Na. Lilian Lundo – MAELEZO
Askofu wa Good News for All Ministry Dkt. Charles Gadi kwa niaba ya dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini wamempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Kamishna wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Dkt.
Gadi ametoa pongezi hizo leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea
na vyombo vya habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO).
“Tunamshukuru Mungu kwa kumuinua Rais ambaye ameonyesha nia na kuwa mstari wa mbele kupigana na biashara hiyo haramu, ni ukweli usiopingika kwamba tatizo la dawa ya kulevya ni kubwa na lenye madhara makubwa sana kwa watanzania wengi haswa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa,” alifafanua Dkt. Gadi.
Aliendelea kwa kusema kuwa, Vijana wengi wamepoteza maisha , kuharibika akili, kupata magonjwa ya kuambukiza, kupoteza malengo
ya kimaisha kwa sababu ya dawa hizo. Vile vile dawa hizo zimeleta
fedheha kwa Taifa kutokana na Vijana wengi wa Kitanzania kuwepo katika
magereza mbalimbali Duniani huku wengine wakisubiri adhabu ya kunyongwa.
Aidha amempongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kuimarisha Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kumteua Kamishna ambaye atasimamia Mamlaka hiyo na anaamini kwamba kwa neema ya Mungu ataweza kumsaidia kikamilifu Rais Magufuli katika kutimiza azma yake ya kukomesha biashara hiyo.
Wakati
huo huo, Dkt. Gadi amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa
kuianzisha vita hiyo dhidi ya matumizi ya dawa kulevya katika mkoa wa
Dar es Salaam. Vile vile amewapongeza waandishi wa habari na vyombo
mbalimbali vya habari kwa kutoa habari zinazosaidia katika upambanaji wa biashara hiyo.
Dkt.
Gadi amewataka viongozi wa Dini kuungana bega kwa bega na Rais Magufuli
kwa kuendelea kutoa maadili kwa vijana ili kuepukana na uovu wa dawa za
kulevya nchini.
0 comments:
Post a Comment