Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam
SUALA
La Bima ya Afya kwa wote limetakiwa kupewa kipaumbele zaidi katika
maandalizi ya Dira ya Taifa 2050 ili kuboresha zaidi huduma za afya ili
kila mtanzania awe na afya bora na kuweza kulitumikia Taifa.
Akizungumza
leo jijini Dar es Salaam katika kongamano la kitaifa la wadau wa sekta
ya ya Afya kuhusiana na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema, Katika kuijenga Tanzania tuitakayo
lazima wananchi waone umuhimu wa kuwekeza katika afya na kuingizwa kwa
suala la Bima ya Afya kwa wote katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050 kutasaidia kuboresha huduma za afya nchini.
Akieleza mafanikio ya sekta hiyo Waziri Ummy ameeleza kuwa ni pamoja na
kufanikiwa kwa kiwango cha juu kwa wanawake kujifungulia katika Vituo
vya Afya, kwa kuongezeka kutoka asilimia 41 mwaka 2000 hadi kufikia
asilimia 81 kwa sasa na mpango ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka
2025.
Waziri Ummy amesema changamoto kubwa katika sekta ya afya
ni ugharamiaji wa huduma za afya, huku akitaja changamoto kubwa kuwepo
katika magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo, kisukari na afya ya akili.
"Tukiwa
na Bima ya afya kwa wote tutafanikiwa kwa kuwa huduma za afya ni kila
kitu, Nchi nyingi katika uchaguzi angalieni Marekani, Uingereza na
kwingineko kampeni kubwa ni kuhusu bima ya afya na hifadhi ya jamii,
kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika gharama za matibabu.” Amesema
Ummy.
Aidha kuhusiana na changamoto ya ugharamiaji huduma za
matibabu kwa wasiojiweza Waziri Ummy ameeleza kuwa, baada ya muswada
kuwa sheria na kuona namna gani watanzania wasio na uwezo watachangia
Rais Samia Suluhu Hassan alielewa suala hilo.
“Na tayari chanzo
cha ugharamiaji kimepatikana sasa hivi kitagharamia wazee wasio jiweza,
watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wajawazito na tutaanzia kwa
watoto wa umri sifuri mpaka miaka miwili," ameeleza Waziri Ummy.
Akizungumza
katika Kongamano hilo Waziri wa Nchi; Ofisi ya Rais Mipango na
Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema tafiti imeonesha kuwa asilimia 81
ya Watanzania wanahitaji mabadiliko katika huduma za kijamii ikiwemo
uboreshaji wa huduma za afya.
Maoni hayo yaliyokusanywa na Tume
ya Mipango kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutoka kwa watanzania
zaidi ya milioni moja, asilimia 81 ya waliohojiwa walipendekeza
uboreshaji wa huduma za afya huku asilimia 19 wakitaka upatikanaji wa
huduma za afya.
Ameeleza kuwa maoni ya wadau hao ni muhimu na
yatapewa kipaumbele katika kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
inaleta tija kwa jamii.
Wadau wa sekta ya afya nchini, wametoa
maoni yao na kushauri kupewa kipaumbele kwa Bima ya Afya kwa wote ili
kuboresha huduma zinazotolewa pamoja na kuwekwa kwa mfumo rasmi katika
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kupambana na changamoto ya ajira kwa
wahitimu wa kada ya Afya wakiwemo madaktari na wauguzi kwa kuwa kada
hiyo ni muhimu na wanahitajika zaidi katika jamii hivyo kukosekana kwa
wataalam hao huchagiza changamoto ya ubora wa huduma.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma (BMH,) Prof. Abel Makubi
akitoa maoni katika kongamano hilo amesema kuwa ni muhimu kuwa na
mikakati ili fedha inayowekezwa katika kusomesha na mafunzo kwa
wataalamu hao ilete tija kwa jamii.
Pia Katibu Mtendaji; Tume wa
Mipango Lawrence Mafuru amesema mwongozo na usimamizi wa matayarisho ya
Dira hiyo ulipitishwa na Baraza la Mawaziri na utakuwa sheria pindi
utakapokamilika rasmi na kuongeza kuwa michango mingi katika simu na
midahalo watanzania wanahitaji huduma bora za afya na kueleza kuwa maoni
yatakusanywa hadi Agosti mwaka huu na baadaye kupangwa kwa ajili ya
utekelezaji.
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imejikita katika
maeneo sita ikiwemo maboresho ya Utawala bora, Haki na Amani,Uchumi na
Jamii,Utunzaji wa mazingira sayansi ya mabadiliko ya kidijitali na
mabadiliko ya tabia Nchi.
Wadau walioshiriki kongamano hilo ni
pamoja na Taasisi za Utafiti, wamiliki wa vituo binafsi vya Afya,
Taasisi za Elimu, watoa huduma za Afya, Waganga wakuu wa mikoa na
wataalam wa Afya.
0 comments:
Post a Comment