na Nasra Abdallah
SHIRIKA la Usafiri wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), limeelezwa kuwa ndilo shirika linaloongoza kwa kutofikisha michango ya wafanyakazi wake katika Mfuko wa Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kama sheria ya kazi ya ajira inavyoelekeza.
Akizungumza na Tanzania Daima katika maonesho ya 36 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam, mwanasheria wa mfuko huo, Celestin Ntagara, alisema kitendo hicho kimelifanya shirika hilo kuwa na kesi ya kudaiwa kiasi cha sh bilioni sita hadi sasa.
Pia alisema kampuni inayofuatia kwa kudaiwa ni ile ya ulinzi inayojulikana kwa jina la Gema Security ambayo nayo inadaiwa takribani sh milioni 900.
Kutokana na hali hiyo alisema tayari baadhi ya kesi zimeshafikishwa mahakamani huku madai mengine yakiwa katika hatua za majadiliano.
Hata hivyo alieleza kwamba mfuko wao hauna lengo la kuwafikisha wateja wao mahakamani ila inatokea pale njia zote za majadiliano zinaposhindikana.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wanaoufanya ili wadau waone umuhimu wa kupeleka makato ya wafanyakazi wao kwenye mfuko huo, Ntagara alisema wamekuwa wakitoa elimu ya mara kwa mara kwa waajiri, waajiriwa na vyama vya wafanyakazi.
Katika wito wake aliwataka waajiri kujitahidi kupeleka michango ya wafanyakazi wao kwa wakati ili kuepuka kupelekwa mahakamni au kupigwa faini ya kutakiwa kulipa zaidi ya asilimia 15 ya kile alichotakiwa kuchangia.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, sheria inawaruhusu kwa wale watakaoshindwa kuchangia kutaifisha mali zao zitakazoweza kufidia kiasi wanachodaiwa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment