Na Adili Mhina
Tume
ya Mipango imeanza zoezi la kuwajengea uwezo wataalamu katika kuandaa
na kutekeleza miradi ya maendeleo inayotumia fedha za serikali au kwa
kushirikiana na Sekta binafsi kwa lengo la kuongeza nidhamu na weledi
katika matumizi ya rasilimali za Umma.
Mafunzo
hayo yanayoendelea katika moja ya kumbi za ofisi ndogo za Bunge jijini
Dar es salaam na kuendeshwa na wataalamu elekezi kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam yanalenga kuanda wataalamu ambao watakwenda kutoa mafunzo
kwa maofisa wa Serikali walio
chini ya idara za Sera na Mipango na zile za uwekezaji katika Wizara,
Mikoa, Halmashauri, pamoja na mashirika na taasisi mbalimbali za umma
hapa nchini.
Akifungua mafunzo hayo mwanzoni mwa Juma, Kaimu Katibu Mtendani kutoka Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alieleza kuwa mafunzo
hayo yatasaidia kuimarisha utendaji, uwajibikaji na kuleta ufanisi
katika matumizi ya rasilimali za umma zinazoelekezwa katika miradi ya
maendeleo.
“Shabaha
kuu ya mafunzo haya ni kutoa maelekezo ya mchakato na hatua
zinazohitajika kufuatwa katika kutayarisha na kutekeleza miradi yote
inayotumia fedha za umma au kwa kushirikiana na sekta binafsi,” Alisema
Bibi Mwanri.
Kamu Katibu Mtendaji huyo alieleza kuwa kutokana na kukithiri kwa kasoro katika miradi ya maendeleo inayotumia fedha za umma, Serikali kupitia Tume ya Mipango ililazimika kuandaa Mwongozo
wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya
Umma (Public Investment Management Operational Manual) ambao utatumika
katika kuandaa, kutekeleza na kusimamia miradi yote inayotumia fedha za umma au kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Bibi
Mwari alieleza kuwa katika awamu hii ambayo Serikali imejikita katika
kujenga uchumi wa viwanda miradi mingi ya maendeleo inatarajiwa
kuanzishwa. Hivyo, bila kuwa na uelewa wa pamoja moingoni mwa wadau
wanaohusika katika kuandaa, kutekeleza na kusimamia miradi hiyo malengo
ya Mpango wa Pili wa Maendeleo hayatafikiwa kama inavyotarajiwa.
“Katika
kipindi hiki ambapo bajeti ya maendeleo imeongezeka na kufikia asilimia
arobaini ni wazi kuwa miradi mingi ya maendeleo inaanzishwa, hivyo ni
lazima kila mtaalamu aelewe kuwa tunawajibu wa kuandaa miradi bora,
yenye tija kwa wananchi na inayoendanda na thamani ya fedha
zinazotumika,” Alisisitiza Bibi Mwanri.
Bibi Mwanri aliwataka wajumbe wote kuhakikisha wanatumia mafunzo hayo vizuri ili kupata uelewa wa kutosha juu ya mwongozo huo.
Mafunzo hayo ya siku tano yamehudhuriwa na wajumbe
kutoka Wizara, Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Asasi za Kiraia
pamoja na Sekta binafsi na yanatarajiwa kuandaa wataalamu bora
watakaokwenda katika kanda mbalimbali nchini kutoa mafunzo tarajiwa kwa walengwa.
0 comments:
Post a Comment