Home » » ASKARI WAACHA LINDO, WAKAMATA BAJAJ

ASKARI WAACHA LINDO, WAKAMATA BAJAJ


na Shehe Semtawa
TABIA za askari polisi kuacha malindo na kufanya kazi zisizowahusu imeendelea kujitokeza jijini Dar es Salaam ambapo jana askari polisi wawili wanaolinda Benki ya Makabwela (NMB) walijikuta wakimkamata mwendesha Bajaj.
Askari polisi hao walijikuta wakiliacha lindo lao karibu na Idara ya Habari (Maelezo) jana saa 6:40 na kumkamata dereva wa Bajaj yenye namba za usajili T 513 kwa madai ya kukiuka sheria.
Akizungumza na Tanzania Daima dereva wa Bajaj hiyo, Issa Songa alishangazwa na kitendo cha kukamatwa na askari hao kwa sababu hakuwa na kosa.
Kwa mujibu wa Songa, askari hao walimvamia huku wakimtishia kwa bunduki walizokuwa wamebeba na kumtaka wasogee naye hadi ilipo benki hiyo.
Songa alikubali kufanya alivyotakiwa na askari polisi hao na walipofika walimlazimisha awape fedha kiasi cha sh 6,000 alizolipwa na abiria wake.
Alibainisha kwamba hiyo ni kawaida ya askari polisi hususan wanaokuwa kwenye lindo kujiingiza kwenye vitendo vya ukamataji wa vyombo vya usafiri wakati hawahusiki.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema atafuatilia madai hayo ili kujua ukweli wake kabla ya kuwachukulia hatu askari polisi hao.
“Nitawahusisha maofisa wanaosimamia utaratibu wa upangaji wa zamu za askari hao,” alisema Kamanda Kova alipotakiwa kueleza iwapo ni sahihi kwa askari hao kuwakamata madereva wa vyombo vya usafiri ama la.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa