Friday, July 29, 2016

Marufuku kufanya kazi za mipangomiji bila kusajiliwa – TPRB

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Bodi ya Usajili ya Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) imewapiga marufuku wanaofanya kazi za Mipangomiji bila kusajiliwa ili kuondoa usumbufu na kupunguza udanganyifu kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo.
Onyo hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Msajili wa Bodi hiyo, Helena Mtutwa katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari kuhusu majukumu ya Bodi hiyo.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 23(4) cha Sheria ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji ya 2007 inasema kuwa ,ni kosa la jinai kufanya kazi hizi bila kusajiliwa kwa hiyo, nawashauri wafanyao shughuli hizo kuacha mara moja”, alisema Mtutwa.
Mtutwa amewataka wananchi wenye sifa zinazowawezesha kusajiliwa na TPRB wafike katika ofisi zao kwa ajili ya kusajiliwa ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza kwao na kwa Bodi hiyo.
Aidha, Msajili huyo amesisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mwananchi yeyote atakayebainika kukiuka agizo hilo.
Bodi  ya Usajili ya Wataalam wa Mipangomiji ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa chini ya Sheria namba 7 ya mwaka 2007 ambapo moja ya majukumu yake ni kusajili wataalam wa Mipangomiji na kusimamia maadili.

No comments:

Post a Comment