Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Serikali
imesitisha waraka wa muongozo uliotolewa kuhusu matumizi ya mihuri kwa
wenyeviti wa Mitaa na vijiji mpaka pale itakaposhirikiana na kukubaliana
namna bora ya kuendesha masuala ya kuhudumia wananchi.
Akizungumza
na baadhi ya wenyeviti wa mtaa, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene amewataka
wenyeviti wa mitaa nchini kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na taratibu
zilizopo.
Mhe.Simbachawene alisema kuwa nia ya kusitisha waraka huo ni kuweka utendaji mzuri baina ya Serikali na watendaji wake wa chini.
“Utaratibu
uliopo uendelee mpaka pale Serikali itakapotoa utaratibu mwingine wa
matumizi mbalimbali ya mihuri hiyo baada ya kujadiliwa na kushirikiana
vya kutosha” alifafanua Waziri Simbachawene.
Mhe.Simbachawene alisema kuwa
kuna baadhi ya wenyeviti wa mitaa wamekuwa wakitumia vibaya mihuri hiyo
na kupelekea migongano na migogoro ya ardhi katika vijiji na mitaa
ikiwemo maeneo ya Ununio, Temeke.
Mbali
na hayo alisema kuwa katika Tangazo la Serikali namba 3 lililotolewa 5
Septemba, 1994 limeeleza baadhi ya vitendea kazi vya mwenyekiti wa mtaa
ni bendera yenye nembo ya Halmashauri, daftari ya kutunza kumbukumbu na
rejista ya makazi.
Alisema
kuwa mamlaka ya mwenyekiti haitokani na mihuri, bali utendaji uliopo
ndani ya mtaa au kijiji husika, hivyo mamlaka ya mwenyekiti ipo pale
pale na haibemwi na muhuri bali muhuri huonesha nguvu ya ofisi baada ya
kuwashirikisha watendaji tofauti ndani ya kijiji katika kutoa maamuzi.
“Mhuri
si mali ya mwenyekiti binafsi, hivyo kwa yeyote atakayekiuka matumizi
ya mihuri hiyo Sheria itachukua mkondo wake” alisisitiza Mhe.
Simbachawene.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya
Temeke Bakiri Makele, ameahidi kushirikiana na Serikali kwa kutumia
mihuri hiyo kwa kufuata Sheria na taraibu zilizopo.
Naye
Katibu wa Wenyeviti hao, Marium Machicha alimshukuru Waziri mwenye
dhamana kwa kauli aliyoitoa baada ya kuliona tatizo hilo na kuahidi
kulifanyia kazi.
Serikali
ilitoa Muongozo huo wa namna wa matumizi ya mihuri kwa wenyeviti wa
mitaa na vijiji kwa sababu ya matumizi mabaya ya mihuri kwa baadhi ya
wenyeviti wa mtaa na vijiji nchini.
0 comments:
Post a Comment