Fatma Salum- MAELEZO
Serikali
imewawezesha watumishi zaidi ya 2000 kumiliki nyumba bora kwa kuwapatia
mikopo yenye riba nafuu na kuchangia kuongeza tija katika utumishi wa
umma.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Nyumba Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Bw. Michael Mwalukasa wakati akizungumza na
waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam.
Mwalukasa
alisema kuwa kupitia Mfuko wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa
Serikali watumishi wengi walioomba mikopo hiyo wameweza kupewa kwa lengo
la kuwawezesha watumishi wa Serikali wa ngazi zote mijini na vijijini
kujenga, kukarabati au kununua nyumba.
“Mfuko
huu umewawezesha watumishi wa Serikali kujenga nyumba kwenye maeneo
yenye hadhi na yanayokubalika kisheria hivyo kuchochea kasi ya
maendelezo ya nyumba kwenye Miji na Wilaya zote hapa nchini” alisisitiza Mwalukasa.
Akifafanua
Mwalukasa amesema kuwa watumishi wanaokopa kwenye mfuko huo hurejesha
mikopo hiyo kwa riba nafuu ya asilimia tatu tofauti na taasisi nyingine
ambazo hutoza riba kubwa.
“Tofauti
na taasisi nyingine ambazo hukopesha nyumba iliyokamilika na kutoza
riba kubwa, mfuko huo unatoa mikopo kwa ajili ya kujenga,kununua na
kuboresha nyumba na kuwapa fursa watumishi kukopa kadiri ya uwezo na
matakwa yao ya ujenzi”. Alisema Mwalukasa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Msaidizi Mikopo ya Nyumba Bibi Lucy Kabyemera
aliongeza kuwa baadhi ya wakopaji pia hunufaika na ushauri wa kutumia
teknolojia ya gharama nafuu za ujenzi kutokana na tafiti zinazofanywa na
Taasisi ya Utafiti wa Vifaa vya Ujenzi wa Nyumba Bora (NHBRA).
Pia
Kabyemera aliwataka watumishi wa Serikali kutumia fursa hiyo ili waweze
kumiliki nyumba bora kwa gharama nafuu katika maeneo yaliyopimwa.
Mfuko
wa Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Serikali ulianzishwa na Serikali
mwaka 1963 kupitia waraka namba 8 na baadae kuendeshwa kupitia waraka wa
watumishi wa Serikali namba 4 wa mwaka 1965.
0 comments:
Post a Comment