WAZIRI
Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amesema tofauti ya kipato ambayo
imeanza kujitokeza nchini baina ya matajiri wachache na wenye madaraka
kwa upande mmoja na maskini walio wengi kwa upande wa pili si dalili
nzuri na ameshauri kudhibitiwa mapema kabla haijaleta madhara makubwa
nchini.
Sumaye alitoa kauli
hiyo mjini Arusha jana katika Mkutano Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati
ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) uliofanyika katika
Sekondari ya PeacHouse.
“Hali hii ni ya hatari
sana kwa amani na utulivu wa taifa lolote kwa sababu walio wengi
hawatavumilia kuona watu wachache wakiishi katika anasa za kutisha,
wakati walio wengi hawamudu hata mahitaji ya lazima kwa maisha kama vile
chakula, matibabu, maji nakadhalika,” alisema Sumaye na kuongeza;
“Tofauti hii imeleta
vurugu katika nchi nyingi na kuathiri amani na utulivu, hapa kwetu hali
hii ipo na dalili isiyo nzuri hivyo inahitajika kudhibitiwa kwa haraka
kabla haijaleta madhara makubwa kwa taifa letu.”
Alisema maskini kwa
walio wengi kwa upande wa pili husababishwa na mfumo mbaya wa uchumi na
ubinafsi uliokithiri usiojali binadamu wengine.
Alifafanua kwamba umoja
ni muhimu kwa amani na utulivu wetu, na pale ambapo umoja haupo hata
maendeleo huwa duni sana. Alisisitiza kwamba bila umoja hakuna moyo wa
uzalendo wa mtu kuipenda nchi yake na watu wake.
“Moyo wa uzalendo
humfanya mtu kuipenda na kuitumikia nchi na watu wake kwa upendo wa
dhati na kuweka masilahi ya taifa na umma mbele badala ya masilahi yake
binafsi,” alisema Sumaye.
Aliongeza kwamba sababu mojawapo ya kukosa maendeleo katika bara la Afrika ni kukosekana kwa umoja.
Alisema kwa sasa
viongozi wa kiroho wana kazi kubwa kuliko huko kipindi cha nyuma. “Leo
nchi yetu ina matatizo makubwa ya maadili kuanzia vijana hadi wakubwa.
Matatizo mengi tunayoyazungumza na yanayowakabili jamii kwa sehemu kubwa
ni kutokana na upungufu wa maadili. Je katika upungufu huu wa maadili
ya jamii viongozi wa kiroho mna nafasi ipi ya kudhibiti mambo haya?”
Alihoji Sumaye.
Sumaye aliongeza kuwa ni jukumu la viongozi wa ngazi na aina zote kushirikiana katika kuelimisha jamii kuondokana na maovu haya.
Alisema viongozi wote
kila mmoja kwa eneo lake na wote kwa pamoja lazima wapige vita maovu
mbalimbali ndani ya jamii yetu ya Watanzania. Umoja wetu katika jambo
hili ndiyo nguzo kuu ya mafanikio yetu. “Tujenge maadili mema katika
jamii ili upendo wa watu kujali binadamu wenzao udumu na heshima kwa
binadamu iwepo. Tukiwa wamoja tutashinda ili Tanzania iwe nchi ya raha,”
alisema Sumaye.
Akizungumzia umoja,
Sumaye alisema ni nguzo muhimu sana kwa nchi. Alisema nchi yenye umoja
baina ya watu wake huwa katika hali ya utulivu zaidi kuliko zile ambazo
zina migawanyiko ndani yao.
Alisema mifano ni mingi
ya nchi ambazo zimeingia katika hali ya uvunjivu wa amani hata kupigana
wenyewe kwa wenyewe kwa sababu hakuna umoja baina ya watu wake na kila
upande ukipigania kuudhulumu upande mwingine au kunakuwa na chuki
zimejengeka baina ya pande zinazohusika.
“Chuki hizi zinaweza
kusababishwa na sababu za kisiasa, ukabila, udini, uchumi na sababu
nyinginezo nyingi,” alisema na kuongeza; “Katika siasa tofauti hizi
huweza kutokea pale ambapo upande mmoja huhisi kuwa unadhulumiwa au
unaonewa katika maamuzi ya kisiasa hasa nyakati za kampeni, upigaji kura
na wizi wa kura,” alisema na kuongeza;
“Wakati mwingine hali
hii hutokea kwa upande moja kukataa tu kushindwa hata kama wameshindwa
kwa halali. Jambo hili la kisiasa limeleta fujo nyingi hasa katika nchi
nyingi za Kiafrika na kusababisha umwagaji wa damu.”
Alisema kwa bahati
nzuri bado haijakumbwa na kadhia hiyo lakini ni eneo la kulitupia jicho
sana lisije likaathiri amani na utulivu. “Ni lazima shughuli zetu za
siasa zifuate sheria na taratibu zilizowekwa kwa uwazi bila kutiliwa
shaka na upande wowote,” alisema na kuongeza;
“Haki ni lazima
isimamiwe kikamilifu nyakati zote za kapeni hadi upigaji wa kura,
kuhesabu kura na hata kutangaza matokeo.” Alitaja eneo lingine la hatari
sana ni chuki za kidini au zinazotokana na imani za watu. Alisema vita
vyote havina macho, lakini vita vya kidini ni vibaya zaidi na huishia
kuuana bila kuwa na mshindi.
“Nchi yetu hatujawa na
tatizo kubwa na jambo hili lakini hatuko salama sana. Kumekuwa kukitokea
chokochoko za hapa na pale zenye sura ya imani. Hapo upendo na uzalendo
vimepungua na kuathiri umoja wetu,” alisema na kusisitiza kwamba;
“Tukiwa wamoja hili
halina nafasi kwa sababu hakuna dini inayofundisha chuki kwa binadamu
mwenzako. Ni lazima tukubali kuwa nchini mwetu kila mtu ana uhuru wa
kuabudu dini aitakayo ili mradi havunji sheria za nchi.
“Viongozi wetu wa dini
mbalimbali ni bora wakasimamia vyema waumini wao ili nchi yetu isije
ikakumbwa na balaa la vurugu za kidini jambo ambalo ni la hatari sana
kwa amani na usalama wa nchi na watu wote. Ni vyema tudumishe upendo ili
umoja wetu uendelee kudumu.”
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment