Home » » Taarifa za kesi kutolewa kwa SMS

Taarifa za kesi kutolewa kwa SMS


Na Hellen Ngoromera
SERIKALI imetangaza kuboresha mfumo wa Mahakama kwa kuanzisha huduma mpya ya kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mienendo ya kesi zao kupitia simu za mkononi (SMZ).
Hatua hiyo ilitangazwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, wakati wa hafla ya kuapishwa kwa majaji 10 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni.
“Serikali imejipanga kuboresha mfumo wa Mahakama hasa katika usikilizwaji wa mashauri kwa kuboresha mfumo wa kurekodi mwenendo wa mashauri hayo.
“Katika uboreshwaji huo pia Mahakama inatarajia kutambulisha huduma mpya ya taarifa kwa njia ya simu, ambapo wananchi wenye mashauri mahakamani wataweza kupata fursa ya kutambua mienendo ya kesi zao kupitia simu za mkononi,” alisema Jaji Chande.
Alieleza kwamba mfumo huo wa simu za mkononi utaenda sambamba na mfumo wa kupata taarifa kwa mtandao wa internet ambapo nakala za mashauri yaliyotolewa hukumu zitawekwa.
Pamoja na mambo mengine alieleza kwamba kuapishwa majaji hao kutasaidia kuongeza kasi ya uendeshwaji wa mashauri mahakamani kwani sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya mrundikano wa kesi na kwamba kwa kuanzia majaji hao watapelekwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi kwa muda wa miezi mitatu ili kuleta ufanisi katika shughuli zilizopo huko kisha baadaye kupangiwa vituo vingine.
Alisema lengo la kufanya kazi katika mahakama hiyo ni kukabiliana na mlundikano wa mashauri kwani mpaka sasa mashauri 2,200 yanakadiriwa kuwapo katika mahakama hiyo huku wakati ina majaji wanne pekee.
Majaji walioapishwa ni Jaji Francis Mutungi ambaye alikuwa Msajili wa Mahakama Kuu, Jaji John Mugeta, Jaji Patricia Fikirini, Jaji Sam Rumanyika, Jaji Salvatory Bongola na Jaji Gerlad Ndika.
Wengine ni Jaji Mathew Mwaimu, Jaji Jacob Mwandengele, Jaji Latifa Mansoor na Jaji Joaquine De-Mello.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa