Na Mwandishi Wetu
MALKIA wa muziki wa Injili nchini Afrika Kusini, Rebecca Malope,
anatarajia kuwasili nchini Aprili 6 mwaka huu, ili kutumbuiza katika
tamasha la nyimbo za Injili la Pasaka litakalofanyika Aprili 8 mwaka huu
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu tamasha
hilo chini ya Kampuni ya Msama Promotions ya Dar es Salaam, Alex Msama,
alisema Rebecca anatarajia kuwasili na kundi la wanamuziki wake 13.
"Rebecca ameahidi atapiga 'live' akishambulia jukwaa kwa takriban saa 2
na ushei na atapiga nyimbo zake mpya tano na nyingine za zamani,"
alisema Msama.
Akizungumza kwa njia ya simu wiki hii kutoka Afrika Kusini, Rebecca
aliahidi kuwaletea Watanzania zawadi ya Pasaka, na akabainisha
ataambatana pia na waimbaji wengine kutoka Afrika Kusini.
Rebecca alisema amewaandalia zawadi nzuri mashabiki wa muziki wa Injili
wa Tanzania, na akatoa mwito wajitokeze kwa wingi siku ya tukio ili
kumshuhudia.
"Naahidi kuwaletea Watanzania zawadi ya Pasaka... nimewaandalia vitu vipya ambavyo naamini watavifurahia," alisema Rebecca.
Rebecca aliyezaliwa katika shamba la tumbaku Afrika Kusini, alisema
katika tamasha hilo la Pasaka mwaka huu ataimba nyimbo mbalimbali
zilizomo kwenye albamu zake, zikiwemo tano mpya.
Rebecca amewahi kutamba na albamu za Saturday Nite (aliyoitoa Januari 1,
2009), Hlala Nami (Novemba 11, 2003), Siyabonga (Desemba 21, 2000),
Free at Last (Novemba 18, 1997), African Classics (Mei 5, 2009) na
Greatest Hits (Januari 10, 2006).
Malope atakuwa mmoja kati waimbaji siku hiyo wakiwemo Rose Muhando,
Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro,
Christina Shusho, Atosha Kissava, Mwinjilisti Faraja Ntaboba, Ephraim
Sekeleti, Maryanne Tutuma, kundi la Glorious Celebration na kwaya ya
Kinondoni Revival.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe. Baada ya kutikisa Uwanja wa Taifa,
mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9
mwaka huu ambako mgeni rasmi atakuwa Naibu Spika, Job Ndugai.
Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili
ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane.
Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria tatu na
kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti
maalumu sh. 10,000.
0 comments:
Post a Comment