Home » » DCB YAPEWA LESENI, YAWA BENKI YA BIASHARA

DCB YAPEWA LESENI, YAWA BENKI YA BIASHARA

Na Gabriel Mushi, Dar es Salaam

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa rasmi leseni mpya ya biashara kwa Benki ya Wananchi wa Dar es Salaam (DCB) na kuifanya kuwa benki ya biashara.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi wa DCB, Paul Rupia, alisema hatua hiyo itaiwezesha benki hiyo kupanua wigo wa kibiashara nje ya mkoa huo.

Alisema kutokana na hatua hiyo, wananchi wa Dar es Salaam wasiwe na wasiwasi kwa kuwa huduma zitaendelea kutolewa kama kawaida kulingana na madhumuni ya uanzishwaji wake.

“Mtakumbuka ya kuwa mwanzoni mwa mwaka huu katika taarifa tuliyoitoa kwenu, benki yetu iliweza kupata faida baada ya kodi kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kwa hesabu zilizokaguliwa.

“Moja ya malengo ya benki hii ilikuwa ni kupanua wigo na kujitanua kibiashara kwa ajili ya kuwafikia wateja wengi zaidi, hii ikiwa ni matokeo ya benki yetu kuweza kufikia mtaji unaoruhusu kujiendesha kama benki ya kibiashara.

“Hivyo uongozi wa benki uliomba leseni ya biashara toka BoT kwa ajili ya kuiwezesha DCB kupiga hatua kutoka Community Bank na kuwa benki ya biashara.

“Kutokana na jitihada hizo, sasa BoT imetoa rasmi leseni mpya kwa benki yetu na hivyo kuifanya rasmi kuwa benki ya biashara.

“Ikumbukwe kuwa lengo la kuanzishwa kwa benki hii ilikuwa ni kuwasaidia wananchi wa Dar es Salaam ambao walikuwa hawawezi kupata huduma za kibenki toka katika benki za biashara,” alisema Rupia.

Alisema pamoja na DCB kupata leseni hiyo na kuwa benki ya biashara ambayo itaruhusu kufungua matawi nje ya Dar es Salaam, dira na dhima ya benki hiyo itakuwa ni ile ile na kuongeza wigo mkubwa kwa wateja wake.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Edmund Mkawa, alisema mwezi ujao wanatarajiwa kufungua tawi jipya Chanika.

“Kwanza tutahakikisha tunaendelea kuongeza matawi hapa Dar es Salaam kutoka matawi matano ya sasa hadi kufikia 10, ndipo tuelekee mikoani kufungua matawi.

“Hata hivyo, tunatarajiwa kuongeza tawi kule Chanika mwezi ujao huu ukiwa ni mkakati ambao utaendelea kuwasaidia wananchi wa vipato vya kati na chini kabisa wa mkoa huu na ndio maana tunawataka wasiwe na wasiwasi katika hili,” alisema Mkawa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa