Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Jakaya Kikwete, akimkabidhi hundi ya
shilingi milioni 5, mfanyakazi bora wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Herman
Kachima, wakati wa kilele cha siku ya Wafanyakazi Duniani ambapo kitaifa
zilifanyika kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana.(Picha na
Khalfan Said)
Kadhalika, Rais Kikwete ametangaza nyongeza ya kima cha chini cha mishahara ambacho kitatangazwa wakati wa Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza Jumanne ijayo na waziri mwenye dhamana.
Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo jana wakati akihutubia maelfu ya wafanyakazi walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Alisema kilio cha kodi ni cha muda mrefu kwa wafanyakazi, lakini serikali imejitahidi kupunguza mwaka hadi mwaka, ili kuwafanya wafanyakazi wafurahie mishahara wanayopata kwa kuishi maisha mazuri.
Alisema mwaka 2007 P.A.Y.E ilikuwa asilimia 18, lakini serikali imejitahidi kuishusha hadi asilimia 13 ya sasa na kwamba itaendelea kuishusha hadi kuwa chini ya asilimia 10.
Alisema mwaka 2013/14 kima cha chini cha mshahara kiliongezwa kutoka 170,000 hadi 240,000 huku Shirikisho la Vyama Huru vya wafanyakazi Tanzania (Tucta) likieleza kwamba kiasi cha Sh 315,000 ndicho kinachomfaa mfanyakazi.
Alisema wakati kima cha chini kikiwa Shilingi 315,000, Tucta inapendekeza kuwa Shilingi 750,000 kwa mwezi itakayomsaidi mfanyakazi kukabiliana na machungu ya maisha.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema serikali inatumia asilimia 44.9 ya Bajeti na asilimia 10 ya Pato la Taifa kulipa mishahara ya watumishi wa umma na kwamba itaendelea kuongeza kwa kadri uwezo utakavyoruhusu.
ASIKITISHWA SEKTA BINAFSI
Rais Kikwete alisema anasikitishwa na waajiri wa sekta binafsi ambao kwa makusudi wameshindwa kulipa wafanyakazi wao kima cha chini ya mshahara na kuendelea kulipa Sh 100,000 kwa mwezi.
MFUMUKO WA BEI
Rais Kikwete alisema ukuaji wa uchumi mwaka ni asilimia 6.5 na kushuka kwa mfumuko wa bei kwa asilimia tisa kutoka asilimia 19.5 mwaka 2013 na kwamba moja ya mambo yanayoongeza makali ya maisha na watumishi kutoona thamani ya mishahara yao ni mfumuko wa bei.
Alisema serikali inaushughulikia kuhakikisha unafikia chini ya asilimia 10 na hata kufikia asilimia tano ili kupunguza ugumu wa maisha kwa Watanzania.
Hata hivyo, Rais alisema serikali iliruhusu kuingizwa kwa sukari na mchele kutoka nje ya nchi kwa kuwa ndizo bidhaa zinazopaisha mfumuko wa bei.
MAWAKALA WA AJIRA
Rais Kikwete alimtaka Waziri wa Kazi naAjira, Gaudensia Kabaka, kuendelea kuchukua hatua dhidi ya mawakala binafsi wa ajira ambao wanawanyanyasa na kuwadhulumu wafanyakazi wanaoajiriwa kwenye kampuni walikowatafutia kazi.
“Mawakala hawa wanakodisha wafanyakazi kwa waajiri, wanachukua na kuwakata mishahara yao, huu ni udhalimu na unyanyasaji mkubwa, nampongeza waziri kwa kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi yao bila kuwaonea aibu,” alisisitiza.
MABARAZA YA WAFANYAKAZI
Rais Kikwete alisema anasikitishwa na taasisi za serikali zinazovunja sheria kwa kutounda Mabaraza ya wafanyakazi na mahali hapo hawafanyi vikao vinavyotakiwa kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha.
“Vikao vya menejimenti vyenye posho fedha zake zinapatikana, lakini kuitisha Mabaraza ya wafanyakazi hawataki…namwagiza Waziri kufuatilia utekelezaji wa sheria ya kuwapo kwa Mabaraza hayo, siyo jambo la hiari bali ni matakwa ya sheria, lazima watekeleze agizo la Rais la mwaka 1970,” aliagiza.
Aidha, alisema anasikitishwa na waajiri wa sekta binafsi ambao wanapinga kuwepo kwa matawi ya wafanyakazi katika maeneo ya kazi na kuwachukulia hatua na kuwasuka suka ikiwamo kufukuzwa kazi, kusimamishwa na kutafutiwa visa mbalimbali wale wanaokuwa mstari wa mbele kutaka kuanzishwa kwa matawi hayo.
Alisema waajiri hao wamejiwekea mfumo mbadala wa kushughulikia matatizo ya wafanyakazi na kuukataa mfumo wa kisheria.
“Narudia tena hili siyo jambo la hiari ya mtu, Taasisi au Kampuni yake, kuanzisha tawi la wafanyakazi sehemu ya kazi ni lazima, hakuna aliye juu ya sheria, ninaagiza litekelezwe haraka iwezekanavyo,” alisisitiza.
Alisema palipo na matawi ya wafanyakazi kumewezesha kuwepo kwa mazingira shirikishi kwenye maamuzi na utendaji kazi kuboreka.
“Naagiza Waziri kutuma wakaguzi kwenye maeneo yote ya kazi kukagua utekelezaji wa sheria, wanaokwenda kinyume wachukuliwe hatua…naambiwa wapo wakaguzi wanaokula rushwa za waajiri ili matawi yasiwepo…nakutaka Waziri kuchukue hatua madhubutu kukomesha,” alisema.
UCHUMI
Alisema uchumi wa Tanzania utabadilika hivi karibuni kutokana uchumi wa chini hadi wa kati kutokana na kugundulika kwa nishati ya gesi na kwamba serikali itakuwa na fedha nyingi za kutatua kero za wananchi wakiwamo wafanyakazi.
MFUKO WA FAMILIA
Rais Kikwete alisema mfuko wa familia utakaowasaidia wafanyakazi walioumia kazini utaanza kufanya kazi mwezi Juni, mwaka huu, ikiwa na mchango wa serikali na sekta binafsi.
Alisema kila mwezi serikali itachangia asilimia moja ya mishahara ya wafanyakazi na waajiri binafsi watatakiwa kuchangia asilimia 0.5.
MADAI YA WALIMU
Alisema serikali inaendelea kuyafanyia kazi madai ya walimu na kwamba uhakiki uliofanyika mwaka jana ulionyesha ni Shilingi bilioni 19 na baada ya kufuatilia kwa undani walibaini Shilingi bilioni tatu haikuwa ni madeni, bali iliongezwa kwa maslahi ya watu.
Alisema serikali inafuatilia walioongeza na hatua madhubuti zitachukuliwa na kwamba ulipaji wa madeni ya walimu unaendelea.
Aidha, Rais Kikwete alisema waraka wa muundo mpya wa utumishi wa walimu unatarajiwa kutoka Juni mwaka huu.
Hata hivyo, alisema hadi sasa Halmashauri 96 zimemaliza uhakiki wa madeni ya walimu na ulipaji unaendelea na kwamba halmashauri 51 bado na utafanyika.
Mgaya: KIMA CHA CHINI 750,00/-
Awali, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya, aliitaka serikali kuhakikisha kima cha chini cha mshahara kinafikia Shilingi 750,000 kwa mwezi kwa sababu ya kushuka kwa thamani ya Shilingi pamoja na mfumuko wa bei.
Aidha, Mgaya alimuomba Rais Kikwete kutimiza ahadi yake ya kuanzisha Tume ya kuboresha maslahi na mishahara ya watumishi wa umma aliyoitoa mwaka 2006 na kwamba ingetekelezeka kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2015.
Alisema ni vyema serikali ikapunguza kodi ya mapato kwa wafanyakazi kufikia digiti moja kwa kuwa mzigo wa kodi umeendelea kuwa mkubwa kwa wafanyakazi wa kada zote na kwamba ni wakati mwafaka kwa serikali kudhamiria kuondoa kero hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Hata hivyo, Mgaya aliiomba serikali kuharakisha kanuni za kukokotoa madai ili zifanane kwa mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ikiwa ni pamoja na mwaanachama kuruhusiwa kuhama kutoka mfuko mmoja kwenda mwingine.
Mgaya aliiomba serikali kutekeleza ahadi yake ya kulipa deni kubwa la Mfuko wa PSPF na madeni mengine yanayotokana na mikopo kutoka katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Kadhalika,, alitaka serikali kupunguza idadi ya mifuko hiyo hali ambayo itasaidia kupunguza gharama kubwa za uendeshaji wa mifuko hiyo na badala yake zihamie katika kuboresha mafao ya wastaafu.
ARUSHA WATAKA KODI ISHUKE
Wafanyakazi wa Jiji la Arusha wameiomba serikali kushusha kiwango cha kodi ya mshahara na kufikia asilimia tisa, ikiwemo uimarishwaji wa ulinzi na usalama, ili kuwezesha wananchi kuishi kwa amani.
Nao wafanyakazi wa Kiwanda cha A toZ kilichopo jijini hapa,walitia fora kwa maandamano yao yaliyokuwa yalikuwa na mabango yanayohamasisha ushirikiano makazini na bidhaa mbalimbali wanazozalisha kiwandani hapo.
Kilio hicho cha Wafanyakazi kilitolewa jana na Mary William, wakati akisoma risala ya wafanyakazi na kusema kuwa ni vyema kodi hiyo ikapunguzwa, ili kuwezesha wafanyakazi kutimiza malengo yao ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi.
Pia walitoa rai kwa Wabunge wa Bunge la Katiba na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha wanazungumza mambo yenye maslahi kwa wafanyakazi na maisha ya Watanzania, badala ya kuzungumzia maslahi yao pekee.
“Tunaomba maslahi ya wafanyakazi yaboreshwe pia hawa wabunge wajadili mambo ya maana badala ya kujadili maslahi yao binafsi, lakini pia tunaomba amani iwepo katika Jiji hili, kwani mabomu yanaathiri mambo mbalimbali ikiwamo sekta ya afya, elimu,utalii na mambo mengine,” alisema.Naye Mwenyekiti wa Tucta jijini Arusha, ,Bertha John, alisisitiza kuwa ni vyema serikali ikaangalia zaidi maslahi bora ya wafanyakazi, ikiwamo huduma muhimu pamoja na mikopo ili kuwezesha wafanyakazi kukabiliana na umaskini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema,serikali inaendelea kushughulikia kilio cha wafanyakazi juu ya mishahara na mazungumzo, bado yanaendelea na kutoa rai kwa wakazi wa Jiji hilo kuhakikisha wanawafichua wenye nia ovu ya kuhatarisha usalama wa wenzao, kwa kutengeneza mabomu ya kienyeji yanayoumiza watu mbalimbali.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa watu hao ili wajulikane wanania gani ovu ya kuhatarisha usalama wa wananchi pamoja na wawekezaji, ikiwemo sekta ya utalii, hivyo ni vyema wananchi wakawafichua wahusika.
MARA WAHIMIZWA KUJITUMA
Wafanyakazi mkoani Mara wamehimizwa kufanya kazi kwa bidii, kwa kujituma, kuweka uzalendo mbele, kuepuka rushwa, kuwa na maadili mema na kuwa na Mshikamano ili kuweza kujiletea maendeleo.
Hayo yamesemwa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Henjewele, katika sherehe za Mei Mosi zilizofanyika katika Uwanja wa Sabasaba wilayani Tarime.
Sherehe hizo ziliambatana na Maandamano katika Mji wa Tarime mjini na baadhi ya Washiriki katika Sherehe hizo walikuwa kutoka vyama kadhaa vya wafanyakazi.
Watumishi bora walizawadiwa zawadi mbalimbali vikiwamo vyeti vya utumishi bora kazini, hundi na fedha taslimu Sh. 500,000,00,
Henjewele alisema kuwa Watanzania wapo kwenye soko la ushindani la ajira na kwamba wafanyakazi wanpaswa kujituma badala ya kufanya kazi kwa mazoea na kwa ujanja ujanja.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment