Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa Chadema, Freman Mbowe akisoma fomu ya kugombea uenyekiti
wa chama hicho baada ya kukabidhiwa na mwakilishi wa wazee wa Mkoa wa
Kigoma, Athumani Mzigo
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe jana alikabidhiwa fomu na makada wa chama hicho na kumtaka
awanie tena kiti hicho, ombi ambalo alilikubali na kufungua milango kwa
wanachama wengine ‘kupimana naye kifua’.
“Nafasi bado ipo, anayetaka kupima kifua na mimi
ajitokeze. Tena nawaomba viongozi wangu msizuie fomu kwa anayetaka,”
alisema Mbowe ambaye ameongoza chama hicho kwa vipindi viwili vya miaka
mitano mitano.
Makada wa chama hicho kutoka maeneo mbalimbali
nchini wakiongozwa na kada maarufu, Athuman Mzigo (Mapigo Saba) kutoka
Kigoma, walikutana na Mbowe na kuwasilisha maombi yao ya kumtaka awanie
tena nafasi hiyo.
“Kutokana na sifa za mwenyekiti wetu,
tumechangishana Sh200 kila mmoja hadi zikafika Sh50,000,” alisema Mapigo
Saba huku akishangiliwa na makada wenzake alioambatana nao na kuongeza:
“Tumemwomba mwenyekiti agombee nafasi hiyo kwa
kuzingatia sifa; kwanza anaijua vizuri idadi ya Watanzania na matatizo
yao, pili anaungwa mkono na watu wengi na amekisaidia chama kukua.
Tulikuwa na madiwani 40 leo wamefika 500, wabunge watano leo 48. Halafu
hana ubaguzi ndiyo maana ameunganisha vyama vya upinzani na kuunda Ukawa
(Umoja wa Katiba ya Wananchi).”
Huku akichomekea maneno ya lugha ya Kiha, Mapigo
Saba alisema kuwa maombi ya kumtaka Mbowe agombee pia yametolewa katika
mikoa ya Rukwa, Manyara, Iringa, Njombe, Jimbo la Same Magharibi,
Zanzibar, Mwanza na Kilimanjaro.
Hotuba ya Mapigo Saba ilifuatiwa na salamu kutoka
kwa wazee wa wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke, Baraza la Wanawake
(Bawacha) na Baraza la Vijana (Bavicha).
Akitoa salamu za Bavicha, mwenyekiti wa baraza
hilo Njombe, Emmanuel Masonga alisema Mbowe ni sawa na Joshua
aliyemalizia kuwaongoza wana wa Israel kuingia nchi ya Kanaani:
“Sisi Wakristo tunajua kuwa Mussa alianzisha
safari ya Waisrael kwenda Kanaani, ila hakuwafikisha. Kina Mtei (Edwin),
Kimesera (Victor), Bob Makani na wengineo walianzisha safari ya kwenda
Ikulu, ila hawakutufikisha. Mbowe ni sawa na Joshua atakayetufikisha
Ikulu,” alisema Masonga.
Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Susan Lymo alimsifu Mbowe akisema ameongeza hamasa ya wanawake kushiriki siasa katika chama hicho.
“Mwaka 2000, kulikuwa na mwanamke mmoja katika
viti maalumu, mwaka 2005 waliongezeka na kufikia sita na mwaka 2010
wamefikia 26. Mwenyekiti pia ameufanya mwaka huu kuwa wa wanawake
kitaifa na ameongeza hamasa ya wanawake kushiriki siasa,” alisema Lymo.
Mbali na viongozi wa chama, alikuwapo pia Sheikh
Rajab Katimba kutoka Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ambaye alimsifu
Mbowe na kuomba agombee tena nafasi hiyo
Mbowe akubali
Baada ya Mratibu wa Vuguvugu la Mabadiliko (M4C),
Nickson Tugara kummwagia sifa Mbowe, Mapigo Saba alimkabidhi fomu, huku
makada wakiimba, ‘Jembe, jembe, jembe…”
Mbowe aliishukuru Kamati Kuu ya chama hicho kwa
kupanga uchaguzi Septemba 14, mwaka huu ambayo ni siku yake ya kuzaliwa
huku akiahidi kujenga chama imara.
“Mtaiona Chadema mpya ifikapo Septemba 14. Hiki
chama hakitakufa na hatutamvumilia mtu yeyote wa kabila lolote
atakayekivuruga,” alisema.
Mbowe alisema hajawahi kuomba kugombea uenyekiti
wa chama hicho tangu aliponza mwaka 2000... “Napata wakati mgumu
ninapofikia wakati huu.
Chadema ina watu mbalimbali wenye taaluma na
uzoefu, kwa nini mimi? Makundi haya yaliyojitokeza kunichukulia fomu
yanaweza kutafsiriwa na wapenda majungu kuwa nimepanga mimi.
“Leo ni mara ya tatu naombwa kugombea uenyekiti,
sijawahi kuomba. Mwaka 2004, Mzee Makani aliniomba nikamkatalia, lakini
akaunda kikundi cha wazee walionichukulia fomu.
Mwaka 2005, chama hakikuwa na mgombea urais, awali
alijitokeza Profesa Mwesiga Baregu lakini akajitoa, nikaambiwa nibebe
mzigo. Mwaka 2009 nikaombwa tena kugombea.”
Alisema amedhamiria kujenga chama kimtandao na
kimfumo ili kuondokana na mfumo wa kienyeji... “Huko nyuma wakati wa
uchaguzi watu walipeana tu nyadhifa kiundugu tukadhani chama
kimeongezeka. Lakini wakati huu uchaguzi umefanyika kwa miezi tisa.
Tulisema hatuwezi kufanya uchaguzi wa Taifa bila kupata viongozi wa mkoa, wilaya, kata, kijiji na mtaa, kitongoji na shina.
Tumefanya uchaguzi, watu wamepima na kuona mambo
magumu, mara unasikia wanakimbia wakisema wameacha uenyekiti, uache
wakati chama kinakua?”
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment