuwa 23,971,467, ukiondoa wale ambao wanakadiriwa kuwa watakuwa wamefariki.
“Idadi hii itahusisha wote waliokuwa na miaka 15, 16 na 17 mwaka 2012 ambao watakuwa wamefikisha umri wa miaka 18 mwaka 2015,” alisema Jaji Lubuva.
Hata hivyo, viongozi wote wa vyama vya siasa waliohudhuria mkutano huo waliilalamikia NEC kwa kutenga muda mfupi wa wiki mbili kwa ajili ya kuandikisha wapigakura.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema muda huo ni mfupi, huku akitolea mfano mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo kumezuiwa kufanyika kwa mikutano ya hadhara, hivyo wananchi wa maeneo hayo hawataweza kupewa elimu na vyama vyao kuhusu kazi hiyo kama ilivyoshauri NEC.
Profesa Lipumba pia alihoji kiasi cha Sh 263 bilioni kilichopangwa kutumiwa na NEC katika kazi hiyo, wakati tume hiyo katika Bajeti ya mwaka 2014/15, imetengewa Sh 7 bilioni tu.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Leticia Ghati alisema licha ya muda kuwa mfupi pia wananchi hawakupewa elimu yoyote na kwamba kwa muda uliobaki hautoshi kwa elimu hiyo kutolewa
Katibu Mkuu Chadema, Dk Wilbroad Slaa naye aligusia sakata la Mtwara na Lindi, kusisitiza kuwa muda ni mfupi kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo.
Mwenyekiti wa Tadea, Lifa Chipaka, Naibu Katibu Mkuu wa DP pamoja na Katibu Mwenezi wa TLP nao waliitaka NEC kuongeza muda huo.
Akijibu hoja hiyo, Jaji Lubava alisema muda huo unatosha kutokana na kuongezeka kwa vituo vya uandikishaji.
Chhanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment