Home » » KAMATI:NYUMBA ZILIZO JENGWA KWENYE FUKWE ZIBOMOLEWE

KAMATI:NYUMBA ZILIZO JENGWA KWENYE FUKWE ZIBOMOLEWE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Al-Shymaa Kwegyr
 
Pamoja na serikali kuagizwa na Bunge kubomoa nyumba zilizojengwa  kinyume cha sheria zikiwemo za ufukweni, majengo hayo yaliendelea kuota kama uyoga.
Miongoni mwa majengo yaliyojengwa ufukweni yalitajwa kuwa ni la Mbunge wa Viti Maalum (CCM-Morogoro) Mchungaji Dk.Getrude Rwakatare na mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Mzamiri Katunzi.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira 2013/2014 pamoja na makadirio ya matumizi ya ofisi hiyo kwa 2014/15, Mjumbe wa kamati hiyo, Al-Shymaa Kwegyr (pichani), alisema kushindwa utekelezaji huo ndiko kunasababisha sheria za mipango miji kuvunjwa.

“Kamati inataka serikali kubomoa nyumba zote zilizojengwa kinyume cha sheria katika kingo za mito na fukwe za bahari ili kurudisha mito iliyoathirika katika hali yake ya asili na kuondoa athari kubwa ya kimazingira zinazoweza kutokea,” alisema.

 Aidha, alisema kamati inataka kujua maendeleo ya zoezi la uchunguzi wa hati za nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria.

Alisema kumekuwa na ujenzi holela usiofuata sheria katika fukwe na kingo za mito na kwamba hali hiyo inasababishwa na wananchi kwa kutokuwa na uelewa kuhusu sheria ya mazingira au kuikaidi sheria hiyo au rushwa.

Kwegyr alisema ujenzi huo hasa katika kingo za mito unaathiri mazingira ya asili ya mito ikiwa ni pamoja na kupindisha mikondo ya mito.

“Hali hii ni ya hatari kwani imekuwa ikisababisha mafuriko kwa pande ambazo mito imeelekezwa na hivyo kuharibu mazingira.

Alipendekeza wale wote waliopewa vibali kinyume cha sheria wawajibishwe ikiwa ni pamoja na waliowapa.

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani (Mazingira), Mchungaji Israel Natse Israel, alisema vigogo waliojenga katika fukwe na tangu ujenzi unaanza hadi unamalizika hawakuchukuliwa hatua zozote.

Alitaka kujua pia uhalali wa Kampuni inayojenga barabara ya mabasi yaendayo kasi ya Strabag  kupewa kibali cha kujenga Jangwani.

Alidai ujenzi huo umechangia wananchi wasio na hatia wa Jangwani kupata matatizo ya mafuriko ambayo awali hayakuwapo kutokana na ujenzi wa ofisi hizo kuzuia njia ya maji.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa