Home » » FERI SASA KUINGIA KWA VITAMBULISHO

FERI SASA KUINGIA KWA VITAMBULISHO

Na Oliver Oswald, Dar es Salaam


UONGOZI wa Soko la Samaki (FERI)umeanzisha utaratibu mpya wa kutoa vitambulisho kwa wafanyakazi na wafanyabiashara wote wa soko hilo ili kuimarisha usalama.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa soko hilo, Rajabu Mng’oi alisema,utaratibu huo utasaidia kuwakamata baadhi ya watu wanaoingia ndani ya soko hilo kwa lengo la kufanya uharifu.

Alisema kutokana na wingi wa watu wanaoingia na kutoka ndani ya soko hilo, wamelazimika kutoa vitambulisho hivyo, ili kupata urahisi wa kuwabaini na kuwatambua watu wanaoenda kinyume na kanuni za soko hilo.

“Vitambulisho hivyo vitatusaidia kwa katika utendaji wa kazi zetu za kila siku, tutawatambua wafanyakazi wetu wanaofanya kazi ndani ya soko hili,”Alisema Mng’oi.

Mng’oi alilalamikia utekelezaji mbovu wa miundombinu ya soko hilo kwa kutofanyiwa ukarabati kwa kipindi cha mda mrefu.

“Nilishaletewa malalamiko na wadau wa soko kuwa wanatumbukia kwenye mashimo ya chemba ambayo hayana mifuniko na kusababisha baadhi ya watu kupata majeraha ya muda mrefu,”Alisema Mng’oi.

Alisema kutokana na utekelezaji hafifu wa miundombinu iliyopo katika soko hilo, baadhi ya wafanyabiashara hawatii sheria na kanuni zilizowekwa na uongozi wa soko hilo.

Aliongeza kuwa, kwa sasa hali ya soko ni nzuri na aliwataka watumiaji wa soko hilo kuacha mazoea ya kutupa taka ovyo kwani sifa ya biashara ni usafi na ubora wa bidhaa.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa