Home » » MAMA KIKWETE AWATAKA WANASACCOS KULIPA MADENI KWA WAKATI

MAMA KIKWETE AWATAKA WANASACCOS KULIPA MADENI KWA WAKATI



Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanachama wa Chama cha kuweka
Akiba na Kukopa cha URSINO na REGENT (URESCO) kuwa na utaratibu maalum
wa kukusanya madeni ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote
watakaochelewa kulipa madeni yao.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) aliyasema hayo jana wakati akifungua SACCOS hiyo iliyopo
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliendelea kusema kuwa ili SACCOS iweze kuendelea ni lazima ijiwekee utaratibu wa kutoa  mafunzo na semina mbalimbali za kuwajengea uwezo wanachama wake  katika uendeshaji na kusimamia miradi ya jamii.
“SACCOS
hii itakuwa imetoa mchango mkubwa kwa jamii ikiwa itaweza kuwasaidia
vijana na wakinamama kutumia mitaji waliyoipata kwa kuanzisha na
kuendelea miradi ya kuongeza kipato na hatimaye kipato hicho
kikawasaidia wazee wastaafu ambao pia wanahitaji msaada kutoka kwa
vijana na kina mama hao”, alisema Mama Kikwete.
Mama Kikwete pia  aliitaka SACCOS hiyo kujiwekea  dhamira
ya kupata maendeleo makubwa zaidi kwa kuendelea kuweka akiba na kuwa
makini katika kurudisha mikopo ili kuweza kuwavutia wanachama wengi
zaidi kujiunga kwani mafanikio yao yatatokana na kuwa na idadi kubwa ya
wanachama ambao wana akiba ya kutosha.
Akisoma
taarifa ya SACCOS hiyo Jonathan Kasesela ambaye ni Mwanachama alisema
kuwa Chama hicho chenye wanachama 242 wenye hisa zaidi ya shilingi
milioni 18 na amana zaidi ya shilingi milioni 128 ilianzishwa mwaka
2006.
“Malengo
tuliyonayo ni kuongeza idadi ya wanachama, kujenga ofisi ya kudumu,
kuwasaidia wazee wastaafu katika eneo la Ursino na Regent ambao ni
asilimia 80 ya wakazi wote wa eneo hili wapatao 1800, kusaidia vikundi
vya vijana  na wanawake katika juhudi za maendeleo”, alisema Kasesela.
Mwezi
Julai mwaka 2007 chama hicho kilianza kukopesha wanachama hadi kufikia
sasa wanachama waliopata mkopo ni 219 ambao wamekopa zaidi ya shilingi
milioni 136.
Taasisi ya WAMA iliichangia SACCOS hiyo shilingi milioni tatu fedha ambazo zitatumika kuongeza mtaji wa mfuko wa umoja huo.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa