BENKI Kuu Tanzania (BoT) imesema, Tanzania ni miongoni mwa nchi za
Afrika zenye viwango vya juu vya ukuaji wa uchumi katika kipindi cha
muongo mmojauliopita (2007 - 2016).
Mkurugenzi wa Uchumi BoT, Johnson Nyella amesema uchumi wa Tanzania
ulikua kwa wastani wa asilimia 6.7 mwaka 2016, wakati pato la taifa
lilikua kwa wastani wa asilimia 7, sawa na ilivyokuwa mwaka 2015 na
2014.
Nyella alisema hayo jana wakati wa sherehe ya Siku ya Takwimu Afrika
(2017), iliyofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa
kiongozi huyo wa Bot, kwa miaka minne mfululizo, mfumuko wa bei wa Taifa
umeendelea kupungua na kubaki katika kiwango cha tarakimu moja.
“Mwaka 2016 mfumuko wa bei ulipungua na kufikia wastani wa asilimia
5.2 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2015 na asilimia 6.1
mwaka 2014,” alisema.
Nyella alisema, takwimu bora za uchumi zinahitajika katika kupanga
mipango ya maendeleo na utungaji wa sera kwa ajili ya kuboreshamaendeleo
endelevu ya mwaka 2030. Kwa mujibu wa Nyella, takwimu bora za kiuchumi
zinasaidia kuongeza tija serikalini katika kupanga mipango ya maendeleo
na kukabiliana na changamoto kadri zinavyojitokeza.
Alisema takwimu bora pia zinawasaidia watunga sera na watekelezaji wa
programu mbalimbali na kupanga mikakati mipya ya kuboresha maisha ya
wananchi.Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina
Chuwa alisema kwenye sherehe hizo kuwa, takwimu bora za uchumi ni muhimu
katika kufikia ajenda ya Bara la Afrika ya mwaka 2063 inayosisitiza
ukuaji wa uchumi wa Bara hilo.
Katika kufikia ajenda hiyo, baadhi ya mambo yanayosisitizwa ni amani,
utulivu, kuboresha uchumi wa Afrika, kukusanya mapato ya Afrika ili
Afrika iweze kujitegemea. Kwa mujibu wa Dk Chuwa, ajenda ya Afrika ya
Mwaka 2063 haiwezi kufanikiwa bila takwimu bora za uchumi.
Alisema Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi ya Afrika (UNECA) kwa
kushirikiana na Ofisi za Takwimu za Afrika, ina kaulimbiu isemayo
“Takwimu Bora za Uchumi kwa Maisha Bora” ikisisitiza umuhimu wa takwimu
za kiuchumi katika kuleta maendeleo endelevu hivyo kuboresha maisha ya
wananchi.
Dk Chuwa alisema kaulimbiu hiyo inaakisi juhudi za Serikali ya Awamu
ya Tano ya Rais John Magufuli kwa kuwa na dhamira ya kutengeneza uchumi
wa viwanda. Alisema kwa sababu hiyo, takwimu rasmi za uchumi za serikali
lazima zitolewe kwa weledi na kwa kufuata kanuni na sheria. “Takwimu
bora za uchumi kwa nchi yetu ni za muhimu sana, hasa wakati huu ambao
Serikali yetu inaimarisha uchumi wa viwanda ili Tanzania iweze kuwa nchi
ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na kuboresha zaidi maisha ya
wananchi.
Takwimu hizi za uchumi ni pamoja na takwimu za kilimo, viwanda,
ujenzi, usafirishaji, nishati, biashara, mazingira, mfumuko wa bei na
uwekezaji,”alisema. Dk Chuwa alisema, ili takwimu zitumike kwa ajili ya
kuboresha maisha ya wananchi, zinatakiwa kuwa bora na za kuaminika.
Alisema takwimu bora ni takwimu zilizo sahihi, zinazotolewa kwa
wakati, linganifu na za kina, zinazozalishwa mara kwa mara na zenye
ufanisi. Dk Chuwa alisema, sifa hizo zote zinaendana na kanuni za msingi
za takwimu rasmi za Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Takwimu wa Afrika,
ambazo maisha ya wananchi, hasa kutekeleza ajenda.
CHANZO HABRI LEO
0 comments:
Post a Comment