Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ujumbe wa Bodi ya Utendaji ya Shirika la Kimataifa la Mfuko wa
Maendeleo ya Kilimo (Ifad), upo nchini kwa ziara ya siku tano kuanzia
jana, kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo.
Ujumbe huo wa watu wanane kutoka mataifa ya
Uswisi, Finland, Uholanzi, Nigeria, Mexico, Indonesia, China, na Angola
pia utafanya mazungumzo na viongozi mbalimbali nchini wakiwamo Rais
Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Taarifa ya Ifad kwa vyombo vya habari iliyotolewa
jana, ilisema wajumbe hao watafanya tathmini kuhusu ufanisi wa miradi
inayodhaminiwa na Ifad kujua imechochea kwa kiasi gani maendeleo ya
kilimo nchini. “Ujumbe wa bodi utatembelea miradi inayofadhiliwa na
Ifad, Tanzania Bara na Visiwani pia utajadiliana na wanavijiji kuhusu
changamoto wanazokabiliana nazo katika kilimo,” ilisema sehemu ya
taarifa hiyo.
Ifad imewekeza takriban Dola 212 milioni za
Marekani (Sh339.2 bilioni) katika miradi mitano inayoendelea ambayo kwa
ujumla wake inagharimu Dola 500 milioni za Marekani (Sh800 bilioni).
Miradi hiyo inatarajiwa kunufaisha kaya milioni tatu nchini.
Ujumbe huo pia utakutana na Sekretarieti ya
Maendeleo ya Kilimo Kusini Tanzania (Sagcot), Idara ya Rais ya Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN), sekta binafsi na washirika wengine wa
maendeleo kujadili namna ya kuboresha kilimo cha wakulima wadogowadogo
kuwa chenye tija.
Tanzania ni nchi ya pili Mashariki na Kusini mwa
Afrika inayopokea msaada mingi ya Ifad katika miradi ya kilimo baada ya
Ethiopia.
Ifad imegharimia jumla ya miradi 15 tangu mwaka
1978 yenye thamani ya Dola 769 milioni za Marekani (Sh1.23 trilioni) na
kati ya fedha hizo, Dola 360 milioni (Sh576 bilioni) zilitoka moja kwa
moja katika mfuko huo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment