Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » MKURUGENZI MAKUMBUSHO YA TAIFA, ASIMAMISHWA KAZI

MKURUGENZI MAKUMBUSHO YA TAIFA, ASIMAMISHWA KAZI


Florence Majani


MKURUGENZI wa Makumbusho ya Taifa, Jackson Kihiyo amesimamishwa  kazi kwa muda usiojulikana  ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi huyo alisema  aliitwa na mkubwa wake wa kazi, ambaye ni Katibu Mkuu  Wizara ya Maliasili na kufahamishwa kuwa amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwani kuna tuhuma kuhusu utendaji wake katika ofisi hiyo.

“Baada ya kupewa taarifa hizo, juzi(jumanne) nilikabidhi ofisi na hivi sasa nipo nyumbani. Cha muhimu ni kuwa sijafukuzwa ila nimesimamishwa na ninaendelea kupata mshahara wangu kama kawaida haid pale watakapomaliza huo uchunguzi wao,” alisema Kihiyo


Kihiyo alisema, hakutaka kumhoji mkuu wake wa kazi kuhusu tuhuma zinazomkabili kwa sababu alitaka wawe huru na wafuatilie kwa kina bila kuingiliwa, hivyo hadi sasa hafahamu kilichomsimamisha kazi.

“Najua wakimaliza watanijulisha, sina mashaka yeyote kwa sababu najua hakuna kibaya nilichofanya, nikiwauliza uliza watadhani ninataka kuwaingilia katika uchunguzi wao. Waache wafanye uchunguzi kwa utaratibu na kwa uhuru wakimaliza watanieleza kilichopatikana,” alisema Mkurugenzi huyo. 

Chanzo cha habari kutoka katika ofisi hiyo kilichozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake kilibainisha kuwa mkurugenzi huyo amefukuzwa baada ya wafanyakazi kupeleka malalamiko kwa katibu mkuu, Maimuna Tarishi, ikiwemo utata katika ukusanyaji wa mapato na  maslahi ya wafanyakazi.

“Mkurugenzi alitoa amri ya kukusanya mapato katika vituo vyote na kisha mapato hayo katika akaunti ya makao makuu. Hili jambo lilizua maswali kwa sababu tutapelekaje mapato yote makao makuu, vituo vitajiendesha na nini? Lakini lingine ni maslahi duni ya wafanyakazi, hatujaboreshewa mishahara kwa muda mrefu,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa malalamiko mengine kuhusu  utendaji wa mkurugenzi huyo ni kitendo cha Ofisi kutumia Menejimeti ya Umma kumuadhibu mfanyakazi badala ya kutumia Kamati ya Nidhamu jambo alilodai linasababisha uonevu mkubwa kwa wafanyakazi.

Shutuma nyingine dhidi ya Kihiyo ni upandishwaji wa vyeo  kwa wafanyakazi usiozingatia sifa stahiki na kutokuwepo mipango endelevu ya mafunzo kwa wafanyakazi. 

Kabla ya Kihiyo kushika nafasi hiyo, Mkurugenzi wa Makumbusho alikuwa ni Nobert Kayombo, ambaye alifariki   Novemba 30, 2010.

Chanzo: Mwananchi


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa