Home » » Wakamatwa kwa kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji binadamu

Wakamatwa kwa kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji binadamu


Kaimu Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Tatu Burhan
Jumla ya watu 12, 864, wakiwemo Watanzania na raia wa nje, wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola kwa kosa la kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Tatu Burhan, alisema kukamatwa kwa watu hao kumetokana na kuimarishwa kwa mfumo wa usimamizi wa mipaka na udhibiti.

Alisema raia wa nje wanaofanyabiashara hiyo wanashirikiana na wenyeji, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi, hivyo ni vyema wakaacha tabia hiyo kwa kuweka uzalendo mbele.
Aidha, aliiomba serikali kuongeza vifaa vya kisasa kutokana na kuwepo kwa mbinu mpya na matumizi ya silaha na kuingizwa kwa silaha za kivita ambazo hutumika kuleta madhara kwa jamii.

Idara hiyo nchi nzima ina askari wasiozidi 3,000 huku mahitaji yakiwa ni 8,000, ambapo mpaka wa Tanzania ukiwa mkubwa unaopakana na nchi nyingi na kutumiwa kama njia ya kwenda nchi nyingine.

Alisema biashara hiyo imekithiri zaidi katika nchi za Ethiopia, Somalia na Bagladesh, ambao wengi huingia kwa lengo la kupita njia na wengine kuweka makazi kwa sababu mbalimbali zinazowasababisha kuzikimbia nchi zao.

Alisema nchi nzima kuna vituo 58, huku kukiwa na umbali wa zaidi ya kilomita 200 kutoka kituo kimoja hadi kingine na kutolea mfano kituo cha Tanga hadi Mtwara kikiwa na umbali wa kilomita 1,200 kwa ukanda wa bahari.

Aidha, alisema hadi kufikia Desemba 2012, idara imetoa pasipoti 537,426 kati ya hizo za kawaida ni 518,561, kidiplomasia 4,753, kiutumishi 1,499 na za Afrika Mashariki 1,2613.

Burhan alisema kwa mujibu wa takwimu hizo, Watanzania wengi wamewezeshwa kusafiri nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za biashara, ajira, masomo, matibabu na nyinginezo.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa