Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wakati serikali ikijikung’uta vumbi la kuwasafisha wahusika wa tuhuma za fedha za Escrow, Kamati ya Katiba, Sheria na na Utawala imeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuharakisha kuchunguza akaunti hiyo.
Aidha, imeitaka Takukuru iwachunguze na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo wahusika ili ukweli ufahamike na haki kutendeka.
Sakata la Tegeta Escrow linahusisha uchotwaji wa zaidi ya Sh. milioni 301 zilizokuwa zimetunzwa na Tanesco na kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL, zikiwekwa ndani ya Benki Kuu (BoT).
Mwanzoni mwa mwezi huu Ikulu ilisema viongozi wa Wizara ya Madini na Nishati ni safi na mawaziri waliowajibika kwenye Operesheni Tokomeza hawakuhusika moja kwa moja na mauaji, hivyo hawana hatia.
Taarifa ya Kamati iliwasilishwa bungeni jana na Mwenyekiti Jasson Rweikiza (pichani) , wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma.
Aidha, iliikumbusha Takukuru kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo kuhakikisha kuwa inadhibiti rushwa. “Kwa kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu ambapo uzoefu unaonyesha kuwa vitendo vya rushwa huongezeka kwa kasi katika kipindi hicho, ni dhahiri kuwa taasisi hii itakuwa na kazi kubwa ya kudhibiti vitendo hivyo na kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unakuwa wa haki na kuondoa rushwa za uchaguzi.” Alisema jukumu hilo litafanikishwa kwa kuiwezesha taasisi kifedha, vitendea kazi, watumishi pia ijengee wadau uwezo wa kuelimisha athari za rushwa kwenye uchaguzi na mafunzo kwa sekta ya sheria kuhusu sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya 2010.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, akiwasilisha bajeti yake aliitaka Takukuru kufuatilia na kudhibiti vitendo vya rushwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba. “Wafuatilie rushwa kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu, wakati wa kampeni, uchaguzi na baada ya uchaguzi,” alisema.
Aidha, katika bajeti ya Manejimenti ya Utumishi wa Umma, hakuna ongezeko la mishahara kwa mwaka 2015/16. Kwa mujibu wa bajeti yake kima cha chini hakikupandishwa licha ya kwamba mwaka jana kiliongezeka kutoka 240,000 hadi 265,000 kwa mwezi. Kombani alisema katika mwaka huu serikali itaajiri watumishi wapya 71,496 idadi hii ni ongezeko la watu 13,013 ikilinganishwa na mwaka unaoishia Julai.
Waziri alisema kipaumbele kitaelekezwa kwenye elimu watumishi 28,957 wakati afya wataajiriwa 10,870 na kilimo 1,791. Aidha, itaajiri watumishi wengine 28,748 kadhalika watumishi 113,520 wa kada mbalimbali wakaopandishwa vyeo.
Ikilinganishwa na mwaka jana ajira mpya ilikuwa watumishi 58,483 katika vibali vya kuajiri watumishi 68,138 vilivyoombwa.
Wizara hiyo imeomba Shilingi bilioni 7.7, kati ya hizo bilioni 6.2 ni bajeti ya matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment