Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » CCM NI RAIS MWANAMKE?

CCM NI RAIS MWANAMKE?

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

  Ni kati ya Dk. Migiro, Spika Makinda na Profesa Anna Tibaijuka
  Kufuata nyayo za Dilma Rousseff, Angela Merkel na Ellen Sirleaf
Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro
Uvumi na tetesi vimeanza kutanda mitaani, kwenye vyama vya siasa na kwenye vikundi vya wapambe kwamba huenda mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwakani akawa mwanamke.
Vyanzo mbalimbali vya habari ambavyo vimezungumza na NIPASHE vimegusia uwezekano wa CCM kumteua mgombea urais mwakani kwa sababu kuu moja, kukata makali ya makundi makubwa ya wanaume ambao wamejipanga kwa nguvu zote kurithi viatu vya Rais Jakaya Kikwete mwakani.

“Unafikiri kwa hali ilivyo sasa ni nguvu gani hasa itatumika kuzuia miamba ya siasa za CCM? Unakumbuka livyolivyokuwa suala la uspika mwaka 2010? Sitta (Samuel) angezuiwa je asigombee tena uspika kama siyo mizengwe ya jinsia?” kiongozi mmoja ndani ya CCM alikumbusha jinsi Sitta alivyokosa uspika kwa maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM kuwa ili zamu ya mwanamke kuwa spika.

Vyanzo kadhaa vya habari vinasema kuwa kutokana na makundi ya urais yaliyojipanga yakitawaliwa  na wanaume zaidi, huku wengi wakihasimiana, huenda karata ya jinsia ikatumika kama njia ya kuyavunja nguvu.

Tangu Tanganyika ipate uhuru mwaka 1961na kisha kuungana na Zanzibar mwaka 1964 na kuzaliwa Tanzania, imeongozwa na marais wanne, wote wanaume.

Hawa ni Rais wa Kwanza ambaye pia ni muasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere, alitawala tangu uhuru hadi 1985 alipoamua kung’atuka kwa hiari; akiacha mikoba kwa Rais Ali Hassan Mwinyi  mwaka 1985 -1995; Rais Benjamin Mkapa mwaka 1995-2005 na Kikwete kuanzia 2005 na anatarajiwa kumaliza kipindi chake mwakani.

Katika vinywa vya watu, wanawake wanaotajwa ndani ya CCM ni pamoja na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Spika wa Bunge la Jamhuri, Anne Makinda.

Ingawa pia wapo wanawake wengine wanaotajwa, watatu hao wamo zaidi kwenye vinywa vya wengi kwa sababu ya wasifu wao.

Makinda ni mwanamke wa kwanza kuwa Spika wa Bunge la Tanzania nafasi ambayo ilikaliwa na maspika wengine wanne wote wakiwa wanaume.
Maspika walioongiza kabla ya Makinda ni pamoja na Adam Sapi Mkwawa; Erasto Mang’enya; Pius Msekwa na Sitta.

Makinda anatajwa kuwa mwanamke wa kwanza Mtanzania kushika wadhifa wa juu zaidi katika mihimili ya dola, huku pia akiwa amekuwa Naibu Spika kwa miaka mitano chini ya Sitta.

Mwanamama huyu amekuwa Mbunge wa Jimbo la Njombe Kusini tangu 1995 hadi sasa, pia aliteuliwa kuwa mbunge mara ya kwanza mwaka 1975. Ameshika nyadhifa mbalimbali za uwaziri tangu awamu ya kwanza na ya pili.

Migiro anatajwa kuingia katika siasa mwaka 2000 alipokuwa mbunge wa viti maalum na kuchaguliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, lakini mwaka 2006 -2007 alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon alimteua kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN Februari 05, 2007 hadi Julai 01, 2012.Profesa Tibaijuka aliingia bungeni mwaka 2010 na kuteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nafasi anayoshikilia hadi sasa.

Profesa Tibaijuka ana wasifu unaofanana na Migiro, wote walikuwa wahadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tibaijuka akiwa ni Profesa wa uchumi, wakati Migiro ni daktari wa falsafa wa sheria.

Tibaijuka pia alishakuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat kuanzia mwaka 2000 hadi 2006.

Pamoja na tetesi za wanawake kuingia ulingoni mwakani kuwania urais, NIPASHE ilifanya mahojiano kwa nyakati tofauti na makatibu wakuu wa vyama vikubwa vya siasa kutaka kujua maoni hao juu ya upepo huo wa kisiasa nchini kwa sasa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, ambaye mwaka 2010 aligombea urais na kushika nafasi ya pili baada ya Kikwete, alisema kimsingi hakuna mahali popote katika sheria za Tanzania, katiba au sheria za uchaguzi zinazokataza mwanamke asigombea urais kwani msingi wa kugombea ni katiba na sheria za nchi.

Alisema kunapokuwa na hoja ya kwamba umefika wakati sasa Tanzania kuwa na rais mwanamke inajenga hoja kwamba inawezekana hapo awali walikuwa wamezuiwa kugombea na sasa zuio limeondolewa wakati hakuna jambo kama hilo.

“Suala la wanawake kugombea nafasi za juu za uongozi ni jambo zuri kinachotakiwa ni kuwahamasisha ili wajitokeze kugombea maana suala la mtu kugombea ni la kwake mwenyewe,” alisema na kuongeza:

“Mwanamke kugombea urais hajakatazwa, lakini Tanzania bado hatujafikia hatua ya kusema safari hii ni zamu ya mwanamke au mwanaume kugombea urais.”

Alisema ni makosa kufikiria kwamba urais ni jinsia (gender) wakati kinachoangaliwa zaidi ni sifa za mtu bila kujali jinsia yake.
Aliongeza kuwa Tanzania kwa sasa inahitaji rais anayefahamu matatizo ya wananchi na ana uwezo wa kukabiliana nayo bila kujali kuwa ni mwanamke au mwanaume.

“Rais anayetakiwa ni yule mwenye uwezo wa kutukwamua tulipokwama na kutupeleka mbele. Sifa zinatokana na katika kipindi cha miaka 50 umefanya nini kwa wananchi,”alisema.

Kwa upande wake  Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sayaka, alisema uchaguzi mkuu 2015 ni muda muafaka wa Tanzania kuwa na rais mwanamke kwa sababu kwa sasa Tanzania ina wanawake wasomi, wenye weledi mkubwa  na uwezo wa kuongoza nchi.

Alisema kwa miaka 50 wanaume wameongoza na wameshindwa kutumia rasilimali za taifa hili kuondoa umaskini, maradhi na ujinga.

Sakaya ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum CUF, alisema miaka 50 na ushei baada ya uhuru bado maadui wakuu umaskini, ujinga na maradhi yanaumiza Watanzania, marais wanaume wameshindwa kuondosha maadui hao, kwa hiyo sasa wanawake wapewe nafasi ili kutoa mchango wao kutokomeza maadui hao ambao wanaathiri zaidi wanawake na watoto.

“Wanawake wengi tuko ‘dedicated’(wanajitoa)  kwa nafasi tunazopata, wanawajibika, wanajituma na ni waaminifu wanapenda kufanya vitu vionekane,”alisema.

Aliongeza kuwa kilichofikisha taifa hili hapa lilipo ni viongozi kukosa uchungu na uzalendo, kuwa wabinafsi, walafi wa mali, kujilimbikizia mali, kila anayepata nafasi anapanga kuchota kilichopo siyo kuongeza alichokikuta.

Sakaya alisema kutokana na ulafi wa mali, hivi sasa viongozi wengi ni mabilionea wakati Watanzania wengi ni maskini.

Alisema chama kilichopo madarakani na viongozi wake wameshindwa kuleta mabadiliko, hivyo ni wakati sasa nchi kuongozwa na rais mwanamke.Naye Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Mosena Nyambambe, alisema Tanzania kuwa na rais mwanamke siyo hoja ya msingi bali viangaliwe vigezo na sifa za rais na kama atakuwa ana sifa hakuna tatizo.

Alisema wanaume wanaojitokeza kugombea urais hususani wa kutoka vyama vya upinzani ni kutokana na katiba na mfumo mbovu wa utawala.Nyambambe alisema kama CCM itaendelea kutawala na katiba na mfumo uliopo sasa wa utawala mbovu hata wanawake watashindwa kuongoza nchi kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema suluhisho la tatizo hilo ni kupata katiba mpya na chama kingine kitakacholeta mabadiliko.

NIPASHE iliwatafuta viongozi wa CCM kwa siku kadhaa, Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana; Naibu Katibu Mkuu Bara, Mwigulu Nchemba na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wote simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa na hata ujumbe mfupi wa maandishi waliotumiwa hawakujibu.

MARAIS WANAWAKE WANAOTAMBA
Wakati upepo wa kisiasa ukielezwa kuvuma kuwainua wanawake nchini mwakani, kwingine duniani, wanawake wanaotamba katika anga za kisiasa ni pamoja na Rais Dilma Rousseff wa Brazil; Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Cristina Fernandez de Kirchner wa Argentina na Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia.

RAIS DILMA ROUSSEFF
Rais Rousseff ni mtoto wa mhamiaji kutoka Bulgaria.Anayo historia ya kukimbilia msituni kwa ajili ya kupambana dhidi ya serikali iliyokuwa ikiongoza Brazil kwa mkono wa chuma, na hivyo akajikuta akionja machungu ya mateso ya serikali.

Kabla ya kuukwaa urais mwaka 2011, mama huyu ambaye ni mchumi alipitia ngazi mbalimbali za uongozi zikiwamo za uwaziri wa nishati na ukuu wa utumishi serikalini.

Alizaliwa katika mji wa Belo Horizonte, ulio Kaskazini mwa jiji la Rio de Janeiro mwaka 1947.Baba yake alikuwa ni mkimbizi wa kisiasa toka Bulgaria aliyehamia Brazil kwenye miaka ya 1920, aliitwa Pedro Rousseff na mama yake ambaye alikuwa mwalimu aliitwa Dilma, jina ambalo analitumia.

Elimu yake ilianzia kwenye shule ya masista iliyokuwa ikifundisha kwa Kifaransa, kabla ya kwenda kwenye shule ya serikali kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita ambako ndiko moto wake wa kisiasa ulipoanzia.

MAISHA YAKE SHULENI NA MAPINDUZI YA 1964
Mwaka 1964 Jeshi la nchi hiyo liliipindua serikali ya mrengo wa kushoto ya rais Joao Goulart iliyoingia madarakani mwaka 1961.
Yalikuwa ni mapinduzi ya tano katika kipindi cha miaka 20 yaliyofanywa na jeshi, na safari hii jeshi lenyewe likishika usukani wa kuongoza nchi, katika mapinduzi ambayo yaliungwa mkono na serikali ya Marekani.

Chini ya udikteta wa kijeshi, haki zote za kiraia zilifutwa na matukio ya watu kukamatwa, kupotezwa na kuteswa yakawa ya kawaida.
Mbaya zaidi nusu ya bajeti ya serikali kwa upande wa elimu ilikatwa.

Akiwa katika shule hiyo ya serikali Rousseff alivutiwa na maandishi ya Regis Debray mwanafalsafa wa Kifaransa pamoja na ya mwalimu wake mmoja aliyemfundisha mrengo wa Kimarx na ambaye baadaye alikuja kuwa komredi mwenzake.

Shule hiyo ilikuwa kitovu cha harakati za wanafunzi dhidi ya udikteta na mwaka 1967, Rousseff alijiunga na kikundi cha kiharakati cha chama cha Brazilian Socialist Party.

Baadhi ya vijana wenzake aliojiunga nao wakati huo katika kikundi hicho ni wanasiasa leo hii akiwa madarakani, kama vile Carlos Minc aliye waziri wa mazingira, Fernando Pimentel, meya wa zamani wa jiji la Belo Horizonte ambaye sasa ni mshauri wake.

Baadaye alikuja kukutana na Claudio Galeno Linhares, mwandishi na mwanaharakati mwenzake ambaye alikuja kumuoa mwaka 1968.

MAPAMBANO YA SILAHA
Kundi lao lilikuja kuungana na makundi mengine na kuwa kundi moja lililojulikana kama Colina (National Liberation Command).

Lilianzisha mapambano ya silaha dhidi ya serikali ya kidikteta iliyokuwa ikitawala Brazil wakati huo.

Mnamo mwaka 1969 polisi waliivamia nyumba ya kikundi chao, ambapo katika makabiliano hayo, polisi wawili walipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya.

Yeye na Galeno walikimbilia katika jiji la Rio de Janeiro, ambapo baadaye Galeno alikimbilia katika mji wa Porto Alegre, na yeye akibakia Rio de Jeneiro ambapo alikutana na mwanasheria maarufu na wa mrengo wa kushoto Carlos Araujo.

Waliendelea kuungana na vikundi vingine na baadaye akaelekea katika jiji la Sao Paulo.

AKAMATWA NA KUTESWA
Mnamo mwaka 1970 Rousseff alikamatwa baada ya kujitokeza bila kutarajiwa kwenye baa moja wakati mpiganaji mwenzake alipokuwa akikamatwa na polisi kwenye operesheni iliyoendeshwa na jeshi hilo, Januari 16, 1970.

Kilichofuata ni siku 22 za mateso makali aliyoweza kuyavumilia, yakiwamo ya kushtuliwa kwa umeme na mengine yakilenga kuleta maumivu kwenye viungo na misuli.

Baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela na miaka18 ya kutokuwa na haki ya kushiriki kwenye shughuli za kisiasa.
Hata hivyo, kifungo hicho kilipunguzwa hadi miaka mitatu, na hivyo mwaka 1973 alitoka gerezani.

UTOTO HADI MAISHA YA SIASA
Mara baada ya kutoka gerezani alihamia katika jiji la Porto Alegre, anakotoka mwanasheria na komredi mwenzake Araujo.
Alirudi masomoni baada ya kutoka gerezani na mwaka 1977 alihitimu shahada ya uchumi.

Alijifungua mwaka 1976 mtoto wake aitwaye Paula aliyezaa na Araujo ambaye sasa ni mwanasheria.

Alifanikiwa kupata kazi serikalini, lakini akaipoteza kutokana na rekodi yake ya nyuma na akaamua kurudi masomoni baada ya tukio hilo kwa ajili ya kusoma shahada ya uzamili.

Mwanzoni mwa miaka ya 1980 wakati majenerali wa kijeshi walipolegeza kidogo misimamo yao, Rousseff na komredi mwenzake Araujo walirudi kwenye ulingo wa kisiasa.

 Sasa wakiwa katika chama cha Democratic Labour Party (PDT) kilichoongozwa na Leonel Brizola, shemeji yake rais Joao Goulart aliyepinduliwa na jeshi mwaka 1964.

Chama hicho cha PDT kilishinda chaguzi na Rousseff akapewa nafasi mbalimbali zikiwamo za ushauri katika ngazi za chini na za kitaifa.
Mwaka 1993, Gavana wa Taifa wa Rio Grande do Sul alimteua kuwa waziri wa nishati.

Hata kabla hajamaliza shahada yake ya uzamili alijisajili kwa ajili ya shahada ya uzamivu ambapo napo alikuja kukatisha.
Mwaka 1999, aliteuliwa kuwa waziri wa migodi, nishati na mawasiliano.

AJIUNGA NA CHAMA CHA WAFANYAKAZI

Mwaka 2001 kiongozi wa chama chao cha PDT aliwalazimisha mawaziri waliokuwa serikalini kutoka chama hicho wajiuzulu.
Badala ya kujiuzulu Rousseff aliamua kukihama chama hicho na kujiunga na Workers’ Party kilichokuwa kikiongozwa na Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa nchi hiyo.

Hata hivyo mwaka 2002 aliondoka serikalini kwa ajili ya kusimamia kampeni ya urais wa Lula ambapo alishinda, na Lula alimteua tena kuwa waziri wa madini na nishati. 
Mwaka 2003, taifa la Brazil lilingia kwenye mgawo wa umeme baada ya mabwawa kukauka kutokana na ukame na miongo ya uwekezaji duni kwenye vyanzo vya umeme.

AWA MKUU WA UTUMISHI
Mwaka 2005 ilitokea kashfa iliyolazimisha mkuu wa utumishi katika serikali ya Lula kujiuzulu na Rais akamteua kuchukua nafasi ya ukuu wa utumishi serikalini.

Miaka michache baadaye minong’ono ikaanza kusikika kuwa ndiyo chaguo la rais Lula kumrithi atakapomaliza kipindi chake cha urais.
Na ndivyo ilivyotokea kwani mwaka 2010 alishinda kiti cha urais na kuwa mwanamke anayeongoza taifa la saba kwa uchumi mkubwa duniani.

ANGELA MERKEL
Angela Dorothea Kasner alizaliwa Julai 17, mwaka 1954 katika jiji la Hamburg huko Ujerumani. Baba yake ni Horst Kasner na mama ni Herlind Kasner, akiwa na ndugu watatu.

Alikulia kwenye mji mdogo wa Templin, maili 50 kaskazini mwa Berlin, kwenye ile iliyokuwa Ujerumani Mashariki, ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikufuata siasa za kisoshalisti.

Na siasa zake zinaanzia kwenye jumuiya ya umoja wa vijana wa kisoshalisti wa Ujerumani  Mashariki.
Ni kupitia kwenye jumuiya hii ya umoja wa vijana, ndipo alipoonyesha ujuzi wake wa uongozi akiwa na umri mdogo, akianzia na uwakilishi wa bodi na katibu wa kikundi cha vijana cha Agitprop.

Familia yao, ikiongozwa na baba yake aliyekuwa mchungaji wa Kilutheri hawakuwa na shida na mtazamo wa kikomusti uliokuwa ukifuatwa Ujerumani ya Mashariki, kwa kuwa walipewa uhuru ambao haukutolewa kwa wachungaji wengine Wakristo.

Walikuwa na ruhusa ya kuvuka mpaka kwenda Ujerumani Magharibi na kurudi na pia walimiliki magari.

Baada ya masomo yake katika mji wa Templin, alijiunga na masomo ya Fizikia katika chuo kikuu cha Leipzig kutoka mwaka 1973 hadi 1978 na kuhitimu shahada ya uzamivu.

Alifanya kazi kwenye kituo kikuu cha Fizikia Kemia katika Chuo Cha Sayansi cha Berlin- Adlershof toka mwaka 1978 hadi mwaka 1990.
Mwaka 1977, Angela Kasner aliolewa na mwanafizikia Uirich Merkel na wakatalakiana mwaka 1982.

Aliolewa tena mwaka 1998 na Joachim Sauer, Profesa wa kemia kutoka Berlin ambaye wanaishi naye hadi sasa.

Kansela Merkel aliingia kwenye ulimwengu wa siasa kwa mara ya kwanza mwaka 1989, baada ya kuangushwa kwa ukuta wa Berlin.

Alijiunga na chama kipya kilichoanzishwa Ujerumani Mashariki cha Democratic Party (Demokratischer Aufbruchfirst).

Kwenye uchaguzi pekee wa kidemokrasia uliofanyika Ujerumani ya Mashariki, Merkel alichaguliwa kuwa naibu msemaji wa serikali mpya iliyokuwa ikiongozwa na Lother de Maiziere.

Baada ya kuunganika kwa Ujerumani Mashariki na Magharibi chama chao kiliungana na chama cha Christian Democratic Union Party (CDU).
Kwenye uchaguzi wa kwanza uliofuata baada ya muungano wa vyama hivyo, alichaguliwa kuingia kwenye bunge la Ujerumani (Bundestag).

Aliteuliwa na Kansela Helmut Kohl kuingia kwenye baraza lake la mawaziri kama waziri wa wanawake na vijana.

Mwaka 1994 aliteuliwa kuwa waziri wa mazingira na usalama wa vinu vya nyuklia, nafasi ambayo kwa kiasi kikubwa ilimjengea msingi wa maisha yake ya kisiasa.

Wakati serikali ya Kohl iliposhindwa katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1998, Merkel akawa katibu mkuu wa CDU; na baada ya kashfa ya fedha iliyotokea mwaka 1999, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza mwanamke wa chama hapo Aprili 10, 2000.

Aliasisi mabadiliko makubwa ndani ya chama cha CDU ambacho kabla ya yeye kuchaguliwa kilikuwa kikitawaliwa na wanaume wahafidhina, chenye mizizi ya Ukatoliki na ngome kubwa magharibi na kusini mwa Ujerumani.

Merkel alikuwa na ngome ya wapiga kura wake huko Ujerumani magharibi.Kwa sifa hizi alitokea kuwa mashuhuri sana kati ya Wajerumani kiasi cha kuwa chaguo lao kwenye nafasi ya Ukansela kuwakilisha CDU na vyama vingine ndugu katika uchaguzi wa mwaka 2002.

Chaguzi hizo hata hivyo hazikwenda vizuri, kwani Merkel alipoteza nafasi hiyo kutokana na kutoungwa mkono na chama chake.

Alihujumiwa na kiongozi wa CSU, Edmund Stoiber aliyeshinda kukiwakilisha chama cha CDU/CSU kugombea ukansela, lakini akashindwa vibaya na Grhard Schoroder.

Baada ya Stoiber kushindwa, mbali na Merkel kuwa mwenyekiti wa CDU, pia alichaguliwa kuwa kiongozi wa upinzani katika bunge dogo la Bundestag.

Katika kipindi chake kama kiongozi wa upinzani, Merkel alitetea kubadilishwa kwa sera nyingi kuhusu mfumo wa uchumi wa Ujerumani, kama vile kuwa na uhusiano ulio imara kati ya nchi hiyo na Marekani.

Ingawaje sera zake wakati mwingine hazikupendelewa sana na Wajerumani, umaarufu wake haukupungua.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, si kwamba alishinda tu tiketi ya kuiwakilisha CDU/CSU kugombea kiti cha Ukansela, bali alimshinda kansela wa zamani Gerhard Schroder na kuwa kansela wa kwanza mwanamke na pia kutoka Ujerumani Mashariki.

Tangu alipoapishwa kuwa kansela Novemba 22, 2005, Merkel aliongoza muungano wa CDU, CSU na chama cha Social Democratic Party (SPD), wakati huo huo akiendeleza ajenda zake za uchumi wa soko huru na mahusiano na Marekani.

CRISTINA FERNANDEZ DE KIRCHNER
Cristina Fernandez de Kirchner alizaliwa Februari 19, mwaka 1953 katika jiji la La Plata, mji mkuu wa jimbo la Buenos Aires ambako ndipo aliposoma na kuhitimu sheria.

Aliolewa na Kirchner ambaye walikutana naye Chuo kikuu cha taifa cha La Plata mwaka 1975, na mwaka mmoja baadaye waliweka makazi yao katika mji wa Santa Cruz, ambako walifungua kampuni ya uwakili

Mwishoni mwa miaka ya 1980, ndipo alipojiingiza kwenye maisha ya kisiasa, baada ya demokrasia kurejea katika nchi hiyo.
Alikuwa ni mjumbe wa jimbo kwenye mkutano mkuu wa chama cha Justicialist Reronist Party (PJ) uliofanyika mwaka 1985 na baadaye akachaguliwa kuingia kwenye bunge la jimbo, akianzia na ngazi ya jimbo na kisha kwenye nyadhifa za kitaifa.

Alikuwa ni mumewe aliyeanza kupata madaraka aliposhinda kiti cha umeya wa jiji la Rio Gallegos mwaka 1987 na mnamo mwaka 1991 akachaguliwa kuwa gavana wa Santa Cruz.

Mwaka 1995 Rais Cristina alichaguliwa kuiwakilisha Santa Cruz kwenye seneti ya nchi hiyo akitumikia vipindi viwili vya kati ya miaka 1995-97, na 2001-05.

Kati ya mwaka 1997-2001aliteuliwa kuingia kwenye Chama cha Manaibu (Chamber of deputies).
Akiwa kwenye Congress, alikuwa ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais Carlos Menem akipiga kura mara kwa mara za kukwamisha mipango ya bunge.

Ilipofika mwaka 2003, mumewe Kircher aligombea urais akishindana na rais Menem aliyekuwa akiwania muhula mwingine ambapo aliamua kujitoa katika mzunguko wa pili baada ya kuona anashindwa na Kircher.

Wakati mumewe alipochukua kiti cha urais mwaka 2003, tayari rais Cristina alikuwa ameshajenga jina katika duru za kisiasa, kipindi ambacho kilikuwa cha hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.

 Alihusika kwa mapana kuziunga mkono na kuzipigania sera za mumewe zilizojumuisha uboreshaji wa matumizi ya kijamii.

Mwaka 2005 rais Kirchner aliingia kwenye mapambano na rais wa zamani Eduardo Duhalde kuhusiana na kuwa na mamlaka ndani ya chama chao cha PJ katika jimbo muhimu la Buenos Aires, ambalo asilimia 38 ya wananchi wa taifa hilo wanaishi.

Msuguano ulifikia ukomo Oktoba ya mwaka huo wakati Cristina alipopambana na mke wa rais Duhalde, Hilda Gonzalez de Duhalde kwenye uchaguzi wa useneta wa jimbo.

Katika kinyang’anyiro hicho Cristina alishinda kwa asilimia 46 ya kura akimshinda kiraisi mpinzani wake huyo ambaye aliishia kwa kupata asilimia 20 tu.

Ushindi huu wa Cristina si tu ulimuonyesha mumewe rais Kirchner kama kiongozi asiye na mpinzani ndani ya chama cha PJ, lakini vile vile ulidhihirisha kuongezeka kwa ushawishi wa kisiasa wa Cristina na ukaondoa zile tuhuma za kutokuwa na udhaifu wakati mwenyewe alipogombea urais mwaka 2007.

Wakati wa utawala wa mumewe, hakukuwa na maamuzi yaliyofanywa bila ya yeye kuwa na usemi, kwa kuwa ushawishi wake ulizidi kwa mbali ule wa watunga sheria.

Alikuwa ni seneta wa kwanza kuwa na ofisi Ikulu, kitu kilichoibua lawama toka kwa vyama vya upinzani.

Chama tawala kilisisitiza kwamba ofisi hiyo ilikuwa ndogo na ilianzishwa kwa heshima yake kama mke wa rais.

Mnamo mwaka 2007 mumewe rais Kirchner aliamua kutogombea urais kwa muhula mwingine, na ndipo yeye rais Cristina alipoamua kuingia kwenye kinyang’nyiro hicho.

Uchaguzi ulipofanyika Oktoba 28 mwaka huo alipata asilimia 45 ya kura zote zilizopigwa, karibu mara mbili ya mshindani wake wa karibu Elisa Carrio aliyepata asilimia 23.

Alichukua madaraka Desemba 10, 2007 kwa muhula wa miaka minne, na mara tu baada ya kushika hatamu alikumbana na malalamiko kutoka taifa la Marekani.

Marekani walimtuhumu kuwa kwa  fedha haramu kwa ajili ya kampeni yake zilizotumwa kutoka serikali ya Venezuela wakati huo ikiongozwa na Hugo Chavez.

Alishinda tena kinyang’anyiro cha urais kwa muhula wa pili Oktoba 2011, kwa ushindi wa kishindo.

Kilichompa ushindi pamoja na kuwapo kwa upinzani ni umaarufu wake toka kwa wananchi wengi wa nchi hiyo na hasa familia zenye kipato kidogo mijini na kwenye maeneo ya vijijini.

Wengi wao wanaona wamefaidika kutokana na sera nzuri za serikali kwenye mambo ya kijamii.Ana upinzani mkubwa unaotoka kwa watu wa kipato cha kati mijini na matajiri.

PIGO
Rais Cristina Fernandez alipata pigo baada ya kufiwa na mumewe kipenzi na rais wa zamani wa nchi hiyo Nestor Kirchner aliyefariki mwaka 2010.

AFANYIWA UPASUAJI
Oktoba 2013 alifanyiwa upasuaji katika hospital moja jijini Buenos Aires ambayo iliisha vizuri na kwa hivi sasa bado anaendelea na majukumu yake.

ELLEN JOHNSON SIRLEAF
Rais Ellen Johnson Sirleaf alizaliwa Liberia mwaka 1938. Sehemu kubwa ya masomo yake ameyasomea nchini Marekani kabla ya kurudi kuitumikia nchi yake.

Mwaka 1980 kulifanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na Sajenti Samuel Doe aliyemuua Rais William Tolbert wa nchi hiyo na hivyo kumfanya akimbilie nje ya nchi.

Alirudi mwaka 1985 kwa ajili ya kuendesha upinzani dhidi ya serikali ya kijeshi.

MAISHA YAKE YA UTOTONI
Alizaliwa Oktoba 29, 1938 katika jiji la Monrovia. Ni mhitimu toka Chuo Kikuu cha West Africa kilichoko katika jiji la Monrovia na baadaye akaendelea na masomo ya uhasibu toka Chuo cha Biashara cha Madison kilichoko Winsconsin, Marekani.
Badaye alisoma shahada ya uchumi toka chuo kikuu cha Colorado na shahada ya uzamili kwenye utawala wa umma toka chuo kikuu cha Harvard, vyote vya Marekani.

AINGIA KWENYE SIASA
Aliporejea Liberia, Rais Sirleaf aliteuliwa kuwa naibu waziri wa fedha kwenye serikali ya Rais William Tolbert.

Baada ya Rais Tolbert kupinduliwa na kuuawa na Sajenti Samuel Doe aliyetoka katika kabila la Krahn, Sirleaf alikimbilia Nairobi nchini Kenya na kisha Marekani alikoenda kufanya kazi kama afisa kwenye jumuya ya mabenki ya kimataifa.

Mwaka 1985 alirejea Liberia na akagombea kiti cha seneti.

Alifungwa miaka 10 jela baada ya ‘kuuponda’ utawala wa kijeshi la sajenti Doe, ambapo hata hivyo alitumikia kifungo hicho kwa muda mfupi kabla ya kuachiwa na kukimbilia kwenye jiji la Washington, D.C.

Alirejea nchini mwake tena mwaka 1997 safari hii akifanya kazi kama mchumi kwenye Benki ya Dunia na Citibank Africa.

AWA RAIS WA LIBERIA
Baada ya kumuunga mkono Charles Taylor alipoendesha kampeni dhidi ya rais Samuel Doe na kisha kumung’oa madarakani, aligombea urais mwaka 1997 akishindana na Taylor ambapo alishindwa.

Taylor akiwa rais wa Liberia aliamua kummaliza Sirleaf kwa kumfungulia mashtaka ya uhaini.

Baada ya jumuiya ya kimatiafa kumshinikiza Taylor kuondoka madarakani Mwaka 2005, Sirleaf alichaguliwa kukiongoza chama cha Unity Party. Aligombea urais wa nchi hiyo akishindana na mchezaji mpira mashuhuri mzaliwa wa nchi hiyo George Weah.

Katika kampeni zake aliahidi kuleta maendeleo ya kiuchumi na kumaliza rushwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Alipoapishwa mwaka 2006 kwa rais wa Liberia, Sirleaf akawa mwanamke wa kwanza mweusi ulimwenguni na mwanamke wa kwanza Afrika kuchaguliwa kuwa mkuu wa nchi.

Miaka mitano baadaye alipewa tuzo ya amani ya Nobel pamoja na Leymah Gbowee na Tawakkol Karman kutokana na msimamo wao wa kutumia njia za amani kushughulikia usalama na haki za wanawake za kushiriki kwa ukamilifu katika kazi za kujenga amani.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa