Serikali imewataka wanafunzi waliokosa mikopo kwa
ajili ya masomo vyuo vikuu kurudi nyumbani na ikiwezekana wakauze viwanja au
ng'ombe ili waweze kujisomesha kwani bajeti iliyopo haitoshi.Kauli hiyo
ilitolewa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philip Mulugo,wakati akizungumza na wanafunzi waliokosa mikopo ambapo
kwa takriban wiki nzima wamepiga kambi wizarani hapo.
"Kasungura kadogo na mkumbuke kuwa
mkopo ni kuomba kuna kupata na kukosa...hivyo wale waliokosa na walikuwa na
vigezo watafute watu wengine wenye uwezo wawasomeshe kwa mwaka mmoja na
unaofuata watume tena maombi," alisema.
Alisema kilio chao amekisikia na leo atazungumza na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusiana na malalamiko yao ambapo suala hilo
litapelekwa Bungeni ili kujadiliwa.
"Kama Bunge litaamua kupunguza
fedha kutoka kwenye bajeti zingine ili kusomesha wanafunzi hao. Bunge litaamua
kwani Serikali ina nia nzuri sana kwani hadi sasa imetoa trilioni 1.5, lakini
ndugu zenu hawarudishi," alisema.
Alitaja sababu nyingine ya wanafunzi kukosa mikopo
ni Serikali kuangalia uhitaji, kwani kuna masomo maalumu walilenga hasa fani
zenye upungufu wa wataalamu.
Alitaja fani hizo kuwa ni ualimu,
udaktari na wahandisi. Alitaja sababu nyingine za wanafunzi kukosa mikopo hiyo
ni waombaji kukosea majina na vitu vingine vidogo vidogo na walipotangaziwa
kwenye vyombo vya habari warudi kurekebisha fomu zao hawakufanya hivyo.
Alisema waliokosea kujaza fomu hizo
walikuwa 6,000 lakini waliorudi kufanya marekebisho walikuwa ni 3,000 na
wengine 2,000 walikuwa na vigezo lakini wamekosa kutokana na sungura kuwa mdogo
(bajeti).
Wanafunzi
waliokosa mikopo walisema kama wenzao wameweza kupata mikopo kwa asilimia 100
basi waangalie namna ya kugawana ili wote waweze kupata
Chanzo: Majira
0 comments:
Post a Comment