Na Jacquiline Mrisho - Maelezo
Wizara
ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari juu
ya ugonjwa wa homa ya manjano ambao umethibitika kuwepo nchi ya jirani
ya Kenya.
Tahadhari
hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokua akiongea na
waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa
kipindupindu nchini ambapo katika wiki ya tarehe 14 Machi hadi 20 Machi
mwaka huu takwimu zinaonyesha kuwa kati ya Mikoa 13 yenye wagonjwa wa kipindupindu , jumla ya wagonjwa 738 na vifo 16 vimeripotiwa huku Mkoa wa Manyara ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kipindupindu.
Akielezea
kuhusu ugonjwa wa homa ya manjano,Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa
ugonjwa huu unasababishwa na virusi ambavyo huenezwa na mbu aina ya
Aedes na baadhi ya dalili zake ni homa, kuumwa kichwa,maumivu ya misuli
na mgongo,kupoteza hamu ya kula pia kutoka damu sehemu za mwili zilizo
wazi.
“Wizara
inapenda kutoa tahadhari ya ugonjwa wa homa ya manjano kwa wananchi
wote na hasa wanaokaa mipakani mwa nchi ya Kenya kwa kuwa ugonjwa huu
hauna tiba kamili ila una chanjo, mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili
zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na kupewa dawa za kushusha homa, maumivu,
kuongezewa maji mwilini kwa kunywa au kuwekewa dripu”alisema Waziri
Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kupambana na magonjwa ya kuambukiza kwa kuimarisha mfumo
wa ufuatiliaji wa wagonjwa na utaratibu wa utoaji taarifa za magonjwa
ya kuambukiza, kuhakikisha wasafiri wanaoingia na kutoka nchi zenye
hatari ya ugonjwa huo wanapewa chanjo kabla ya kuingia nchi nyingine,
kutoa elimu ya afya kwa wananchi, kuandaa timu za wataalam, vifaa tiba
na chanjo za kutosha ili kuweza kukabiliana na ugonjwa huo endapo
utajitokeza nchini kwa kusimamia na kuhimiza usafi wa mazingira na
kuzingatia kanuni za afya.
Pia,amewaonya
maofisa wanaotoa chanjo ya homa ya manjano walioko katika vituo vya
Afya vya kupokelea wageni wanaoingia na kutoka nchini kuacha mtindo wa
kupokea rushwa na kuwapitisha watu bila kupatiwa chanjo.
Mwisho, ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari na kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa afya walioko katika maeneo yao kwa kutoa taarifa haraka kwenye uongozi husika endapo kuna mgonjwa mwenye dalili za kipindupindu au homa ya manjano.
0 comments:
Post a Comment