Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa
waandishi wa habari nchini kuandika habari zinazohamasisha maendeleo ya
nchi badala ya kuandika habari ambazo hazina manufaa kwa taifa.
Akizungumza
wakati ya hafla ya kuwaapisha mawaziri, mabalozi pamoja na Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais Magufuli alisema kuwa
waandishi wa habari wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuandika habari za
kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo pamoja na
kuunga mkono jitihada mbalimbali za Serikali.
“Nchi
yetu ina sifa nzuri nje, Rais wa Benki ya Dunia alipotembelea katika
nchi yetu hivi karibuni alitupatia jumla ya shilingi trilioni 1.74 na
benki hiyo ipo mbioni kutupatia fedha nyingine shilingi trilioni 2.8,
lakini vyombo vyetu vya habari haviandiki kwa mapani juu ya taarifa ”
alisema Rais Magufuli.
Alibainisha
kuwa fedha hizo zitatumika katika miradi ya Ujenzi wa barabara za juu
eneo la Ubungo, maboresho ya miji, pamoja na Vyuo Vikuu vya Sokoine na
Mandela na kuleta maendeleo ya nchi yetu lakini taarifa zake hazikupewa
uzito unaostahiki katika vyombo vya habari.
Rais
Magufuli aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa
habari kufuata uweledi wa taaluma ya habari pamoja na kuweka mbele
maslahi ya taifa badala ya maslahi ya mtu mmoja mmoja.
Aidha,
Rais Magufuli amewapongeza viongozi aliowaapisha na kuwataka
kufanyakazi kwa bidii na juhudi ili kutimiza azma ya serikali ya kuwa
nchi ya uchumi wa kati kwa kutekeleza agenda ya viwanda.
Viongozi
walioapishwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.
Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi
na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Alfayo Kidata.
Wengine
ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dkt. Abdallah Possi, Balozi wa
Tanzania nchini Israel Job Masima, Balozi wa Tanzania nchini Comoro,
Sylvester Mabumba pamoja na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
Stellah Mugasha.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment