na Dianarose Matikila, Dar es Salaam
ZOEZI la ujazaji fomu kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya taifa linaloendelea jijini Dar es Salaam, limeanza kugubikwa na dosari nyingi ambazo ikiwa hazitarekebishwa ni dhahiri wananchi wengi watashindwa kujiandikisha.
Licha ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kujaribu kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi, wakihamasishwa kujitokeza kwa wingi kujaza fomu hizo kwa muda uliopangwa, uchunguzi wa Tanzania Daima katika vituo kadhaa vya uandikishaji umebaini zoezi hilo kuzorota.
Wananchi wengi waliozungumza na gazeti hili, walilalamikia zoezi hilo wakidai linawachukua muda mrefu bila sababu ambao wangeutumia kufanya shughuli zao nyingine.
Kasoro mojawapo iliyoonekana kwenye vituo vingi ni watu kuanza kujiandikisha badala ya kujaza fomu hizo, jambo ambalo limeleta usumbufu mkubwa kwa wale waliokwisha andikishwa mapema.
Pia kumekuwa na upungufu wa makarani wa uandikishaji, jambo linalosababisha kuwapo kwa misururu mirefu ya watu vituoni.
“Haiwezekani tusimame hapa kwenye jua kwa muda wa zaidi ya saa moja na nusu halafu foleni yenyewe haisogei, na hiyo yote inatokana na utaratibu mbovu wa kwenda kujaza fomu hizo, alilalamika mkazi mmoja wa Kata ya Wazo.
Aidha, baadhi ya wajumbe wa kata wameiomba NIDA iongeze idadi ya makarani vituoni kwa ajili ya kurahisisha na kuharakisha zoezi hilo la uandikishwaji na ujazwaji wa fomu hizo.
Chanzo: Tanzania Daima
1 comments:
NIDA wangeacha muda wazi na si kutisha wananchi kila siku kwamba mwisho siku fulani. Watu tuko kazini, ingekuwa rahisi zaidi kutupata kazini kuliko uvunje siku nzima, ukae kwenye foleni na huenda bado usijiandikishe. Katika tekinolojia ya leo kwa nini fomu zisiwe kwenye tovuti mtu anadounilodi, anajaza kisha anapeleka kwenye ofisi husika akiwa na viambatanisho husika. Kazi ya makarani itakuwa kuhakiki tu nyaraka na siyo kusimamia mtu akijaza fomu. Au kuna mkono wa kisiasa kwenye hili pia?
Post a Comment