Home » » CWT chatii amri ya Mahakama, chasitisha mgomo wa walimu

CWT chatii amri ya Mahakama, chasitisha mgomo wa walimu




Rais wa CWT, Gratian Mukoba
Waandishi Wetu
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimesitisha mgomo na kuwataka walimu kote nchini kurejea kazini kuanzia jana wakati kikijipanga kukata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na mahakama juzi.
Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi juzi ilitoa hukumu na kukitaka chama hicho kuwaagiza walimu kurejea kazini kuanzia jana kwa kuwa mgomo huo ulikuwa batili.


Hukumu hiyo imekuja siku moja tangu Rais Jakaya Kikwete aliposema kwamba Serikali haitawalipa walimu kiasi wanachoomba kwa sababu haina uwezo huo.
Jana, Rais wa CWT, Gratian Mukoba aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam kwamba bado kinaitafakari hukumu hiyo.


“Chama kinawasiliana na wakili ili kuona uwezekano wa kukata rufaa kwa kuwa baadhi ya vipengele vya hukumu hiyo vinahitaji ufafanuzi wa Mahakama ya Rufaa ili kuondoa utata wa kisheria,” alisema Mukoba.


Rais huyo amewasihi walimu kurejea kazini na kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Nawaomba mrudi kazini kama hukumu ya Mahakama inavyosema, tutakuwa tukiwafahamisha kila kitakachokuwa kinaendelea,” alisema Mukoba.


Rais huyo alisema: “Walimu wanarudi kazini wakiwa wamekata tamaa kabisa kwa sababu kila hatua wanayochukua mwajiri wao anakimbilia mahakamani.”


Alisema pamoja na walimu kuendelea kupuuzwa na mwajiri wao, chama hicho kitaendelea na majadiliano na Serikali kuhusu nyongeza za mishahara na posho.


“Chama kina imani kuwa hukumu hii imetoa somo kwa mwajiri ili atambue umuhimu wa kuzungumza na walimu,” alisema.
Alisema walimu wanarudi kazini bila ya kuwa na mawazo yaliyotulia na kwamba utendaji wao wa kazi utaathirika.


“Chama kinatoa wito kwa Serikali kukutana na CWT kwa haraka kuendeleza majadiliano ya madai ya walimu,” alishauri.


Akizungumzia fidia wanayotakiwa kuilipa Serikali kwa hasara waliyopata wanafunzi, Mukoba alisema chama kinasubiri taarifa rasmi ya Serikali kuhusu hasara hiyo.
“Mwenye uwezo wa kuwasilisha hasara hiyo ni mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Serikali, kwa hiyo tunaisubiri itueleze tunadaiwa nini,” alisema Mukoba.


Usalama wa viongozi wake
Rais huyo alisema CWT kina wasiwasi kuhusu usalama wa viongozi walioshiriki na kuhamasisha mgomo wa walimu.


Alitoa wito kwa Serikali na vyombo vya dola kuhakikisha kwamba viongozi wa chama na wanachama waliohamasisha mgomo wanakuwa salama bila ya kufanyiwa unyama.
“Kiongozi yeyote atakayefanyiwa unyama wowote ule, Serikali itabeba lawama kwa sababu vitisho vilishaanza wakati wa mgomo,” alisema.


Alisema sababu ya hofu hiyo ni kutokana na viongozi kadhaa wa walimu kukamatwa na polisi na wengine kufunguliwa mashtaka mahakamani.


Walimu nchini wanataka nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100, posho ya asilimia 55 kwa walimu wanaofundisha masomo ya sayansi na asilimia 50 kwa walimu wa masomo ya sanaa huku wale wanaofundisha katika mazingira magumu wakitaka asilimia 30.


Dar watii amri
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Shule ya Msingi Shekilango na Sekondari Manzese za Wilaya ya Kinondoni, walimu walionekana kutii amri hiyo ya Mahakama.


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Shekilango, Esther David alisema: “Tumeitikia amri iliyotolewa na Mahakama, tumerudi kazini kama kawaida ingawa leo ilikuwa ni siku ya kufunga shule na hapa shuleni kwangu wanafunzi wanafanya mitihani yao ya kufungia shule.”
Katika Wilaya ya Temeke walimu pia walionekana wakifundisha katika Shule za Mabatini, Temeke na Madenge.


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Makamba, Anastazia Mapembe alisema: “Walimu walikuja asubuhi na kuondoka. Kwa sasa darasa la kwanza na la sita wamefunga shule na darasa la saba itabidi warudi Jumatatu kuendelea na masomo katika maandalizi ya mitihani yao ya kumaliza.”


Mtihani maalumu wa darasa la saba katika Shule za Msingi Manispaa ya Temeke umeahirishwa mpaka Jumatatu kutokana na mgomo huo.


Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi katika shule za msingi za manispaa hiyo walisema mgomo huo haukuwaathiri sana kwa sababu ulianza siku za mwisho karibu na kufunga shule.
Akizungumza mgomo huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alisema tabia iliyoibuka hivi sasa ya vyombo vya dola kutumia nguvu kudhibiti migomo, maandamano ni uvunjaji mkubwa wa Katiba ya nchi.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Kibamba alisema  wananchi wana haki ya kudai maslahi yao huku akisisitiza kuwa hivi sasa kila anayeonekana kuwa kiongozi anafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.


Habari hii imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Badi Mashamba, Zakhia Abdallah, Fidelis Butahe, Halima Shebuge na Victoria Mhagama


Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa